prince john john
JF-Expert Member
- Aug 31, 2016
- 2,166
- 3,294
KIBWAGIZO CHA JUMA KUU NA PASAKA
-MOYO WA YESU UNAKARIBIA KUPASUKA KWA JINSI TUNAVYOMTESA SIKU HIZI
_Padri Titus Amigu_
Mniwie radhi sana ninapotumia lugha hii ya picha ambayo hoja yake inaweza isilingane kwa asilimia mia na mafundisho msingi ya imani (dogma).
Lakini siwezi kuuzuia mkasa huo kwani ndivyo inavyokuwa katika matumizi yote ya lugha ya picha. Nakupa mfano mdogo ili unielewe. Sikiliza ukisema, “Fulani ni mkali kama simba” usitegemee kumwona mtu yule ana meno kama simba, mkia kama simba, kucha kama sifa na kwamba anawinda na kula nyama kama simba.
Si mara haba, katika kulinganisha mambo mlingano unaweza kuwa katika kipengele kidogo tu. Kwa mfano, katika mfano wetu wa mtu kuwa mkali kama simba, mlingano wenyewe upo katika mhemko wa ukali tu na wala siyo katika mambo yote ya simba. Ndipo katika hili “dude ninaloliamsha”, mlingano hauwezi kutazamiwa katika mwono wa moyo wa nyama maana Yesu tangu alipokufa na kufufuka Yesu Kristo hana moyo wa nyama ambao unaweza kuvimba na kupasuka.
Tangu kifo na ufufuko wake, Yesu Kristo hamiliki tena moyo wa nyama kama sisi wanadamu. Baada ya ufufuko Yesu Kristo ana mwili wa ufufuko.
Natumaini nimejieleza kwa kueleweka. Ndiposa, lugha ya picha ninayowasihi mhusike nayo wakati huu ya Juma Kuu na Pasaka ni hii: Moyo wa Yesu unakaribia kupasuka kwa jinsi tunavyomtesa. Mtaniuliza mara moja, Wakristo au Wakatoliki tunamtesaje na kuvimbisha moyo wake siku hizi? Ni katika vipengele kumi tatu vifuatavyo:
MOSI, KUPUUZA NA KUKAIDI AMRI NA MAAGIZO YAKE.
Yesu anateseka sana. Alituagiza tunaposali tusipayuke payuke, kinyume chake sisi tunapayuka payuka pasipo adabu. Tunaliita jina lake ovyo ovyo, hususan katika sarakasi za maombezi na miujiza feki. Kuhusu hili hili, alitutahadharisha tusiwaige wanaofanya hivyo, kumbe sisi tumewaiga nap engine tunakaribia kuwapita wenyewe walioanzisha mtindo huo wa kusali. Rejea maneno yake katika Mt 6:5-8.
PILI, KUHANGAIKIA ZAIDI YAMWINGIAYO MTU BADALA YA YAMTOKAYO MTU.
Kadiri miaka inavyopita, Wakristo au Wakatoliki chungu nzima hawaogopi tena vipengele vya amri kumi za Mungu, isipokuwa makosa ya mwonekano wa nje tu. Wapo wasiojua dambi ni nini. Hao hawaogopi kufanya uovu. Kwa kuwa wamefaulu katika kuziua dhamiri zao, hawa kitu kama “kuumwa na dhamiri”. Wivu, hasira, ulevi, uzinzi, uasherati, ufisadi, mafarakano, tamaa mbaya, mawazo maovu, uaji na kadhalika ni mambo ya “zilipendwa” tu.
Lakini, kwa hali hii ya mambo, Yesu anateseka sana. Bwana wetu alisema tusihangaike na kimwingiacho mtu maana hicho huishia chooni tu. Alimaanisha tusiogope kula senene, kumbikumbi, “likungu”, kambare, konokono, pweza, ”kitimoto” (Noah) wala “samaki nchanga” (panya). Alichotuagiza ni kuogopa kimtokacho mtu, lakini tunarudi Agano la Kale na kujivisha hofu za Kiyahudi mintarafu nyama haramu (Law 11:1-45). Kumbe, tusome Mk 7:14-23 tuone tunavyosigana na mafundisho yake.
TATU, MAKANISA KUZALIWA KAMA UYOGA.
