Na tujenge miundombinu kwanza kuweka misingi imara ya taifa

Egnecious

JF-Expert Member
Jul 8, 2015
875
960
Heri ya Mei Mosi Watanzania wenzangu. Bilashaka tumesherehekea vema siku hii muhimu ya wafanyakazi duniani.

Binasfi nimeona nichangie maoni yangu kwa siku hii kuwa ni HERI TUJENGE MIUNDOMBINU YETU KWANZA iwe imara sana kwaajili ya kuweka misingi thabiti ya uchumi endelevu kwa Taifa letu ili kumudu kuhudumia kizazi cha sasa na vile vijavyo.

Nipende kujipambanua kuwa nami pia ni mfanyakazi na kwahiyo ninaposema haya naomba kutoeleweka kuwa huenda mimi ni wa tabaka tofauti na wafanyakazi.

Kwa juu juu nimejaribu kufikiria mapato ya Taifa letu sambamba na matumizi ya sasa ya fedha hizo ndipo nikadhani niseme kwa ufupi kwamba sisi kama Watanzania na tuvumilie pia turidhike na hali ya vipato ya sasa ili kupitia aina hii ya hisani zetu kama wafanyakazi Wazalendo tuendelee kusaidia KAZI NYETI za UJENZI wa Miundimbinu ya Taifa letu ambayo ndo muhimili mkubwa kwa uchumi wetu na yamkini kwa muda mfupi ujao tutaanza kuvuna matunda yake.

Ninapoona miradi mikubwa sana ya barabara za lami zinazounganisha mikoa yetu yote zikijengwa na kukarabatiwa..

Ninapoona ukarabati wa barabara za vijijini ktk ubora wa hali ya juu..

Ninapoona ufufuzi wa kasi sana wa shirika letu pendwa la ndege (ATCL)..

Ninapoona ujenzi na uimarishaji wa bandari ya Darisalama na zinginezo..

Ninapoona ujenzi wa vivuko vikubwa vya majini ktk maziwa yetu nchini..

Ninapoona ujenzi wa miradi mikubwa ya uzalishaji na usambazaji umeme nchini kote vijijini na mijini...

Ninapoona ujenzi wa SGR ambayo ina ubora wa kimataifa..

Ninapoona mikopo ya elimu ya juu ikitolewa sambamba na elimu bure kuanzia shule za msingi na sekondari..

Ninapoona timizo la azma ya uhamishaji wa Makao Makuu ya Serikali kuja DODOMA unaoambatana na ujenzi wa soko kubwa Afrika Mashariki na Kati pamoja na uwanja bora wa mpira wa miguu zaidi ya ule wa Darisalama..

Ninapoona udhibiti mkali ktk baadhi ya vyanzo vikuu vyetu vya kodi kupitia TRA na agency zake..

Nionapo usimamizi na udhibiti wa rasilimali muhimu za Taifa mf. Madini, wanyamapori, misitu nk..

Ninapoiona kwa macho vita kali inayopigwa dhidi ya rushwa na ufisadi nchini..

Ninapoona mengi mikoani yanayosimamiwa na Serikali hii ya Awamu ya Tano..

Sina shaka wala maswali kuwa muda mfupi ujao Tanzania itakuwa nchi ambayo tutajitoa kuwa miongoni mwa nchi ombaomba duniani na hivyo kumudu kujisimamia kwa kujiamini ktk mambo ya msingi na hasa kiuchumi, kijamii na Kisiasa na hivyo kujijengea heshma miongoni mwa mataifa ya dunia.

Ni dhahiri kwamba mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe, yaani mkulima, wewe mfanyakazi na pia mfanyabiashara kupitia kodi na uzalishaji mbalimbali unaofanywa na tabaka hizo.

Ni dhahiri kwamba TRA na Mamlaka zake za kodi zimejitahidi sana kukusanya kodi ambazo ndio chanzo kikuu cha mapato ya kuwezesha utekelezaji wa miradi muhimu sana tunayoiona ktk Taifa letu ikitekelezwa hadi sasa.

Hata hivyo bado ninadhani kuna maeneo mengi sana ambayo hayajafikiwa ili kukusanya kodi kwa ajili ya kuiongezea mapato Serikali yetu ili kuiwezesha kutoa huduma bora kwa jamii nzima ya Watanzania.

Mathalani, mazao ya kilimo na wafugaji, bidhaa za maduka ktk vijiji vyote Tanzania nzima ambako idadi kubwa takribani 80% ya Watanzania wanaishi kule nk.

Kwa kuangalia mtazamo huo wa eneo kubwa la kodi isiyokusanywa kwa kila mwezi ni jambo lililo bayana kuwa Serikali inahitaji sana ushirikiano wetu sote kama Watanzania ktk kuelimisha, Kuhamasisha na kukusanya kodi kwa uaminifu ili kufikia malengo ya Ujenzi wa Uchumi Imara wa Viwanda sambamba na kuboresha maslahi ya Wafanyakazi wa Umma na huduma zinginezo muhimu ktk jamii yote.

Ipo haja ya elimu na hamasa ya kodi kuanzia ktk ngazi ya familiya.

