SoC04 Nafasi ya wananchi kukua kwa maendeleo ya nchi

Tanzania Tuitakayo competition threads
May 23, 2024
15
43
Tanzania tuitakayo inahitaji watu wanaokua.

Mdumao wa karne kwa karne wa Afrika sio kosa letu. Simaanishi tupo tulipokuwa, ila tunajongea kwa mwendo wa kinyonga ukilinganisha na mataifa kwenye mabara mengine. Tunadumaa kwa sababu dunia inaogopa tukifunguliwa tutakuwaje.

Nchi kubwa kama Tanzania imewahi fanya tathmini juu ya mfumo wake wa elimu? Serikali au taasisi binafsi zimewahi kukusanya takwimu na kufanya uratibu wa uwezo/kiwango cha juu cha kufikiria cha mtanzania(IQ) kama jibu ni ndio sina tatizo kama ni sio, hapa nina swali moja, Taasisi ya elimu ina uhakika gani kama mfumo wa elimu inayotolewa kwa watanzania inaendana na uhalisia na uwezo wao?

Sisi tuliosoma shule za uma tunaelewa ubadhilifu kwenye mitihani ya taifa/ mchujo kuisha sio kazi nyepesi. Shida kubwa hapa ni kwamba, kuna watu uwezo wa darasani hawana ila kwa kulazimisha na kulazimishwa wanakuja kugharamikiwa na serikali kusomeshwa vyuo ili waje wafanye kazi walipe deni la serikali.

Je, wizara imewahi fanya tathmini ni watu wangapi hufa bila hata kuanza kulipa madeni hayo? Ni mabinti wangapi na elimu zao za vyuo waliishia kuolewa na kuishi hadi kuzeeka bila kulipa mikopo yao ya chuo?

Ni wanaume wangapi wamezeeka na mwiso kufariki kwa kuunga unga pasi na ajira ya kuwaweka kwenye mfumo wa kuweza kulipa mikopo yao ya chuo?

Kwa maswali haya machache ya kufikirisha natamani Serikali na wizara husika ya elimu iwape watanzania kitu nilichokiita mimi....

NAFASI YA KUKUA.
Naiomba serikali yangu tukufu ikishirikiana na wizara ya afya na ile ya elimu, ifanye kampeni mahususi kabisa ya uchunguzi na ufanyaji tathmini wa AKILI' za watoto walioko mashuleni hivi sasa. Wapo wataalamu na dunia ni wazi sana zama hizi, vipo vifaa maalumu vya kupima uwezo wa akili wa mtu.

Lakini mbali na hilo, tangu huku chini, shule ya msingi watoto wapewe uhuru wa KUTANUA MBAWA ZAO.
Kuna watoto uwezo wa darasani hawana, ila wana vipaji vikubwa vinavyoweza kuibadili taswira ya Afrika duniani. Watoto wapewe nafasi ya kukua kulingana na uwezo walionao. Namaanisha....

Kuwe na karakana shule kwanzia ya msingi. Mtoto apewe elimu ile ya msingi ya darasani ila apewe nafasi ya kujifunza kile kitu anachokipenda zaidi maishani. Akihitimu shule ya msingi, badala ya kupoteza muda kwenye sekondari ambayo haitomsaidia, akulie kwenye kupata weledi wa ile taaluma aipendayo. Wenye uwezo wa kitaaluma wapewe nafasi lakini pia wafunzwe stadi za maisha.

Utafiti wangu mdogo usio rasmi umebainisha hakuna watu wavivu makazini kama wale waliosoma kwa starehe (waliokaririshwa) changamoto ya watu hawa, nje ya makaratasi hawana kingine cha kuongeza thamani kwenye elimu yao kubwa.

Ufanyike upya utathmini wa mtaala wetu wa elimu. Acha zirejee zama za walimu ni wito. Udakitari ni wito. Uhudumu ni wito. Zama hizi haziwezi kuja kama watoto wataendelea kukaririshwa na kulazimishwa kusomea fani yenye ajira ya uhakika wasiyoipenda ni wazi elimu itazidi kudumaa na sekta zote nyeti zitajaa uozo na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Nchi inayokua kila leo na kuendelea, inahitaji wanataaluma wanaozipenda taaluma zao.
Ukitembelea shule za serikali, hospitali za serikali utaelewa nini nasema. Watu wanafanya kazi ili wapate mshahara na sio ili wahudumie. Hakuna wito na kama wito haupo basi hakuna ukuaji.

Hebu jaribu kufanya tafiti juu ya watu wanaojiita "Memes Lords" watengenezaji wa vituko maandishi vya mitandaoni, utabaini zaidi ya kile nilichobaini mimi. MTANZANIA AKIPEWA NAFASI NA UHURU WA KUKUA, DUNIA ITAISHANGAA HII NCHI.

Mtu anayeweza kubadilisha chochote kuwa utani ni mtu anayeweza kubadilisha utani kuwa maisha. Inahitajika jitihada ya ziada kufanya taifa likue.

NINI KIFANYIKE?

Serikali yangu tukufu, ichague hii nchi kuishi kama nchi huru. Iruhusu watu kutoa maoni chanya juu ya swala zima la elimu ya mtanzania. Ifanyike tafiti ili uwezo wa mtanzania ubainishwe. Elimu ya utambuzi binafsi iwekwe kwenye somo la haiba. Elimu hii ilenge kutoa ule uwezo wa ndani wa mtoto/mtu ili uwe fursa. Mbali na hapo, kampeni ya huduma ni wito ifanyike. Kuna wamama hufariki ama kupoteza watoto wakati wa kujifungua shauri tu, wamekutana na wale ma Daktari waliolazimishwa kusomea udakitari ili wapate ajira.

Kuna wanafunzi wanakuwa na matunda mabovu ya masomo yao kwa sababu ya upuuzaji wa walimu wa shule za serikali. Kuna wakati natamani, walimu wa serikali wangepewa amri ya kusomesha watòto wao shule za serikali labda ingeamsha mori na jitihada za ufundishaji.

MAENDELEO YA NCHI YOYOTE, YANAHITAJI SANA MAENDELEO YA RAIA WAKE.

HAKUNA MAFANIKIO PASIPO NA UKUAJI.
 
Naiomba serikali yangu tukufu ikishirikiana na wizara ya afya na ile ya elimu, ifanye kampeni mahususi kabisa ya uchunguzi na ufanyaji tathmini wa AKILI' za watoto walioko mashuleni hivi sasa. Wapo wataalamu na dunia ni wazi sana zama hizi, vipo vifaa maalumu vya kupima uwezo wa akili wa mtu.
Dada umewaza nn!! Unahisi tuna mzigo mzito kuliko uwezo.... anyway utafiti utatuambia majibu.

Nchi inayokua kila leo na kuendelea, inahitaji wanataaluma wanaozipenda taaluma zao.
Ukitembelea shule za serikali, hospitali za serikali utaelewa nini nasema. Watu wanafanya kazi ili wapate mshahara na sio ili wahudumie. Hakuna wito na kama wito haupo basi hakuna ukuaji
Kweli mwanangu, kila kazi tu iwe na maslahi ya kuruhusu anayeifanya kwa wito kufaidika vema.
 
Back
Top Bottom