Hospitali ya Taifa Muhimbili imesema kuwa inaendelea kuboresha huduma za afya ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kupitia utaratibu mpya wa madaktari Bingwa kuwaona wagonjwa kupitia Kliniki zilizoanzishwa katika hospitali hiyo.
Mkuu wa Idara ya Huduma ya Wagonjwa wa Nje wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Raymond Mwenesano akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo leo jijini Dar es salaam amesema kuwa utaratibu huo utawasaidia wagonjwa kupata huduma kwa wakati na kupunguza muda kusubiri huduma.
Amesema utaratibu huo utawahusu wagonjwa wote wanakwenda kutibiwa katika Hospitali ya Muhimbili na kuondoka hususan wale wanaolipa fedha taslimu na wale ambao ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bima za mbalimbali za Afya na watumishi ambao makampuni yao yana mikataba na Hospitali kutibu wafanyakazi wao.
Dkt. Mwenesano ameeleza kuwa tayari Kliniki hizo zimekwisha anza kufanya kazi na kuongeza kuwa katika hatua hiyo madaktari Bingwa pekee ndiyo watakaoona wagonjwa wakati wa siku za kazi kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 12 jioni, pia jumamosi kuanzia saa 3 asubuhi hadi za 8 mchana.
“ Muhimbili tumeamua kufanya mabadiliko haya kuanzisha Kliniki na kuwatumia madaktari bingwa peke kwa lengo la kuboresha huduma zetu, awali tulikuwa na Kliniki hizi lakini huduma zake zilikuwa hazitolewi kwa kiwango cha kuridhisha kutokana na kutokuwepo kwa muda wa kutosha wa mdaktari hao kuhudumia wagonjwa” Amesisitiza.
Aidha, amefafanua kuwa wagonjwa wanaopatiwa rufaa kuja hospitali ya Muhimbili wataendelea na utaratibu wa kawaida wa kwenda na Barua za Rufaa ili waweze kupatiwa huduma.