Msiuze maeneo ya wazi - Pinda

May 14, 2024
80
63
Na Joel Magese Moshi

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amewataka Watanzania kuacha mara moja tabia ya kuuza maeneo ya wazi ili kuhifadhi ardhi kwa matumizi ya dharura na maeneo mbadala yanapohitajika.

Mhe. Pinda amesema hayo katika kikao cha wananchi na watumishi wa Ardhi Mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika Septemba 19, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa mkoa huo.

Maeneo ya wazi yana faida kubwa kwa kwa jamii ikizingatiwa hutoa huduma za jamii wakati wa dharura inapojitokeza na kutumika kulingana na mahitaji ikiwamo ujenzi wa vituo vya Afya, maeneo ya biashara na ujenzi wa vituo vya kutolea elimu katika shule mbalimbali.


"Maeneo haya ya wazi niwasihi watanzania wenzangu muendelee kutayatumia kwa vibali vya Mkurugenzi, tutafanyia wapi biashara ndogo ndogo? Kwa sababu hata tukiuza hawa watoto wetu na wajukuu watafanyia biashara wapi? Muungane na mimi maeneo ya wazi tusiweke wazo la kuyauza" amesema Mhe. Pinda.

Mhe. Pinda amelipongeza Baraza la Madiwani la Halimashauri ya Moshi Mjini kwa msimamo wao imara wa kuzuia uuzaji wa maeneo ya wazi.

"Nawashukuru sana Waheshimiwa madiwani mna madiwani wana misimamo thabiti, wamesimama imara baadhi ya maeneo kutoyaruhusu yauzwe, mfano lile eneo la gerage" amesema Naibu Waziri Pinda.

Aidha, Mhe. Pinda amewaonya Maafisa Ardhi wasio waaminifu na weledi kwa taaluma zao na kujihusisha na ugawaji kiwanja kimoja mara mbili na kusisitiza kuwa Wizara itachukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya mtumishi atakayekiuka maadili ya utumishi wa umma kwa taaluma yake.

"Kama litamhusisha Afisa wa kwetu kwenye jambo la kugawa kiwanja kimoja mara mbili, sasa hivi hatunamswalia Mtume tutachukua hatua kali" amesema Naibu Waziri Pinda.

Naibu Waziri Mhe. Pinda yuko katika ziara ya kikazi mkoni Kilimanjaro ambapo mbali na mambo mengine atasikiliza na kutatua changamoto za ardhi kwa wananchi wa mkoa huo pamoja na kufanya vikao kazi na watumishi wa Ardhi mkoani humo.
 
Back
Top Bottom