MOSHI: BINTI AMUUA MAMA YAKE MZAZI ILI ARITHI MALI, MWILI WAGUNDULIWA BAADA YA MWAKA MMOJA
• Meya Juma Raibu ashindwa kujizua amwaga machozi na kulaani vikali, awaasa vijana kuacha tamaa na starehe
•Meya Raibu ampongeza Rpc Kilimanjaro ACP Simon Maigwa na timu Yake Kuendelea Kusikiliza Na Kutatua Jinai Mbali Mbali
Ikiwa zimepita siku kadhaa toka litokee tukio la kijana mmoja jijini Arusha kumuua mama yake mzazi Kwa tamaa ya Mali, Limegundulika tukio lingine la kinyama mkoani Kilimanjaro katika Manispaa ya Moshi ambapo binti mmoja aliejulikana Kwa jina Moja la Wendy amemuua Mama yake mzazi (Mama Ipepu) ambae ni Nesi mstaafu wa Hospital ya KCMC.
Jeshi la Polisi limeufukua Mwili huo leo tarehe 09-01-2022 katika kata ya Rau baada ya kumhoji binti huyo Kwa zaidi ya wiki mbili sasa Kisha kukiri kumchinja mama yake Kwa panga na kumfukia nyumbani hapo.
Ni takribani Mwaka sasa ndugu na majirani walipokuwa wamuulizia mama huyo walipatiwa majibu na binti huyo kuwa amesafiri Kwa matibabu nje ya nchi.
Akizingumza Kwa uchungu huku akilengwalengwa na machozi Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ndg Juma Raibu ameonesha kusikitishwa na kitendo hicho na amelaani vikali tabia ya vijana kuendekeza tamaa na kukosa uvumilivu wa utafutaji Mali Kisha wanaishia kufanya matendo ya kinyama.
Namnukuu
"Kiukweli hili ni tukio la kutisha, nitoe pole Kwa familia ndugu na majirani wote mliofika hapa, nimepata huzuni sana kuona jinsi gani ya taamaa Mali imetufikisha hapa, nalaani na ninatoa wito Kwa vijana wenzangu wote nchini kuacha kupaparikia Mali na starehe mwisho wake tunageuka kuwa wanyama kiasi hiki, yaani unamuua mama mzazi?
Hivi unakuwa huoogopi laana na adhabu ya mola? nalipongeza Jeshi letu la Polisi Kwa hatua hii nawatia Moyo mwendelee na kazi hii njema ya kufichua na kudhibiti wahalifu wa namna hii na wanaoshirikiana nao".
mwisho wa kunukuu.
Tayari madaktari wameanza kufanyia uchunguzi wa postmortem Mwili huo kwajili ya hatua zinazofuata.
#MoshiBlog UpdatesView attachment 2075108
------
Muuguzi huyo raia wa Tanzania mwenye asili ya Kijerumani, anadaiwa kuuawa mwezi Februari, mwaka jana na mwanawe wa kike na kisha kumzika kwa kificho pembeni ya nyumba yake ndogo iliyoko Kijiji cha Uru-Mkuruti, Kata ya Uru Kusini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Simon Maigwa, hadi kufikia jana mchana, watu watatu walikuwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kuhusiana na mauaji hayo.
“Kati ya tuliowakamata wakihusishwa na mauaji haya, yumo mtoto wa kike wa marehemu pamoja na waganga wawili wa kienyeji. Kati yao mganga mmoja anatokea Mkoa wa Tanga na mwingine jijini Dar es Salaam.
“Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kuwa waganga hao, walikwenda nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya kumpatia tiba mama huyo aliyekuwa mgonjwa. Sasa wakati akiendelea kupatiwa matibabu ya asili, mama huyo alishtukia zaidi ya shilingi milioni 60 za kiinua mgongo alizokuwa nazo zilishatumika na haoni matumaini ya kupona.”
Aidha, Kamanda Maigwa alisema, baada ya mama kuhoji matumizi ya fedha hizo, mwanawe wa kike na waganga hao walikuwa wakimtaka Patricia aende akatoe pesa nyingine na kuzuka purukushani iliyosababisha watuhumiwa hao kuamua kutekeleza mauaji yake.
“Walipomaliza kutekeleza mauaji hayo, waliuchukua mwili wake na kuuhifadhi katika moja ya chumba nyumbani kwa marehemu, wakisubiri giza liingie ili wakachimbe kaburi na kuuzika mwili huo,” alisema.
NDUGU WAHOFU
Kamanda Maigwa, alisema baada ya watuhumiwa kutekeleza dhamira ovu, baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki, walianza kupata shaka ya mwenendo wa mtoto wa kike wa marehemu (hakumtaja jina), kuuza rasilimali, huku mama yake akiwa hajulikani alipo.
Katika taarifa yake, Kamanda alisema binti huyo alianza kuuza mali za mama yake na alipokuwa akiulizwa, alikuwa akijibu anauza ili atume fedha nchini India, ambako mama yake alikuwa akipatiwa matibabu.
Maigwa alifafanua: “Desemba 20, mwaka jana, majirani zake walikuja Polisi kutoa taarifa za shaka kwamba huenda Patricia aliuawa miezi 10 iliyopita. Tulianza uchunguzi ikiwamo kukusanya vielelezo na tulifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa hao ambao walienda kuonyesha walipouficha mwili wa marehemu.
“Ilipofika Januari 9, mwaka huu, tulifanikiwa kuufukua mwili huo na ndani ya kaburi hilo kulikuwa na panga lenye nywele. Baada ya kujiridhisha kwamba ni mwili wa binadamu ulizikwa bila kufuata taratibu, tulichukua mabaki ya mwili huo na kwenda kuyahifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufani ya KCMC, kusubiri uchunguzi wa kina wa kitabibu,” alisema.
Kamanda Maigwa, alisema baada ya uchunguzi wa kina kutoka kwa wataalamu, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalowakabili la mauaji ya kukusudia.
Jana, Nipashe ilifika nyumbani kwa marehemu Patricia na kuwakuta baadhi ya majirani akiwamo Richard Estomii, ambaye alisema enzi za uhai wake Patricia alijaliwa kuzaa watoto wawili mapacha, mmoja akiwa nje ya nchi na mwingine anayetuhumiwa kumuua mama yake.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Musa Lyari, alisema licha ya kutafuta ukweli kwa muda mrefu, binti huyo hakuwahi kuwaonyesha ushirikiano wa alipo mama yake, zaidi ya kudanganya yuko nchini India akipatiwa matibabu.
“Nimemuuliza zaidi ya mara tano kila anapouza viwanja, kila mara anasema anafanya hivyo ili aweze kupata fedha za matibabu kwa ajili ya mama yake aliyeko India," alisema Lyari.
Chanzo: Nipashe