Si jambo baya kuwaelimisha hata watoto wetu majumbani na mashuleni umuhimu wa kulipa kodi ili watumwapo madukani na hata sokoni waweze kudai stakabadhi halali ili kusaidia kuwajengea utamaduni wa kutokukwepa kodi pindi wakiwa watu wazima.

Na pia kwa kufanya hivyo sina shaka kunaweza saidia kuongeza asilimia za makusanyo yetu ya ndani.

Hatuna wajomba wa nchi watakaoendelea kutuhisani kwa umri huu tuliofikia wa miaka karibu 60 tangu tupate Uhuru wetu.

Tukiendekeza kutegemea hisani za mataifa mengine ipo hatari kubwa ya kujikuta tumeuza Uhuru wa milki ya nchi yetu.

Baba wa nyumba ana heshma kubwa anapoitunza familiya yake kwa jasho lake badala ya kumtegemea jirani yake kumhisani hadi nguo za watoto na mkewe.

Ikitokea hisani pana hivyo si ajabu ndoa ikaingia tafrani endapo baba-hisani yaani jirani akiamua vinginevyo.

Tuweni macho ndg zangu Watanzania! Tujidhatiti ktk kujenga nchi kwa jasho letu! Mmenielewa?

Niseme tu kwamba nchi ambazo leo tunaziita wahisani zina mifumo imara ya uzalishaji na utozaji kodi.

Nchi hizi zinaheshimika leo sana kwasababu ya uimara wa Uchumi wao na si jambo jingine.

Na kinachowapa heshma hiyo si miujiza bali walianza miaka mingi sana iliyopita kujenga misingi imara ya uchumi wao.

Mfano mmojawapo ni Korea Kusini ambao takribani miaka 60 iliyopita walikuwa nchi duni ambayo haikuwa na kiwanda hata kimoja cha gari na leo hii ni Taifa imara kiuchumi duniani.

Historia inaonesha kuwa viongozi wao wazalendo waliamua kwanza kujenga upya mindset ya wananchi wao ktkt ya umaskini wa kupindukia.

Wakajitambua na kujiona wao ni ndg na Taifa moja kisha wakaamua kujenga nchi yao ambayo sasa tunaiona.

Ikafikia hatua wafanyakazi walikuwa wakitoa nguvu zao, ujuzi wao na sehemu ya fedha zao za mishahara kwaajili ya kujenga Taifa lao.

Na sasa leo tunaifahamu Korea ilipo! Tujifunze kwao..

Hali kadhalika Taifa kubwa la China mbapo sasa ni Taifa lenye nguvu na kauli duniani.

Historia yao ipo bayana chini ya siasa za Kikomunisti ambapo wao kwa miongo mingi waliamua kuwa na mfumo wa siasa ambazo walizitafsiri na kuzichambua vizuri hadi wakapata zinazowafaa na wakaamua kutofuata kabisa siasa na demokrasia ya mataifa ya magaribi hadi walipojenga uchumi imara.

Kupitia moyo wao wa utaifa na uzalendo wa dhati kwa nchi yao, leo tunajua kuwa China ikiendelea hivi miaka michache ijayo ndo litakuwa Taifa lenye nguvu kubwa kijeshi na kiuchumi duniani.

Mifano ipo mingi sana, Cuba, Urusi (USSR), North Korea, Singapore, India nk.

Watanzania wenzangu, hayupo kiongozi yeyote duniani na hasa Mzalendo anayependa kuona wafanyakazi na wananchi wake wanaishi maisha ya dhiki.

Hebu pia tuufahamu mfano huu mdg ktk ngazi ya familiya kuwa Baba huwa hana ujasiri wala furaha mtaani kwake endapo wanae ni duni na ombaomba.

Fahari ya Baba ni kuona wanae wana elimu bora, afya njema, vipato vikubwa na maisha bora kwa ujumla. Kinyume na hapo kila Mzazi mwenye kujitambua hawezi kuwa na amani wala furaha!

Hali kadhalika Koingozi Mzalendo hawezi jisikia furaha na amani kuongoza Taifa lake ambapo kila wakati nchi yake inabakia kuwa ombaomba na zaidi kila kukicha anona wafanyakazi wana hali duni sana, wakulima na wafanyabiashara wana maisha magumu, na hali kadhalika hospitali hazina dawa wala watumishi wa kutosha, barabara hazipitiki, uonevu na dhuluma kila kona ya nchi nk nk.

Narudia kusema kwamba hakuna kiongozi Mzalendo atakayejisikia faraja kuyaona hayo yametapakaa nchini mwake.

Hii ndio sababu Mh. Rais wetu JPM na Serikali yake amejidhatiti kwa vitendo kuhakikisha tunasogea hatua nyingi mbele Watanzania.

Ni jukumu letu la dhati kumuunga mkono maana ameonesha moyo wa Kizalendo kulijenga Taifa letu Tanzania akiendeleza pale walipoishia watangulizi wake.

Hima tuvute subira na kwa hakika si majira mengi yajayo tutathibitisha mema mengi tuliyoyatarajia.

Niwatakie Mei Mosi njema tena.

Viva Tanzania.

Mr. Golden, F
Makao Makuu Dodoma
 
Back
Top Bottom