- Source #1
- View Source #1
- Source #2
- View Source #2
Nimepita mahali nikakutana na jopo likiwa na gari yao likiuza na kutangaza faida za mmea wa mwani ikiwa ni pamoja na kutatua tatizo la upungufu wa nguvu za kiume
Kuna ukweli wowote kwenye hili?
Kuna ukweli wowote kwenye hili?
- Tunachokijua
- Bahari imechukua 70% ya ardhi yote ya dunia ikiwa na utajiri wa vyakula mbalimbali vinavyofaa kwa matumizi ya binadamu. Kwa mujibu wa Marine Conservation Society, zipo zaidi ya aina 32,000 za Samaki baharini ambao hutofautiana maumbo, rangi na tabia.
Utajiri wa vyakula vya baharini hauwezi kukamilika pasipo kutaja uwepo wa Mwani (Sea moss), zao lililojipatia umaarufu mkubwa duniani zaidi ya milenia moja iliyopita ambalo kwa Tanzania hulimwa ukanda wa mwambao wa Bahari ya Hindi huku kisayansi likifahamika kama Chondrus crispus.
Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA) inabainisha kuwa, kila gramu 100 za zao la Mwani huwa na takriban gramu 81.3 za maji, gramu 1.51 protini, 0.16 gramu za mafuta, gramu 12.3 za wanga Pamoja na kiwango kidogo cha Sukari, Madini ya zinc, Iodine, Chuma, Selenium, Folate, Calcium, Manganese na Copper.
Ukiondoa Ladha yake ya kipekee, Mwani huwa na faida nyingi kwenye mwili wa binadamu ikiwemo kuboresha afya ya tezi za thyroid, husaidia kuimarisha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na mfumo wa kinga Pamoja na kudhibiti na kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa Kisukari. Aidha, uwepo wa Omega 3 huboresha moyo na mfumo wa damu hivyo kusaidia kupunguza hatari ya kupatwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanayoshambulia moyo.
Mwani unaongeza nguvu za kiume?
Dhana ya nguvu za kiume ni pana sana, lakini tunaweza kuirahisisha kwa kusema ni uwezo wa mwanaume kusimamisha uume kiasi cha kuweza kushiriki kikamilifu tendo la ndoa. Uwepo au kutokuwepo wa nguvu hizi huchangiwa na mambo makuu matatu ambayo ni mfumo wa usafirishaji wa damu mwilini, mfumo wa neva za fahamu Pamoja na mfumo wa homoni za mwili.
Aidha, uwepo baadhi ya magonjwa sugu kama Kisukari, matumizi ya baadhi ya dawa Pamoja na changamoto za kisaikolojia vinaweza pia kuchangia kutokea kwa tatizo hili ambao kwa mujibu wa tafiti linakabili takriban 50 ya wanaume wenye umri kati ya miaka 40-70.
Lakini, mdau anafafanua kuwa katika pitapita zake amekutana na gari ikitoa matangazo kuwa mmea huu unaweza kutibu changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume. Baadhi ya watu wamewahi pia kuchapisha madai haya mtandaoni, tazama hapa na hapa.
Madai haya yana ukweli kiasi gani?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck umebaini hakuna Ushahidi wa moja kwa moja wa kitafiti unaothibitisha hoja hii. Pamoja na kuwepo kwa uhusiano mdogo wa baadhi ya virutubisho na uboreshaji wa ufanisi wa tendo la ndoa, bado hakuna uthibitisho unaoteta hoja hii.
Kiambata cha Zinc kinachopatikana kwenye Mwani ndicho kinachotajwa kuwa nguvu iliyo nyuma ya uwezo wa mmea huu katika kutibu changamoto ya nguvu za kiume. Zinc huongeza uwezo wa mwanaume kuzalisha homoni za kiume (Testosterone) ambazo huchangia katika kuamua ubora wa afya ya uzazi. Aidha, uwepo wa folate huongeza ubora wa shahawa zinazozalishwa na mwanaume.
Hii pekee haitoshi kuhitimisha kuwa mwani unaweza kutibu changamoto ya nguvu za kiume kwani tatizo hili ni mtambuka kama lilivyofafanuliwa huko Juu.
Matibabu ya tatizo la nguvu za kiume hutegemea chanzo chake na yanaweza kufanikishwa kwa kutumia dawa, kubadili mtindo wa Maisha (Chakula na vinywaji), kuzungumza na washauri nasihi, kupitia tiba ya upasuaji, mazoezi Pamoja na njia zingine zinazoweza kushauriwa na madaktari kulingana na chanzo kilichopelekea kutokea kwake.
Aidha, ni muhimu kukazia kuwa, chakula kina mchango mkubwa katika kusaidia kurejesha ubora wa nguvu za kiume kwa mtu mwenye changamoto hiyo. Hata hivyo, pamoja na ukweli kuwa mmea huu umekuwa unatumika kwa miaka mingi kwenye jamaii nyingi ukinasibishwa na uwezo wake wa kutibu changamoto tajwa, bado Ushahidi wa kisayansi unahitajika kuthibitisha suala hilo.