musicarlito
Senior Member
- Dec 29, 2020
- 189
- 307
NAWATUKANA VIJANA WOTE WA AFRIKA
(Sehemu ya kwanza)
Najua, najua, tena najua sana kwamba kwa kusoma tu kichwa cha makala hii, watanyanyuka vijana watakaohamaki kunitukana hata pasipo kusoma kwa kina makala hii. Yaani pasipo kujua mada inahusu nini na hoja imejengwaje, watakurupukia mwendo wa tusi kwa tusi. Haya, hayo nimeyazoea. Kama ni kupambana nataka nipambane na vijana wote wa Afrika kifikra. Katika yote, nagombea fikra mbadala barani mwetu.
Katika muktadha huu, kwa makala hii nawalenga kwa makusudi vijana wote wa Afrika wanaoamini kwamba “AFRIKA TUNA WATU”, yaani kwamba “tuna wachawi wenye nguvu zisizomithilika za kutendea maajabu”. Na kama kuna watu wazima na wazee wao nao pia nataka niwatukane. “Kuwa na watu” kwa maana ya kuwa na mabingwa wa ulozi ni msemo uliozuka miezi si mingi iliyopita katika duru za kandanda.
Nisikilizeni vyema enyi vijana! Eti nyie vijana, hivi majuzi zimepokelewa ndege mbili mpya huko Zanzibar. Mlifurahi na kuandika kwa namna mbali mbali kwenye mitandao. Vyema! Lakini kwangu kila zinapopokelewa ndege mpya siachi kuuliza umma wa Waafrika: Hivi watu wetu wanaoitwa “wachawi” wanafanya nini? Au wako wapi? Hivi kwa nini haitokei siku fulani watu hao wakawaalika na kuwakabidhi viongozi wetu fisi wapya, nyungo mpya au vipembe vipya kwa ajili ya maendeleo ya wizara ya uchukuzi na mawasiliano na pesa zinazotumika kununulia ndege Ulaya kutoka Kanada, Marekani au Ufaransa zikatumika kujengea madaraja, kutafutia chanjo za kwetu za UVIKO 19 na malaria, kujengea hospitali na shule, kuchimbia visima na kadhalika?
Wako wapi basi watu wetu? Hivi kwa uwezo wao wasingeliweza kubuni usafiri wa gharama nafuu tukanufaika sote? Kwa uwezo huo wakashindana na kampuni za teknolojia za ndege kama Boeing, Airbus na Bombardier pamoja na kampuni za teknolojia za magari, kama vile, Toyota, Suzuki, Tata, Mercides Benz, Fiat na kadhalika? Waafrika tungekuwa matawi ya juu kabisa. Tunafeli wapi? Za nini hizi gharama za kujengea miundo mbinu tunayoweza kukwepa? SGR ya nini? Barabara za lami za nini? Kujenga bandari na magati kwa nini? Kujenga meli na vivuko kwa nini? Hivi kwa fisi wadogo wadogo, nyungo ndogo ndogo na vipembe vidogo tusingeliwezeshwa kuwa na magari madogo, dala dala, boda boda na kadhalika tukanunua sote na hivyo tukajipunguzia dhiki ya kutembea kwa miguu, kuomba lifti na kubeba mizigo vichwani au migongoni kama punda na ng’ombe?
Nina hakika faida zingelikuwa nyingi kupita maelezo. Hivi kwayo “wachawi” wenyewe wasingelijipatia tuzo la NOBEL katika Fizikia na pia kulipatia heshima bara letu kwa kutuondolea aibu ya kuwa bara linalouziwa vitu mbalimbali “used” (mitumba): magari, baiskeli, suruali, mashati, sketi, chupi na hata sidiria? Tusemeje? Tuseme hao“wachawi wetu” hawajui kwamba kuna tuzo nono ya NOBEL, tuzo inayoambatana na kitita kikubwa sana cha pesa? Au huu ndio ushahidi wa kutokuwapo kwao kati yetu?
Waafrika tu Wajinga Sana
Ashkum si matusi, leo nawatukana vijana wote wa Afrika lakini baadaye nitajiingiza mwenyewe na wazee wenzangu. Sisi Waafrika ni wajinga sana, ukitaka kuongeza ni wapumbavu sana, ruksa! Atakayenilalamikia kwa tusi hili shauri lake. Lakini ninachotaka kumaanisha ni kwamba kama kweli “TUNA WATU TUNALIA NINI?” tunalilia nini taabu za usafiri na mawasiliano, ajira, mitaji, njaa, maradhi na hata vita? Nifuatilie katika tusi langu.
