LGE2024 Mchungaji Dkt. Kimondo: Uchaguzi wa Serikali za Mitaa haukuwa wa haki, tudai Katiba Mpya

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024
Nov 19, 2024
83
275
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde Dkt. Steven Kimondo, ameeleza kusikitishwa kwake na mwenendo wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji akidai haukuwa huru na haki katika kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi ambao bado hali zao za kimaisha ni mbaya kwa sehemu kubwa.

Dkt. Kimondo amesema hayo katika mahojiano yake yake maalumu Jumatatu ya Desemba 16, 2024 ili kupata maoni yake baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Mchungaji huyo, amesema uchaguzi huo ulivurugwa na Serikali tangu mwanzo kwenye zoezi la uandikishaji wapiga kura kutokana na kushuhudiwa kwa dosari kadhaa hivyo kueleza uchaguzi huo kuwa haukuwa huru na haki na ulijawa na upendeleo, uenguaji wagombea wa vyama vya upinzani bila sababu za msingi na mengineyo.

"Nikija kwenye uchaguzi ambao mimi siamini kama ulikuwa uchaguzi kwa maana halisi ya uchaguzi ulivurugwa kwa makusudi kuanzia hatua za awali kabisa tangu kutungwa kwa sheria na kanuni za uchaguzi watu walilalamikia lakini hawakusikilizwa, kwenye uandikishaji kuna mambo ya ajabu yaliyotokea kama kuandikisha so watoto wadogo na marehemu lakini hata wakati wa uchaguzi tulisikia kulikuwa kura za wizi au kura bandia, lakini pia zaidi ya hayo tulisikia mauaji ya baadhi ya wagombea na watu wengine waliokuwa washiriki katika zoezi la uchaguzi, tulisikia mauaji huko Singida, Tunduma na mahali kwingine mauaji yaliyohusishwa na uchaguzi huo, watu walinyimwa haki ya kuchagua watu waliowataka wawe viongozi wao na wengine walinyimwa haki ya kuchaguliwa kuwa viongozi kwasababu ya taratibu zilivyowekwa”, ameeleza.

Kutokana na hayo, kiongozi huyo wa kiroho na mfuatiliaji wa siasa za Tanzania amewashauri wananchi kuungana kudai upatikanaji wa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi ambayo haitakuwa na upendeleo.

"Watanzania ninawaomba tuungane kukemea vitendo viovu vya uchaguzi nchini Tanzania. Naomba tuungane kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi ili katika chaguzi zinazofuata zifanyike zikiwa huru na haki wananchi waamue wao wanataka viongozi wa aina gani na wananchi wakishiriki maana yake wanakuwa na mamlaka ya kuwawajibisha iwapo wanakwenda kinyume na matarajio yao lakini pia wanakuwa tayari kushirikiana na viongozi hao kufanya shughuli za maendeleo. Kwahiyo kama tutakubaliana kuhusu katiba mpya ombi langu kwa wa-Tanzania tuanzie pale tume ya jaji Joseph Warioba ilipoishia kuna mambo mazuri ndani yake", amesisitiza Kimondo.

Mchungaji Dkt. Steven Kimondo anasema ikiwa mabadiliko hayatafanyika ikiwemo kubadili mifumo ya kiuchaguzi na kupata katiba basi uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 hautakuwa na tofauti na wa Serikali za mitaa mwaka 2024 akisema pia uchaguzi huu umeendana na ule wa 2019 wa viongozi waliopatikana kupita bila kupingwa.

Chanzo: Jambo
 
Back
Top Bottom