Yesu anateseka mmoja. Yeye alizungumzia umoja wa wafuasi wake (Yn 17), kinyume chake, siku hizi kila Mkristo anayetamani sifa binafsi na “mshiko” anajianzishia kanisa na kujitungia sheria na kanuni zake. Mtu analala akiwaza na kuwazua jinsi ya “kutoka kimaisha”, akiamkia mkono kulia tu anajitangaza yeye ni nabii, mtume, mchungaji, mjoli au mtumish wa Bwana na kujianzishia kanisa lake na kuanza kula vya wajinga ndiyo waliwao ambavyo kimsingi ni “vya wenye imani” iliyokaa henamu. Ndiposa, makanisa yanazaliwa kila siku na kila mahali kama uyoga. Nahofia, hadi karne ijayo, hapa Afrika, kila nyumba itakuwa na kanisa lake na kila mtaa utakuwa na askofu, nabii, mtume au mchungaji. Lakini “kubiashirishwa” huku kwa Injili ni kitendo kile kile cha Yuda kumuuza Yeye. Kifupi, kutafuta pesa kumelikata koo la Injili. Yesu anaumia sana maana wanaofanya usaliti huu ni wale wale aliowapenda sana hata kuwafia msalabani.
NNE, KUFADHAISHWA KWA UTUME NA UMISIONARI.
Tusome Mt 28:18-20. Bwana wetu alitutuma twende kwa mataifa yote tukawafanye watu wote kuwa wanafunzi wake huku tukiwabatiza katika Utatu Mtakatifu. Alitupa amri ya kusambaa ulimwenguni tukihubiri. Alituagiza twende hadi mwisho wa dunia.
Kinyume chake, badala ya kwenda kwa mataifa na mwisho wa dunia, tunaunda vyama na vikundi vya kupita kuwababaisha katika imani waliobatizwa tayari. Tunathubutu kuingia majumbani mwao na kuwaonesha kwamba wanatakiwa kuanza upya katika imani. Tupo tunaowataka wabatizwa wabatizwe tena. Tupo tunaowaita wenzetu ‘hawajaokoka’ huku tukijiita wenyewe “tumeokoka” kinyume na kauli ya Yesu (Mk 13:13). Kabla hatujafa hatujaumbika na kujisifu tusijisifu wenyewe (Mit 27:1-2, YbS 11:27-28). Tupo tunaowahukumu wenzetu kama “waenda motoni wa uhakika” na kadhalika.
Hapo hapo, tupo tunaokazania kuinjilisha mijini tu huku tukinyanyapaa kwenda vijijini na sehemu fukara. Mambo ya uinjishaji ni kama yamepigwa gia ya kurudi nyuma (reverse) badala ya gia ya kwenda mbele hadi miisho ya dunia. Nia ya tunayoyatenda haijafichika mbele ya Yesu. Sisi mbele ya Yesu ni kama matenga, hatuna lililositirika asilione na kulijua.
Hivi kwa hakika, Yesu anajua, tunapenda mijini si hasa kwa sababu ya kuinjilisha bali kwa sababu kuna maisha mazuri na pesa tele. Anajua tunapenda pesa iliyomo katika mifuko ya watu, utume na uinjilishaji ni kisingizio tu. Tungependa utume na umisionari tusingeliogopa kwenda kwa watu hata walio fukara sana. Anajua fika kwamba tumejitengenezea mabwana wawili, na bwana mmoja ambaye ni Mungu hatumpendi sana zaidi ya “mshiko”. Anajua fikra zetu za “utume na uinjilishaji vijijini au kati ya fukara havilipi”.
TANO, KUHUBIRI HOFU, LAANA, UCHAWI, MAPEPO, “MAJINI” NA KADHALIKA BADALA YA HABARI NJEMA YA FURAHA.
Yesu alikuja kuwahubiria watu Habari Njema na kuwaondoa watu katika uvuli wa mauli, kinyume chake sisi tunatoka na kuwahubiria watu mambo ya kutishatisha hadi wanagonjeka. Unazidi kuwagandamizia watu kwenye uvuli wa mauti. Nadhani ukifanyika utafiti, Wakristo, hasa wa Afrika, tunaweza kugunduliwa kuwa watu wa mwisho katika kipengele cha furaha, maana tunatishwa sana, tena kwa jina la Ukristo wao huo huo.