1. Kama kweli “SISI TUNA WATU” tunalia nini na taabu ya usafiri? Si tuunde makampuni yetu ya usafiri wa fisi, nyungo, mikeka na vipembe? Tunasimuliana mambo ya kuruka usiku kwa spidi ya kufumba na kufumbua. Hata hivyo, tunaruka wapi na tunakwenda wapi? Si siri, wenzetu siyo tu wanaruka hapa duniani wakitoka bara moja kwenda lingine kwa ndege zao za BOENG, BOMBARDIER, AIRBUS na kadhalika, wanarusha pia roketi na roboti kwenda sayari za mbali, kama vile, Mars, Jupiter na kadhalika wakitafuta sayari ya kuhamia watuache sisi tukicheza singeli hapa duniani! Kwa mradi huu, nchi kama Marekani ina bajeti kubwa kwa matumizi huko NASA (kituo cha mambo ya anga, California) siyo kama sisi ambao hata bajeti ya kilimo inachekesha. Vivyo bajeti wanazo Urusi, China, Umoja wa Ulaya na hata India.
Sasa vijana wapendwa mnaoamini uwapo wa uchawi mu wapi? Wengine wenu mu wabunge na mawaziri katika nchi zetu za Afrika. Lakini kama mambo ya kwenda kwenye anga za juu yanatushinda si tuwatumie watu wetu kutuboreshea haya yanayotuzunguka tuishi vizuri? Katika hayo makubwa tunayosema na kuamini pasipo kutendea vitu vya kuboreshea maisha yetu wenyewe, tunamdanganya nani, tunajidanganya wenyewe au tunawadanganya Wazungu?
Wamerikani wametuma roboti “curiosity skycrane” kwenda Mars, Wahindi wametuma huko “mangalian”, Wachina wametuma chombo chao, nchi za Umoja wa Ulaya wametuma chao, Umoja wa Nchi za Kiarabu wametuma chao, sisi watu weusi vipi? Si tutume basi fisi, nyungo au vipembe huko angani? Lakini we, thubutu yake! Fisi ataweza kuingia katika anga za juu, nje ya dunia? Ah, atakufa mwenyewe kwa baridi na kukosa hewa! Yaani atakufa kwa matatizo ya kupumua! Ha, ha, ha, ha, ha! Nacheka kama mazuri vile! Eti wakipata sayari ya kukaa, nao wakagawana vipande vya ardhi, tutajitokeza Waafrika kuomba ardhi au tutalalamika kwenye vyombo vya mataifa kwamba tunatunyimwa maeneo. Ebo! Kazi wafanye wao wakati sisi tulikuwa tukicheza singeli na kujigamba kwa maneno matupu kwamba tunaruka kwa fisi, nyungo na vipembe tu! Watugawie sisi ardhi kwa sababu gani hasa?
Kama tunabishana juu ya haya, basi siyo tu tuwatume fisi katika sayari hizo za karibu, bali tuwahi kuwatuma kwenye sayari inayoitwa SUPER EARTH, yaani sayari iliyogunduliwa katika karne za hivi karibuni, sayari inayoonekana kwa vyombo vikali vya kutazamia vitu angani, sayari inayoonekana kuwa na ukubwa mara mbili ya ukubwa wa dunia yetu, sayari yenye hali inayoonekana inaweza kuwezesha kuwapo uhai, isipokuwa kwa vile ilivyo umbali wa miaka 111 ya spidi ya mwanga, Wazungu wamefeli kuwa na teknolojia ya kupelekea chochote huko. Wenyewe wanajipa moyo na matumaini kwamba katika miaka laki saba ijayo watapata utaalamu na teknolojia ya kupeleka chombo huko na hata kuwapeleka wanadamu.
Je, hapo hapana fursa kwa “wachawi wetu” wa Tanga, Sumbawanga, Shinyanga, Sumbawanga, Mkuranga, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe, Afrika ya Kusini, Nigeria, Uganda, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Camerooni na kadhalika? Si tuwahi sisi basi na fisi wetu, nyungo zetu au vipembe vyetu? Si twende huko tukajikatie viwanja bora kuliko kutafuta viwanja Vingunguti, Ilemela, Kisasa, Ngaronaro, Uyui au Mbalizi? Lakini, thubutu yake! Hatuna ubavu huo!
Mnanibisha? Basi, nina habari nyingine. Sisi tunatafuta na kujivunia sana vitu na vyombo vya kigeni. Lakini vijana wetu wasingelijivunia kununua “vitu vya kwetu”: fisi, nyungo au vipembe? Watu, hasa vijana, wasingelipiga picha za fahari na kujidai na fisi wetu, nyungo zetu au vipembe vyetu? Tusingeliona fahari kutuma picha zetu kwenye Facebook, Instagram na mitandao mingine kama hiyo? Hivi vijana wetu na mastaa wetu, kama akina Daimond, Harmonize, Alikiba na wenzao wasingelishindana kununua fisi, nyungo na vipembe vya dizaini mbalimbali na matoleo yake mapya badala ya kushindana kununua ndege na magari ya gharama kutoka Uingereza, China, Japan au Ujerumani?
Si hivyo tu, hivi kwa mitindo mbali mbali ya usafiri kutoka kwa watu wetu, maaskofu, mapadre, wachungaji na masheikh tusingelipata nafuu ya usafiri wa aina yake badala ya kupigiana kelele za harambee kwenye nyumba za ibada tuwezeshwe usafiri wa magari au pikipiki? Je, kwa kurahisishiwa usafiri hivyo, tusingeliweza kufanya uchungaji , kueneza neno la Mungu na kusambaza maadili ya kidini kwa urahisi tukapata sote uzima wa milele kwa urahisi?
