Katika siku za hivi karibuni baadhi ya nchi za magharibi zimekuwa zikitumia majukwaa ya siasa za kimataifa, kutoa kauli na maazimio yanayoikosoa China kuhusu Xinjiang. Ukosoaji huo umekuwa ukitumia maneno yaleyale licha ya kuwa wanaotoa maneno hayo wanatambua kuwa hayana mantiki na yanaendelea kupuuzwa na jumuiya ya kimataifa kila kukicha.
Ndani ya muongo mmoja uliopita, mkoa wa Xinjiang umebadilika kutoka moja ya maeneo korofi yenye changamoto ya siasa kali na hata matukio ya kigaidi, lakini sasa mkoa huo umekuwa moja ya maeneo yanayotia matumaini, yanayovutia idadi kubwa ya wawekezaji wa ndani na hata wa nje, na watu wake kuwa watu wenye maendeleo.
Kwa watu wanaofahamu vizuri hali ya China wanajua wazi kabisa, kuwa kupata maendeleo kwa mikoa ya magharibi mwa China iliyokuwa nyuma kiuchumi, lilikuwa ni suala la muda tu. Sababu ni kuwa China ina kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya maendeleo ya maeneo hayo. Katika muongo mmoja uliopita wakati baadhi ya maeneo ya Xinjiang yalikuwa yakitatizwa na changamoto za usalama, kulikuwa na changamoto nyingine nyingi, kama vile za miundombinu, ajira na hata masoko kwa ajili ya bidhaa zinazozalishwa katika maeneo hayo.
Kutokana na maendeleo makubwa ya miundombinu, iwe ni ile ya reli, barabara na hata mawasiliano ya habari, maeneo mengi ya mkoa wa Xinjiang yameunganika na maeneo mengine ya China. Hali hii sio kama tu imetoa fursa kwa makampuni kutoka sehemu mbalimbali za China kwenda kuwekeza katika mkoa huo, bali pia imewezesha watu wa huko kuanzisha shughuli zao mbalimbali za kujiingizia kipato.
Kuongezeka kwa makampuni kutoka maeneo ya mashariki mwa China yenye maendeleo makubwa kiuchumi, kumetoa mchango mkubwa katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira. Na watu waliopata ajira kwenye makampuni hayo wamekuwa ni chanzo cha mapato kwa watu wanaojiajiri na wale walioanzisha shughuli ndogondogo za kujiingizia kipato.
Pengine uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya Tehama pia umeleta mabadiliko makubwa kwa wenyeji. Si jambo la ajabu kwa wenyeji hata wale walio katika maeneo ya ndani kabisa vijijini kuwa na mawasiliano ya simu na kuwa na internet, na sio jambo la ajabu kwa wenyeji kuangalia televisheni na kupata upeo mpana kuhusu maendeleo.
Bahati mbaya ni kuwa vyombo vya habari vya nchi za magharibi vinajenga picha mbaya ya Xinjiang, kama kwamba ni mkoa ambao watu wake wanaishi katika hali ngumu na taabu. Licha ya kuwa kiwango cha maendeleo ya mkoa huo bado hakijafikia kiwango cha mikoa ya mashariki mwa China, hali halisi ni kuwa watu wake wanafurahia maisha kama wenzao wa mashariki, na ni wazi kabisa kuwa ni suala la muda tu kwa mkoa huo na maeneo mengine ya magharibi mwa China kufikia maendeleo kama ilivyo mikoa ya mashariki.
Wahenga walisema “debe tupu haliachi kutika”. Ukweli umeonesha kuwa changamoto nyingi za usalama zilizojitokeza mkoani Xinjiang katika muongo mmoja au miwili iliyopita, kwa kiasi kikubwa zilitokana na vijana kukosa fursa. Vijana wa mkoa wa Xinjiang kwa sasa wanapata fursa nyingi iwe ni za kuajiriwa na hata kujiajiri. Utulivu uliopo sasa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya vijana kuwa shughuli za kufanya na kuondoa hali ya wao kutumika na watu wenye nia mbaya.