Msemaji wa Chuo Kikuu cha SAUT ajibu madai ya mfumo wao wa Matokeo kuchezewa na baadhi ya watu, asema upo imara

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
3,807
13,577
Baada ya Mwanachama wa JamiiForums.com kudai kuwa kuna changamoto kadhaa ndani ya mfumo wa Chuo Kikuu cha SAUT (Augustine University of Tanzania - SAUT), ufafanuzi umetolewa.

Mwanachama huyo alidai kuna baadhi ya Watu ambao sio waaminifu wakiwemo baadhi ya Watumishi wa taasisi hiyo wamekuwa na kawaida ya kuingilia mfumo na kuchezea matokeo ya Wanafunzi jambo ambalo anashauri Chuo kiwe makini na kuboresha uimara wa mfumo.

Kusoma zaidi alichoandika Mwanachama huyo, bofya hapa ~ Chuo cha SAUT kishughulikie Mfumo wa Matokeo kuna malalamiko ya chinichini kuwa ‘unachezewa’

UFAFANUZI WA SAUT

Afisa Uhusiano wa Chuo Kikuu cha SAUT, Medard Wilfred anaelezea:

Mfumo wa sasa ni imara (wa SIMS) umeimarishwa tofauti na ule uliokuwa unatumika awali (wa OSIM) ambao ulikuwa na changamoto kadhaa.

Mfumo wa sasa kunapofanyika mabadiliko yoyote ya taarifa za Mwanafunzi itaonekana, hata Vice Chancellor na Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma wataona na watahoji kama kuna kitu kimefanyika nje ya muda sahihi.

Mtu wa IT naye hana mamlaka ya kuingilia taarifa za Mwanafunzi, kazi yake ni kuangalia mfumo upo sawa na kila kitu kinaenda vizuri.

Mwalimu naye anatakiwa kuweka matokeo ya Mwanafunzi ndani ya muda, inapotokea nje ya hapo lazima kuwe na sababu ya kufanya hivyo.

Pia, inapotokea Mwanafunzi ana changamoto ya matokeo kwenye mfumo kuna Kamati ya Nidhamu ambayo anaweza kuwasilisha malalamiko yake na yakafanyiwa kazi ili kama ni makosa ya kibinaadamu basi itajulikana.

Mfano kuna Wanafunzi ambao walitakiwa kuhitimu hivi karibuni, baadhi yao alama zao zilikuwa hazionekani kwa kuwa walikuwa na mitihani ya marudio, sio kwamba alama zao hazikuwepo ila Mwalimu akisahihisha kuna kujaza fomu maalum ambayo anaitumia kuwasilisha matokeo ya Wanafunzi.

Mbali na hapo mwanafunzi anaruhusiwa kukata rufaa anapoona kuna vitu havipo sawa kwenye matokeo yake na hayo yote anafanya kwa njia ya mfumo, akiwasilisha taarifa yake inakuwa wazi kwa viongozi wote wa juu ambao wataona rufaa hiyo.

Maana yake ni kuwa rufaa hiyo ikifikishwa itafanyiwa kazi, inaweza kutafutwa Mwalimu wa chuo kingine kwa ajili ya kusahihisha mtihani au mitihani ya Mwanafunzi mwenye malalamiko.

Hata hivi karibuni tulipoanza masomo Wanafunzi walipewa semina elekezi kuhusu maboresho ya mfumo, walijulishwa kuhusu vitu vilivyoongezwa na vilivyopunguzwa ndani ya mfumo waweze kuutumia vizuri.

Yapo yale ya kukubali ambayo ni changamoto za kibinaadamu lakini kama mfumo wenyewe hauna shida na ndio maana unatumia na vyuo vingine pia zaidi ya vitano hapa nchini.
 
Back
Top Bottom