KwetuKwanza
Member
- Mar 13, 2023
- 72
- 133
Sisi wakazi wa Kijiji cha Bukundi Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa Maji ambao tuliambiwa thamani yake ni Sh. Milioni 500 kisha ukafanya kazi kwa muda wa miezi mitatu tu, tunaomba kujua hatma ya mradi huu na huduma ya maji kwenye kijiji chetu.
Mwaka 2016, Serikali ilianza kutekeleza mradi huo, ambapo Mkuu wa Wilaya wakati huo namkumbuka kwa jina moja Bwana Chilongani, alifika hapa kijijini na kuweka jiwe la Msingi.
Ukweli Wananchi wa hiki kijiji tulifurahi sana, kwani tangu nchi ipate uhuru hatukuwahi kupata maji safi wala salama, maji ambayo tulikuwa tunatumia muda wote ni kutoka Mto Bukundi.
Maji hayo ya mto tulichangia na mifugo, ni maji ambayo hayakuwa safi na salama, baada ya kuona mradi huo tulifurahi sana, tukapiga kelele za kufurahi kwa kupata mradi wa maji.
Mradi ulitekelezwa vyema na mwaka 2017 nakumbuka ilikuwa tarehe 07/04/2017 mradi ulizinduliwa rasmi na Mwenge wa Uhuru ambao ulifika katka kijiji chetu.Wananchi tulifurahi sana baada ya Mwenge wa Uhuru kuzindua mradi wa Maji kwenye kijijiji chetu, wananchi tulianza kutumia maji hayo.
Pia, soma: √ - Waziri Aweso: Kijiji cha Bukundi hakina huduma ya Maji Kuanzia tarehe 1-12-2024 na siyo kuanzia 2017
Tuliendelea kutumia maji hayo takribani miezi mitatu tangu Mwenge wa Uhuru uzindue mradi wetu, lakini baada ya muda huo wa miezi mitatu mpaka leo mradi hautoi maji.
Watalaamu walikuja siku moja, wakatengeneza mradi ukatoa maji wiki moja tu, kisha baada ya hapo maji hayakutoka tena, Wananchi wa kijiji hiki tumerudi kwenye maisha yetu yale ya zamani ya kutumia maji ya Mto Bukundi.
Kwa sasa tunatumia maji ya kuchimba vidimbwi kwenye mto wetu, maji ambayo tunachangia na ngo’mbe, mradi kwa sasa umetelekezwa, miundombinu kwenye chanzo imeanza kuharibiwa na mingine kuharibika.
Mabomba ya maji yameanza kuibiwa, mengine yamekatika, lakini Jenereita kwenye eneo la kusukuma maji halifanyi kazi kwa sasa, na liko katika hatari ya kuibiwa.
Wananchi tunateseka kupata huduma ya maji, lakini mradi wa Shilingi Milioni 500 kodi zetu wananchi zimetumika kwa miezi mitatu tu, na tumerudi katika mateso yetu ya kila siku ya huduma ya maji.
Hakuna kiongozi yeyote awe wa kijiji, hadi Taifa ambaye amekuja hapa kuangalia hizo Sh Milioni 500 zilivyoteketea, tuliwahi kuuliza uko nyuma, tuliambiwa Watalaamu walitengeneza vibaya.
Tunaomba Waziri wa Maji, Rais kuingilia kati hili jambo, hizi Sh Milioni 500 zimeteketea hivi hivi jamani? Wananchi tunaangaika na maji kwa sasa halafu kodi zetu zimechezewa kiasi hiki!