LICHA ya Rais wa awamu ya nne,Jakaya Kikwete kuacha maagizo ya kulipwa mshahara na marupurupu kama walivyokuwa wanalipwa makocha wa kigeni waliopita, kocha mkuu wa timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Boniface 'Master' Mkwasa anadai Sh. milioni 200 imebainika.
Mkwasa alipewa mikoba ya kuiongoza Stars baada ya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuamua kusitisha ajira ya Mdachi,Mart Nooij Juni 21 mwaka jana baada ya kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Uganda (The Cranes).
Taarifa za ndani kutoka katika shirikisho hilo ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE imezipata zinaeleza kwamba Mkwasa ambaye mshahara wake kwa mwezi ni Sh. milioni 25, hajalipwa tangu Agosti mwaka jana.
Chanzo chetu kiliendelea kusema kuwa tangu kocha huyo ambaye aliachana na ajira yake ndani ya klabu ya Yanga alipoajiriwa kuiongoza Stars,amepokea mshahara mmoja tu wa Julai.
Kilisema kuwa Juni alipewa posho wakati timu hiyo ikijiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya The Cranes ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zilizopita za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) ambayo Stars ilitolewa na Waganda hao.
"Kiukweli hali ni ngumu na mambo mengi yaliyoko kwenye mkataba wake hayajatekelezwa, mshahara kama mshahara amelipwa mmoja tu, tangu hapo amekuwa akilipwa posho za kawaida akiwa kambini na timu inaposafiri," kilisema chanzo chetu.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa mbali na madai ya mshahara, vipengele vingine vilivyoainishwa kwenye mkataba wa miezi 18 ambao kocha huyo alisaini,
pia havijatekelezwa licha ya wakati wote akionekana kufanya kazi zake kwa uadilifu.
"Kiufupi Mkwasa anafanya kazi katika mazingira magumu, waswahili wanasema wanamchukulia poa,hajapewa nyumba wala usafiri, hakuna hata kitu kimoja kilichotekelezwa kwenye mkataba,"chanzo chetu kiliongeza.
Habari zaidi kutoka kwa mtu wa karibu na Mkwasa zinaeleza kwamba kocha huyo anataka kubwaga 'manyanga' baada ya mechi kati ya Stars na Misri inayotarajiwa kufanyika Juni 4 mwaka huu endapo madai yake hayatafanyiwa kazi.
"Kila akiwauliza wakubwa (viongozi wa juu wa TFF) wanamuambia bado suala lake linafanyiwa kazi, ila ameshafikiria kuachana na timu baada ya Juni akimaliza mechi dhidi ya Misri na hapo atakuwa ametimiza mwaka mmoja kwenye ajira hiyo,halipwi fedha na wakati huo huo sasa TFF imemrejesha Kim (Poulsen), je mzungu anaweza kukaa muda wote huu bila kulipwa haki yake," kiliongeza chanzo hicho.
Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema jana kuwa Mkwasa ni mwajiriwa wa shirikisho hilo na hawezi kuweka wazi taratibu taarifa zinazomhusu kocha huyo.
"Siwezi kusema anadai au hatudai, hata mimi (Mwesigwa) au mwajiriwa mwingine wa TFF anaweza kuwa na madai yake, lakini taratibu haziniruhusu kusema," alisema katibu huyo.
Mkwasa alisaini mkataba wa miezi 18 ambao unatarajiwa kumalizika Machi 31 mwakani.