Facebook wamempa zawadi ya dola 10,000 za Kimarekani kijana mdogo wa miaka 12 kama zawadi baada ya kijana huyo kugundua udhaifu kwenye utengenezaji wa app ya Instagram.
Mtoto huyo ni raia wa Finland aligundua kosa kwenye code ya app ya Instagram ambayo inaweza muwezesha mtu mwenye ujuzi wa udukuzi kuweza kufuta ‘comment’ zozote za watu katika app hiyo.
Kijana huyo amepewa dola 10,000 za kimarekani ambazo ni takribani Tsh 22,000,000 | Ksh 1,000,000.
Makampuni makubwa kama Facebook na Google wanautaratibu wa kuruhusu wadukuzi (hackers) kugundua udhaifu wa teknolojia zao na pale wanapojitokeza na kuzionesha basi huwa wanapatiwa zawadi ya pesa.
Kijana huyo amesema kubobea katika fani ya usalama wa kimtandao ndio lengo lake na anahamu sana ya kuja kufanya kazi katika eneo hilo la teknolojia.
Kijana huyu wa Finland ambaye jina lake limefichwa kutokana na ombi la baba yake amekuwa moja ya hackers wadogo zaidi kuwahi kupokea zawadi za kazi ya namna hii. Baba yake amesema kijana huyu na kaka yake wanatumia masaa kadhaa kila siku kuchunguza code za mitandao na huduma mbalimbali kuona kama watagundua makosa. Hii ni mara ya kwanza kwa kupata pesa kutokana na juhudi hizo.
Wenzetu huanza kuwaweka karibu watoto na masuala ya teknolojia mapema zaidi, je unaona mtazamo gani wa hali ilivyo nchini kwetu kutuwezesha kufikia viwango hivi?
Source teknokona