JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,661
- 6,395
Mpina awafungulia kesi Spika wa Bunge, Waziri wa Fedha, Waziri wa Kilimo, Kamishna wa TRA, AG na Makampuni yaliyopewa tenda ya kuagiza Sukari
Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina amefungua kesi mbili Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambapo kesi ya kwanza ni dhidi ya Spika ambapo anahoji juu ya uhalali wa kuadhibiwa na Bunge kwa kusimamishwa vikao 15.
Kesi ya pili ni Mpina dhidi ya Waziri wa Kilimo, Waziri wa Fedha, Kamshina wa TRA na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na kampuni ya Itel na Zanzibar Merchandise ambapo anahoji uhalali wa utaratibu uliotumika kutoa vibali vya uagizaji wa Sukari, ambapo Mpina anadai kuwa utaratibu huo ulikiuka Sheria, ambayo anadai kuwa vibali vinatakiwa kutolewa kwa muagizaji ambaye ni mazalishaji wa sukari.
Aidha kesi nyingine imefunguliwa na Mkulima anayetambulika kwa jina la Mzigondevu dhidi ya Waziri wa Kilimo na Mwanasheria wa Serikali, ambapo Mkulima huyo anayewawakilisha wengine wanahoji mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024 ambayo wadai yamefungua mlango wa uagizaji holela wa sukari, Kwamba Waziri anaweza kuruhusu yeyote kuagiza sukari jambo ambalo wanadai kuwa likitekelezwa linaweza kuathiri wazalishaji wa ndani.
Akizungumzia kesi hiyo, Wakili Boniface Mwambukusi ambaye amesema anaungana na Mawakili wengine takribani 100, akiwemo Wakili Dkt. Rugemeleza Nshala kusimamia kesi hizo tatu.
Ameeleza mteja wao kwenye kesi ya pili anahoji masuala mbalimbali "Anahoji uhalali na usalama wa sukari inayoingizwa nchini kama unafuata taratibu za kiafya na taratibu za taratibu zilizowekwa kimataifa kuhusu uingizwaji wa sukari. Lakini vilevile anataka kupata majawabu kama ilikuwa sahihi kwa misamaha ya Kodi iliyotoka ikiwa ni mabilioni, ambayo mteja wetu anaamini zinatakiwa kuingia kama Kodi au tozo"
Amesema nia kubwa ya mteja wao (Mpina) ni kutekeleza haki za ulinzi wa Taifa na usimamizi wa sheria.
Aidha, Mpina akiwa mahakamani hapo leo August 28, 2024 amesema "Niseme kwamba najua katika uamuzi huu niliouchukua ni uamuzi wa maamuzi magumu kwa Mbunge kuchukua hatua hizi."
Amesema uamuzi huo ni 'challenge' kwa Bunge na Wabunge wenzake pamoja na watu ambao wamepewa dhamana ya uwakilishi
PIA SOMA
- Kuelekea 2025 - Luhaga Mpina amshtaki Spika Tulia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuondolewa Bungeni kinyume na Sheria