Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wa wilaya ya Makete mkoani Njombe na mlinzi wa ofisi za taasisi hiyo wilayani humo, wanashikiliwa na TAKUKURU wakituhumiwa kuomba na kupokea rushwa.
Watumishi hao wanatuhumiwa kuomba rushwa ya Sh 600,000 kutoka kwa mtumishi anayetuhumiwa kughushi vyeti vilivyomwezesha kupata ajira.
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Njombe, Charles Nakembetwa alimtaja mwanasheria huyo kuwa ni Frednand Nsakuzi na Julius Hasani ambaye ni mlinzi wa ofisi ya taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Nakembetwa alisema watumishi hao waliomba rushwa kwa mtumishi huyo ili kuficha ukweli wa taarifa alizohusishwa nazo.
Alisema TAKUKURU kwa kushirikiana na mteja wao huyo waliweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kuongeza kuwa mtego uliotegwa Juni 28, mwaka huu, watuhumiwa hao walipokea Sh 100,000 kama malipo ya awali katika tukio lililofanyika kati ya saa 1:00 na 2:00 usiku.
“Walikamatwa wakati wakipokea kiasi hicho cha fedha kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007,” alisema. Alisema uchunguzi unaendelea na ukikamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.