Naibu waziri wa mazingira Mh.Mpina akifunga kiwanda cha kusindika ngozi Shinyanga.
Serikali imekifunga kwa muda kiwanda cha kusindika ngozi kilichopo mjini Shinyanga kiitwacho Xing Xua kinachomilikiwa na raia wa China kutokana na kuwapo kwa ukiukwaji wa sheria za mazingira na kanuni zake za mwaka 2004 pamoja na kukitoza faini ya shilingi milioni 25 kutokana na kuchafua mazingira.
Kiwanda hicho kimefungwa na naibu waziri wa nchi, ofisi ya makamu wa rais mazingira na muungano Mh. Luhaga Mpina, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza na kubaini kuwa kinafanya kazi kikiwa hakijakamilika pamoja na mazingira yake kuwa hatarishi kwa afya za wafanyakazi pamoja na wananchi wanaokizunguka.
Kwa upande wake mratibu wa baraza la taifa la mazingira (NEMC) kanda ya ziwa Anna Masasi akizungumzia kuhusu kiwanda cha hicho cha kusindika ngozi, amesema licha ya kiwanda hicho kuomba cheti cha kuchinja mifugo na kusindika nyama, lakini kimekiuka na kufanya kazi ya usindikaji ngozi kinyume cha cheti cha uwekezaji nchini na kukitaka kibadili cheti hicho.bado kimefungwa na kupigwa faini ya shilingi milioni 25 kwa uchafuzi wa mazingira.
Ziara hiyo pia imemfikisha katika mgodi wa dhahabu wa Buzwagi ambapo akizungumza na wafanyakazi pamoja na uongozi wa mgodi huo alipewa taarifa na meneja wa mgodi huo Asa Mwaipopo kwamba, ifikapo juni mwaka huu shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika mgodi zitasitishwa lakini uzalishaji utaendelea hadi mwaka 2019 watakapofunga mgodi huo rasmi, huku naibu waziri huyo akipinga kufungwa kwa mgodi huo kwa maelezo kuwa itakuwa ni hasara kwa taifa kwa vile kiasi cha kikubwa cha dhahabu kitakuwa kimeondolewa.
Chanzo: ITV