Walioajiriwa kama mawaziri, manaibu mawaziri, madaktari, wahandisi, walimu wasingepata usafiri rahisi kuliko kutumia mishahara yao kulipia usafiri wa kwenda na kurudi kutoka kazini? Tungelihitajije mafuta kwa vyombo vyetu vya usafiri vya binafsi? Tusingelijipatia nafuu ya maisha wenyewe?
2. Sasa wenu vijana mnaotafuta kazi na wakati huo huo mnaamini kwamba TUNA WATU. Kama kweli “SISI TUNA WATU” vijana mnalia nini tatizo la ajira? Tatizo la ajira linatushindaje kulitatua? Hivi wachawi wetu wakianzisha boda boda za fisi, nyungo na vipembe tusingelimaliza tatizo la ajira kwa urahisi wa ajabu? Kuna vijana watakaonibisha wakati hawana ajira. Wanaamini kwamba kuna wachawi nao wana uwezo mkubwa sana. Sasa kwa nini ninyi vijana hamkazani wachawi hao wawetengenezee ajira? Kwa nini mnatazama mama Samia Suluhu Hassani au Mohamed Mo ajenge viwanda aajiri vijana? Kwa nini basi msiwaambie wazazi, jamaa na babu zenu wachawi waanzishe makampuni ya kusafirisha watu kichawi muwe marubani wake? Mnalia nini?
Enyi vijana wapendwa, hususan ninyi mnaotembea na vyetu kuomba kazi, kama mnaamini “kuna watu”, magwiji wa “mitikongo” kwa nini wasiwawezeshe kupata ajira kwenye makampuni makubwa yanayouza bidhaa za kieletroniki, kama vile, Apple (California, Marekani), Samsung (Korea ya Kusini), HP (Marekani), Microsoft Corporation (Marekani), Hitachi (Japan), Sony (Japan), Panasonic (Osaka, Japan), Toshiba (Tokyo, Japan), LG Electronic (Korea ya Kusini) na Intel (St. Clara, California, Marekani)? Watu hao wana uwezo gani? Kwa nini mtafute ajira ndogo kama za udereva wa Fuso za kusomba ndizi mzuzu na mpunga kutoka Ifakara? Na si hivyo tu, kwa nini wenyewe hao hao, namaanisha “wachawi” wasiwe wamejipatia ajira bora hata kabla yenu? Mbona hawajawapatia ajira hizo lau watoto wao na jamaa zao? Eti vijana, sasa mnaamini katika nguvu gani hasa? Ndiyo kisa basi nawatukaneni wote.
Tuendelee. Au mnaliaje habari ya kukosa mitaji? Kwa nini vijana mtazame macho yenu benki au “sakosi?” mnachezaje vikoba au mnakwendaje kubeti mpira? Si mwaambie wazazi, jamaa na wazee wenu wenye chuma ulete wakatumbukize kwenye benki za Uingereza, Ujerumani au Urusi noti zijae za majumbani kwenu mfungue “supermarkets?” Vijana wa vyuoni mnaoamini uwapo na nguvu ya uchawi mnashindwaje kulipa ada au mnapiga pasi ndefu na kusubiri boom au mikopo wakati labda wazee wenu wana vyuma ulete? Hawawezi kutumia vyuma hivyo kuwaibia pesa China na Japani mwishi pasipo dhiki? Mnachoamini kina ukweli gani na faida gani? Watu tunaamini uwapo wa nguvu za ajabu wakati tunapata taabu? Jambo hili si ujinga?
Tunafeli wapi Waafrika? Kwa nini hatuna ajira, hatuna mitaji, hatuna hiki na kile? Hivi huu si ushahidi wa kujidanganya kwetu?
Lakini tunapodai tunaweza hili au lile, hatulingani na watoto ambao katika kushindana kwao huweza kusema uongo: “Baba ana pesa nyingi, ana nyumba mjini au anataka kununua gari” kwa uongo tu huku wakitaka kuwakoga na kuwashinda watoto wenzao tu?
Tukiona ndege Ulaya zinatua kwenye viwanja vyetu vya ndege hatuoni haya ya uso? Eti pamoja na kuziona ndege za kweli bado tunajificha kwenye imani zetu za kale kwamba tuna watu wetu wanaoruka usiku kwa ndege zetu wenyewe. Kituko hiki nakifananisha na kiroja cha mtu kuwaona watu wanakula pilau naye kuwaambia watoto wake wasihangaike kwani kwao kuna watu wanakula vizuri usiku. Au kituko cha mtu kuwaona watu wamevaa vizuri naye kuwatuliza watoto wake wasihangaike kuyatamani mavazi hayo maana kwao kuna watu wanavaa vizuri usiku. Ha, mimi hapa nauona utoto fulani.
Mzee wenu Pd. Titus Amigu. ITAENDELEA.