Wakristo wangapi leo hawawezi kuhimili kuwaona popo, kuwasikia bundi wakilia, kuona mijusi ukutani na mende vyumbani? Najua ni wengi na hata vijana wameshaanza kutokwa na jasho la hofu. Usinibishe. Ukinibisha, jiulize, maana ya sala za kukemea ni nini! Ni balaa. Kumbe, mafundisho ya kutiana hofu yanazidi kutamalaki katika ya Wakristo wa Afrika. Hakika, tunajidumaza na kujiharibu kwa kutojiamini sawa na watu wa mabara mengine. Tusome Lk 4:18 tuone tunavyoigeuza.
SITA, KUJISIFIA KARAMA NA UTAKATIFU.
Watu tunaojitangaza kuwa na karama chekwa ni wengi sana. Watu tunaojikweza tunaongezeka siku kwa siku. Watu tunaojihukumu na kujitangazia utakatifu tunaongezeka. Mambo yale yale ya kujikweza badala ya kujidhili ni bayana bin mubashara sasa. Yaani, jambo lile lile alilotaka Yesu kulitahadharisha kwa mfano wa farisayo na mtoza ushuru linafurahiwa na wengi. Samahani, tumeacha njia iliyonyooka sasa tunatokomea kwenye “mchepuko”. Kumbe tusome tena Lk 19:9-13.
SABA, KUTEKWA KWA ROHO MTAKATIFU. Tupo majasiri tunaotamba huko na huko kwamba tunaye Roho Mtakatifu katika utele wake wote na kifupi kwamba “yumo mifukoni mwetu”. Ni wengi ambao kwa maisha yetu na majigambo yetu tunajinasibu kwa kusema, “Mimi ninaye, mimi ninaye”. Lakini, Bwana wetu alisema Roho Mtakatifu ni Mungu naye, kama Mungu, atakaa kwetu akitufundisha na kututetea.
Kumbe, sisi tunavyomweleza Roho Mtakatifu, siku hizi, ni kama tunaosema Roho Mtakatifu anafanana na “noti ya Msimbazi” (shilingi elfu kumi ya Tanzania) ambayo unaweza kuikunja, kuiweka mfukoni na kuwaeleza watu kwamba unayo na wakati wowote utakapotaka unaweza kuitumia au kumpa mtu unayetaka mwenyewe kumpa. Jambo hili linamtesa sana Yesu Kristo. Ni kumkufuru Roho Mtakatifu katika umungu wake.
NANE, KUTANGAZWA, KUKUZWA NA KUJAZWA SHETANI KILA MAHALI ULIMWENGUNI WAKATI FUMBO LA PASAKA NDIO TANGAZO LA KUSHINDWA KWAKE.
Bwana wetu Yesu Kristo alisema amemfunga Shetani (Mt 12:29) na hivyo anaviteka vitu vyake na alilifanikisha hili kwa mateso yake makali msalabani. Yesu amemvunja kiuno Shetani. Kama ingekuwa ni mpira wa miguu amemfunga mabao mia kwa bila. Ndiyo kisa sasa tunatawala na Kristo miaka ile elfu (Ufu 20:1-3). Lakini kinyume cha ukweli huu, Wakristo au Wakatoliki wanaomhubiri Shetani ni wengi. Yaani ni kama Shetani sasa ni Nafsi ya Mungu. Siongopi, Wakatoliki wa namna hii wanamwona Shetani kila mahali. Nikikopa istalahi zao wenyewe ni hivi hawa sasa “wanamwinua na kumbariki Shetani” sana. Nadhani Shetani anafurahia sana uongo huu. Mbinu hii ya “kupendwa kwa kinyume” ni mbinu kiboko kabisa aliyoibuni Shetani mwenyewe. Kwayo keshaingia sebuleni kwa mlango wa nyuma. Kumbe Shetani, mwerevu kweli kweli! Hebu tuachane naye, “ulofa” wetu unamuumiza sana Bwana wetu!
Nina ushahidi kwamba Shetani keshajipatia waumini wengi. Ushahidi ni huu. Waumini wake wakianguka sababu yao ni Shetani. Wakilewa, Shetani. Biashara ikienda ovyo, Shetani. Wasipoolewa, Shetani. Wakikosa watoto, Shetani. Wakigombana, Shetani. Wasipopata ajira, Shetani. Wakifukuzwa kazi, Shetani. Wakiumwa magonjwa yenye kutatanisa, Shetani na kadhalika.
