Unapoangalia Moto unavyoteketeza Mali za watu binanfsi na za umma kwa kukosekana kwa Magari ya zimamoto, unajiuliza ni kwa nini tulitumia fedha nyingi sana kununulia Magari ya maji ya kuwasha badala ya Magari ya Zimamoto ambayo ni ya muhimu zaidi kwenye maisha ya kila siku ya watanzania.
Inapokuwa Mgonjwa (Baraka Elias Mashauri) inashindikana kutibiwa Kwenye Hospitali ya Taifa Mhimbili kwa kukosekana vifaa vya kusaidia kupatiwa tiba, unajiuliza ni kwa nini fedha vya kununulia vifaa hivyo inakosekana ila serikali inazo fedha za kununulia Mashangingi.
Ukiangalia kuanzia utungaji wa sheria, mikakati ya kimaendeleo, mipango ya kiuchumi, na mambo mengine mengi ambayo mwisho wa siku taifa linapata hasara, wali la msingi ni nani hasa anaweka vipaumbele vya taifa letu? Inakuwaje tunatangatanga kama wana Israel walivyokuwa wanatangatanga Jangwani kwa miaka 40 mahali walikoweza kufika kwa siku arobaini tu?
Jamani Watanzania wenzangu mbona sisi tuna hii hulka ya kutegemea mtu mwengine (serikali au mfadhili) kutufanyia hata kile kilichopo ndani ya uwezo wetu?
Upinzani unaweza kutusaidia sana kwa kufanya vitu vya kuigwa nchi nzima.
Mifano:
1. Zimamoto
Kwa nini kwenye majimbo na mitaa ilioko chini ya upinzani wasiunde vikosi vya zimamoto wa kujitolea (hawalipwi) wawe zimamoto wa mtaa, kijiji, au mji.
Wabunge, madiwani, na viongozi wengine wa sehemu hizi wanaweza kutoa posho zao, sehemu ya mishahara yao, n.k. kuchangia kunua magari na vifaa vingine vya zimamoto. Hapa pia tunaweza kuwaomba wafanyabiashara wa sehemu hiyo kuchangia.
Hii italifanya jukumu la zimamoto kuwa la jamii ya hilo eneo na sio jukumu la serikali.
2. Vifaa Hospitalini
Hapa pia viongozi wa upinzani wanaweza kutoa mfano. Katika majimbo yao wanaweza kuanzisha mfuko utakaochangiwa (kwa hiyari) na watu wote pamoja na biashara za eneo hilo ili kuweka vifaa muhimu katika mahospitali yao.
Mambo makubwa kama majengo, mashine za bei mbaya, n.k. vinaweza kutolewa na serikali. Lakini kuna vifaa vingi muhimu vinavyoweza kununuliwa kwa kutumia huu mfuko.
Tusiisubiri serikali kwa kila kitu jamani. Badala ya kuilaumu serikali kuwa haifanyi hiki au kile, mambo mengine tunaweza kufanya wenyewe kama tuna uongozi mzuri.
Hapa upinzani unaweza kuonyesha mfano wa kuigwa. Mnataka kupata kaulimbiu wakati wa uchaguzi mkuu, fanyeni haya.
Vipaumbele tunaviweka sisi wananchi ambao ndio tunaofaidika na hayo mabadiliko na sio serikali. Tukionyesha ni kipi cha muhimu kwetu, serikali itafuata. Tunahitaji mtu atuongoze. Hii ni kazi muhimu kwa upinzani.
Upinzani, show your leadership please na sio kupinga, kulaumu au kukosoa serikali tu.