Uongozi wa Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara,umemvua madaraka ya ualimu mkuu wa shule ya msingi ya Bunda Bw Laurent Augostino baada ya kutuhumiwa kuwachukua wanafunzi wa madarasa ya tano na sita kisha kuwafanyisha mtihani wa upimaji wa kitaifa wa darasa la nne mwaka jana ili kuwezesha shule yake kuongoza katika mtihani huo.
Uamuzi huo umechukuliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri wa Bunda mji Bi Janeth Mayanja,wakati akizungumza na waratibu elimu kata na walimu wakuu wa shule za msingi,ambazo zimefanya vizuri katika mtihani wa kitaifa wa darasa la saba mwaka jana,na kwamba pamoja na uamuzi huo tayari suala hilo limefikishwa katika mamlaka za nidhamu katika idara ya elimu.
Hata hivyo mtendaji huyo mkuu katika halmashauri ya mji wa Bunda,ameagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria baadhi ya walimu walitakiwa kuwalisilisha vyeti vyao,kisha kutoroka vituo vya kazi,na hivi sasa wamebainika kuanza kurejea katika vituo hivyo.
Katika hatua nyingine halmashauri hiyo,imeanzisha utaratibu wa kuwazawadia walimu wakuu wa shule za msingi ambao shule zao zitafanya vyema katika mitihani ya taifa,ili kutoa motisha kwa walimu hao,na hivyo kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi katika mji huo.
Chanzo: ITV