Lakini mambo haya haya yanaweza kupewa sababu nyingine nne tofauti: mapepo au majini, laana au uchawi na sasa hata Frimasoni. Inategemea tu mtu ni muumini wa sababu ipi.
Waumini wa mapepo na majini, pasipo kujua mapepo na majini ni nini, wakianguka, mapepo au majini. Wakiangusha kikombe chini, mapepo au majini. Wakiwa walevi au walafi, mapepo au majini. Biashara ikienda ovyo, mapepo au majini. Wasipoolewa, mapepo au majini. Wakikosa watoto, mapepo au majini. Wakigombana, mapepo au majini. Wakiugua, mapepo au majini. Wasipopata ajira, mapepo au majini. Wakifukuzwa kazi, mapepo au majini na kadhalika.
Waumini wa laana, wakianguka, laana. Wakilewa, laana. Biashara ikienda ovyo, laana. Wasipoolewa, laana. Wakikosa watoto, laana. Wakigombana, laana. Wasipopata ajira, laana. Wakifukuzwa kazi, laana na kadhalika.
Waumini wa uchawi, wakianguka, uchawi. Wakijilegeza na kushindwa kuacha pombe, uchawi. Biashara ikienda ovyo, uchawi. Wasipoolewa, wamerogwa kwa uchawi. Wakikosa watoto, wamerogwa kwa uchawi. Wakigombana, wamerogwa kwa uchawi. Wakiugua wenyewe au jamaa na rafiki zao, wamerogwa kwa uchawi. Wasipopata ajira, wamerogwa kwa uchawi. Wakifukuzwa kazi, wamerogwa kwa uchawi. Akifa mtu, hata akiwa mzee sana, amerogwa kwa uchawi na kadhalika. Lakini kuamini uchawi, ni kikomo cha kufikiri. Soma pia Africae Munus 93. Jambo hili linamtesa sana Yesu Kristo kwa sababu alipotuumba (sisi tumeumbwa naye –Mwa 1:26, Yn 1:3) alitupatia akili na utashi tukabiliane na matatizo yetu kwa juhudi na maarifa, tofauti na wanyama wa kufugwa na hayawani.
Hatimaye, waumini wa Frimasoni, wakianguka, Frimasoni. Wakijilegeza na kushindwa kuacha pombe, wametekwa na Frimasoni. Biashara ikienda ovyo, Frimasoni. Wasipoolewa, Frimasoni. Wakikosa watoto, Frimasoni. Wakigombana, Frimasoni. Wakiugua wenyewe au jamaa na rafiki zao, Frimasoni. Wasipopata ajira, Frimasoni. Wakifukuzwa kazi, Frimasoni. Akifa mtu, hata akiwa mzee sana, ametolewa kafara na Frimasoni na kadhalika.
TISA, WATU KUDAI KUWEZA KUFANYA MIUJIZA KAMA MAFUNDI WA KUSOMEA (TECHNICIANS).
Wakatoliki wanaotengeneza mabango na kuwaalika watu waje washuhudie miujiza na maajabu ya Mungu kana kwamba wao ni “wataalamu” wapo siku hizi. Wanapuuza ukweli kwamba miujiza ya kweli ni majaliwa yanayowezeshwa na Mungu mahali na wakati anapoona mwenyewe inafaa na siyo kwa kukamiwa au kwa matamasha au makongamano.
Zaidi ya hayo, kuna kituko kingine. Watu wanaofuja maneno ya Yesu Kristo kwamba “wanafunzi wake watafanya miujiza mikubwa kuliko yake” (Yn 14:12) ni wengi. Lakini hapa ilitupasa tumwelewe vyema. Hakumaanisha tufanyie utani kauli yake hiyo. Alitoa sharti kubwa imani. Mwenye imani kubwa ndiye atakayefanikisha miujiza ya kweli na mikubwa, asiye nayo asijitangazie kuweza kitu chochote, akae kimya. Huyo asijidanganye mwenyewe wala sisi wenzake seuze Yesu Kriso mwenyewe. Kumbe, anayetaka miujiza ya kimatamasha asishirikiane na Yesu bali ashirikiane na Shetani, adui wa ukweli anayewezesha miujiza feki kusudi wenye njaa ya miujiza wapotee. Soma 2 Thes 2:9-12.
KUMI, AKINAMAMA KUFANYWA MRADI NA “WAPIGA HELA” WAJANJA.
Yesu alitaka tuwaangalie kwa namna ya pekee akinadada na akinamama. Injili ya Luka ni ushahidi wangu. Yesu aliwakuta wakinyanyaswa na kudharauliwa na jamii zilizokolea mfumo dume. Alikuwa amekuja kuwakomboa hata hao.
Lakini kinyume na Yesu, siku hizi, watu wengi wamegundua kwamba kuna hela katika kujidai kuwasaidia akinadada na akinamama katika matatizo yao. Akinadada na akinamama “WANATOA”. Akinadada na akinamama hawana simile katika “KUCHANGIA HUDUMA”. Kifupi, wanatoa pesa kwa shukrani kwa kila wanayeamini amewasaidia. Ashakum si matusi. Wengine hushukuru hata kwa kujitoa wenyewe kingono.
Basi, katika muktadha huo, wapo wanaopita huko na huko wakijinasibu kuweza kuwasaidia wasioolewa, walioachika, wanaotishwa na kuonewa katika ndoa zao, wajane, wasio na watoto (yaani tasa) na kadhalika. Hata wakiwa na magonjwa kama nurosisi, hysteria (umanyeto), skizofrenia, mania (kucharukia sana kitu) na phobia (hofu) wao wanasema wanaweza kuwasaidia ilmradi waandae mifuko yao kiukarimu. Watu kama hao wanaweza kuwatonosa akinadada na akinamama majeraha yao kwa mahubiri ya kutisha ili kuwaliza na hivyo wadai wana mapepo na kisha kuwatuliza ili wadai wamewatoa pepo.
Akinadada na akinamama chungu mzima wanashindwa kuugutukia mchezo huu mchafu. Hivi wanageuzwa wahanga wa uongo. Kumbe, mkasa huu wa kuwageuza akinadada na akinamama vitega uchumi au hata bidhaa unamtesa sana Yesu, maana yeye mwenyewe alimsaidia Maria Magdalena bure, mke wa Kuza bure, mkwewe Simoni Petro bure, mama aliyekuwa akitokwa na damu kwa miaka mingi bure, mama aliyefiwa na mwanawe kule Naini bure na kadhalika.
KUMI NA MOJA, VIONGOZI WA DINI KUINGIA WOGA HATA KUSEMA UONGO. Dini hazijaanza jana, wala siasa hazijaanza jana. Kwa Wakristo Wakatoliki, kwa woga, watu wanafuja vipaimara vyao na sakramenti ya Daraja inayowafanya wawe makuhani, manabii na wafalme hapa ulimwenguni. Hao wanapatwa na woga kiasi hiki wanasema uongo wa kwamba dini haipaswi kuhusiana na siasa.
Ni uongo kabisa kwani hata Pasaka yenyewe, tunayoisherehekea kila mwaka, ni matunda ya mwingiliano wa dini na siasa. Wayahudi wanaokolewa kutoka katika mikono ya Farao (mwanasiasa). Musa alikuwa mtu wa dini lakini alipambana na Farao, mwanasiasa. Kumbe, kudai dini isihusiane na dini siyo tu woga unaowashika viongozi wa dini isipokuwa ni pia ishara ya kutoyajua Maandiko. Tangu mwanzo wa Biblia hata mwisho wake, watu wa dini walihusiana na wanasiasa. Abrahamu alihusiana na Melkizedeki, mfalme. Tena alihusiana na Farao kule Misri hata akalazimika kusema uongo wa kwamba Sara si mkewe akiogopa kuuawa. Yusufu alihusiana kisiasa na Farao sawia na Putifa na mkewe.
Musa ndiyo tusiseme alihusiana na Farao. Mapigo kumi dhidi ya Wamisri shauri lenyewe lilikuwa siasa, utumwa. Na tunajua pigo la kumi na mbili, kuuawa kwa wazaliwa wa kwanza wa wanyama na wanadamu wa Wamisri ndilo lililo asili ya sikukuu ya Pasaka. Tupo pamoja?
Naomba niendelee na mifano. Samweli alihusiana na wanasiasa Sauli na Daudi. Elisha alihusiana na akina Ahabu na Jezebeli. Isaya alihusiana na akina Sairusi. Yeremia alihusiana na siasa za wafalme wengi hata akatupwa katika shimo la simba. Danieli na wenzake walihusiana na akina Nebukadreza na Belshaza. Manabii wote walihusiana na wafalme ama wakiwaunga mkono na kuwashauri au kuwaonya na kuwasahihisha. Yohane Mbatizaji alimkanya mwanasiasa Herodi Antipasi akalipia kwa shingo lake. Yesu mwenyewe alihusiana na wanasiasa kama akina Herode na Pilato. Mbona tunakumbuka kwamba Yesu alihukumiwa na Pilato,
Hatimaye, mitume nao walihusiana na wanasiasa, wengine wakali sana wakawatoa roho zao. Hata kitabu cha mwisho cha Biblia (ndiyo Ufunuo) ni mahusiano kati ya Dola ya Rumi na Wakristo. Makaisari walikuwa wanasiasa. Kaisari Konstantino aliyelisaidia Kanisa kupata nafuu ya madhulumu alikuwa mwanasiasa. Je, hatumsifu kwa kuwa mtu mwema?
Baada ya mitume, watakatifu mbalimbali walihusiana pia na wanasiasa kwa kuwaunga mkono au kuwakanya. Akina Thomas More na John Fisher walipotezaje maisha yao? Maximilian Kolbe alikufa katika muktadha gani? Kwa nini Baba watakatifu walioishi wakati wa biashara ya utumwa na hata wakati wa mauaji ya kimbari yaliyoendeshwa na Adolf Hilter dhidi ya Wayahudi wanalaumiwa kwa kutokuwa na misimamo ya kuwatetea wanyonge?
Si hivyo tu, historia ya Kanisa imejaa hati zinazohusika na mambo ya siasa. Rerum Novarum ina muktadha upi? Gadium et Spes ina muktadha gani, kwa nini tuseme Kanisa Ulimwenguni? Ulimwengu wa wapi wanaoishi wanadini peke yao pasipo dola, nchi na mataifa? Sasa inakuwaje ajabu au haramu kwetu sisi tunaoishi katika karne hii kujihusisha kwa namna yake na siasa?
Tusijipinge wenyewe. Kwa nini kila tunaposali sala za waumini tunaiombea serikali na viongozi wao? Tunawaombeaje ikiwa mambo yao hayatuhusu? Lakini ukweli ni huu. Tunaishi katika ulimwengu mmoja na wanasiasa. Ni katika ulimwengu huo huo tunamoaswa kufanya utume. Yesu Kristo hajawapa Wakristo ulimwengu wao peke yao (Yn 16:33).
Kama ndivyo, tutawezaje kuzungumzia mambo ya haki, amani na upatanisho pasipo kuwagusa wanasiasa na watawala ambao ndio wenye vyombo vinavyohusika na hayo? Anawezaje mwanadini kuzungumzia haki bila kuigusa nchi na watawala wake? Anawezaje mwanadini kuzungumzia haki na amani pasipo kuwagusa polisi na mahakimu?
Nadhani kama Wakristo wasingelikuwa raia wa nchi za ulimwengu huu na wanasiasa wasingelikuwa waamini wa dini za ulimwengu huu, dini na siasa vingeliweza kutenganishwa vizuri kabisa. Lakini kama waamini tusingelikuwa raia tusingelilipa kodi na wala tusingelishiriki chaguzi zozote na wanasiasa nao wasingelikuwa waamini tusingeliwatazamia waje kusali wala kushika amri yoyote ya Mungu. Kumbe basi, woga wetu usitufanye tuseme uongo wa kutaka dini na siasa visigusane, tunamuumiza sana Yesu aliyekuwa jasiri namba moja.
Ukweli ni kwamba wanadini siasa inatuhusu na wanasiasa dini inawahusu. Nani aliyesema mwanadini hawezi kuwa mwanasiasa na mwanasiasa hawezi kuwa mwanadini? Tusipotoshe mambo kwa woga wetu. Kumbe, kinachohitajika ni busara na kujali uwiano wa kusifiana, kuhimizana, kujadiliana na kuonyana ili wote tusiukose uzima wa milele. La sivyo, waamini na viongozi wao wasiseme wanashiriki ofisi za unabii na ufalme za Yesu Kristo!
Aidha, kukutana dini na siasa si ajabu. Kama tumetumwa ulimwenguni tukawafanye watu wote wanafunzi wa Yesu tusistaajabu kukutana na wafanyabiashara, wanasiasa, wema na wabaya. Acha nikumbuke wimbo wa zamani. Ni hivi kila mwamini, kwa sababu ya utume wake wa kimisionari ambao kwao anatakiwa kukutana na watu wote, anapaswa kujiimbisha wimbo wa zamani wa “Wote ni abiria wangu”, maana yake wanasiasa na siasa zao wamo kati ya abiria wake.
KUMI NA MBILI, WATU KUSHUGHULIKA ZAIDI NA UJENZI WA MAJENGO NA MIRADI BADALA YA KUILINDA NA KUIJENGA IMANI.
Sisemi kujenga majengo na miradi mbalimbali ya Kanisa ni vibaya isipokuwa kuzipa kazi za ujenzi na miradi kipaumbele mbele ya kuijenga na kuiimarisha imani ni kosa. Swali alilopata Yesu kuwauliza wafuasi wake ni, “Je, atakaporudi mwana wa Adamu ataikuta imani duniani?” (Lk 18:8) wala hakuuliza atakuta majengo ya makanisa, kumbi, shule na nyumba za kupangisha za Kanisa ngapi? Lakini kwa kuwa hatuko kwenye imani zaidi, kuna michango ya kila rangi na miradi inayoitwa ya kujitegemea ya kila kimo na upana.
Wakristo au Wakatoliki wanaohangaika watakula nini watavaa nini na kadhalika ni wengi kuliko wanaofuata kauli ya Yesu ya “kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu” hayo mengine wapewe kwa ziada (Lk 12:22-33). Jambo hili la kufanya ujenzi wa majengo kipaumbele badala ya imani, linamtesa sana Yesu Kristo. Ndiyo kwa sababu ya imani kuwekwa chini ya miradi ya ujenzi na kujitegemea, watu wanaofundisha na kupotoa mafundisho ya Kanisa hawakemewi, kuonywa wala kusahihishwa ilimradi “wanachangia sana”.
Nguvu ya pesa ni mtego mbaya dhidi ya ujasiri wa watumishi wa Mungu. Wapotoshaji wenyewe wameshajua pia kwamba pesa inaweza kuwafunga midomo hata waliopaswa kusema na mahali pengine tayari wanaishi kwa falsafa hiyo. Mimi sitabiri bali najua kwa hakika, kasoro hii italipiwa kwa gharama kubwa huko mwishoni mwa maisha yetu, hususan sisi viongozi.
KUMI NA TATU NA MWISHO, KUZIPUUZA SAKRAMENTI.
Sakramenti ya Ubatizo inazimwa na madai ya “ubatizo katika Roho”. Sakramenti ya Kipaimara sijui inaelewekaje. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu polepole inageuka chakula cha kawaida kama chapati, yaani bora ufike mezani tu. Sakramenti ya Kitubio inafinyangwa kwa visingizio mbalimbali vikiwamo vya waungamishi kutokuwa na uwezo wa kuungamisha watu kwa vile wenyewe ni wadhambi, wakati ukweli ni kwamba ufanisi wa sakramenti hautegemei hali ya mhudumu wake. Ukitaka Kilatini sema, “ex opera operato”. Lakini inaonekana tunarudishana kwenye uzushi wa zamani kuhusu sakramenti na ufanisi wake kwa mwendo kasi.
Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa inaoneshwa ni dhalili mbele ya karama za uponyaji na utoaji pepo. Sakramenti ya Ndoa inaonekana kuwa desturi ya gharama za bure na mwishowe sakramenti ya Daraja inaonekana kutokuwa na maana yoyote kwa vile inawezekana mtu kujitangazia uongozi kanisani kwa kadiri ile “moyo inapenda”.
Lakini, kudharauliwa kwa sakramenti kwa jinsi hii kunamuumiza sana Kristo. Maisha ya Wakristo pasipo sakramenti hufanana na maisha ya inzi jalalani. He, mkasa mkubwa! Kumbe, nawaombeni sana, kila mtu kwa kadiri ya hali yake, ampunguzie Yesu mateso, tunamtesa mno. Na wewe Yesu nakuomba utuhurumie nasi utusaidie. Tuangazie nuru yako tugundue tunavyokutesa na kujirudi kikamilifu. Amina.
Acha nikomee hapa. Kwa herini mintarafu kibwagizo hiki! Ndimi mzee wenu
Pd. Titus Amigu.
Ujumbe huu ni mahususi kwa ajili ya wakatoliki tu..