Mr Lukwaro
JF-Expert Member
- Jun 3, 2023
- 359
- 628
KANISA
Mchakato wa Mtumishi wa Mungu Mwl. J.K. Nyerere unaendelea!
Mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwamini mlei kutoka Jimbo Katoliki la Musoma, ulianzishwa na hayati Askofu Justin Samba, ukaboreshwa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma na sasa umefikishwa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania! Mchakato unaendelea! Salini!Na Padre Alfred Stanslaus Kwene, Butiama, Jimbo Katoliki Musoma.
UTANGULIZI: Wapendwa taifa la Mungu, tumsifu Yesu Kristo… Sinodi Musoma…! Karibuni kwa adhimisho hili la Misa Takatifu kwajili ya kumwombea Marehemu Mtumishi wa Mungu Julius Kambarage Nyerere. Desturi ya Kanisa Katoliki inatualika kuwaombea marehemu kwa nafasi mbalimbali, na moja kati ya nafasi hizo ni katika kumbukumbu ya kila mwaka katika tarehe ileile mmoja alipofariki.
Ni kwa msingi huo, tunaadhimisha leo Misa hii takatifu ikiwa ndo tarehe rasmi aliyofariki baba yetu wa Taifa Mwl. J.K. Nyerere, miaka 20 iliyopita. Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwafikishieni salamu za upendo kutoka kwa Mhashamu Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo hili la Musoma, ambaye alitamani kusali pamoja nasi leo hii, ila kwa sababu zisizoweza kuzuilika hakuweza na hivyo amenituma kumuwakilisha katika Ibada hii muhimu ya siku ya leo. Muwe na hakika yuko pamoja nasi kwa sala katika kuendelea kumwombea huyu mpendwa wetu Mwl. J.K. ambaye leo anatimiza miaka 20 tangu Mwenyezi Mungu amwite kwake.
Tunapoadhimisha Ibada hii ya Misa, ni nafasi yetu ya kuendelea kumshukuru Mungu kwa namna ya pekee, kwa zawadi ya maisha ya mtumishi wake – Mwl. J.K. Nyerere kwetu kama waamini wenzake wa Jimbo la Musoma na Taifa kwa ujumla, hasa kwa mazuri mengi aliyoyafanya wakati wa uhai wake, kwa urithi aliotuachia hivi kwamba hadi leo hii baada ya miaka hii 20 tangu kifo chake bado tunamkumbuka…bado anaendelea kuishi ndani ya mioyo yetu. Kwa ajili hiyo tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa ajili yeke. Ndugu zangu katika Kristo, inapotimia rasmi sasa miaka hii 20 tangu Mwl. J.K. Nyerere aage dunia, kitaifa kumekuwepo na fursa mbalimbali za kufanya rejea kwa yale mengi ambayo ametuachia kama urithi wake kwetu na pia kualikana kuyaenzi kila mmoja kwa nafasi yake. Wengi tumeshuhudia makongamano, warsha, midahalo na mkusanyo wa maoni mbalimbali yakifanyika kwa lengo hilo. Kwa vile hayo tayari yamekwishafanyika na bado yanaendelea kufanyika; katika muktadha huu kwa kiibada hususani katika tafakari yetu ndani ya adhimisho hili, nisingependa kujikita katika kuyarudia/kuainisha hayo tena.
Kwa tahadhari hiyo, ninapenda kuchukua nafasi hii, kwa namna ya pekee, kuwaalika tuitumie siku hii kuielekeza tafakari yetu juu ya mambo haya makuu mawili: MOSI, Mchakato wa Mtumishi wa Mungu - Mwl. J.K. Nyerere na nafasi/thamani yake kwetu: Kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya mchakato, ninapenda kwa nafasi ya kwanza, tukumbushane ya kuwa, tunafanya Ibada hii sio kwa heshima, bali ni ibada ya kumb./ya kumwombea… kwani kadiri ya miongozo ya MCHAKATO kwa ngazi ya sasa – ambapo yeye bado ni Mtumishi wa Mungu, haturuhusiwi kufanya ibada ya hadhara kwa heshima yake…wala kuipamba kwa shangwe (mf. hatuimbi Utukufu…) kwani ibada ya aina hiyo hufanyika kwa watakatifu.
Tafsiri rahisi ya kufanya ibada ya namna hiyo ni kuvuruga mchakato au kwa maneno mengine ni sawa na kujichukulia madaraka yasiyo yetu ya kumtangaza kuwa mtakatifu wakati kazi hiyo ni ya Vatican kupitia Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu ndiyo inayohusika. Ndio maana rangi ya Liturujia ya adhimisho hili ni URUJUANI…rangi ambayo kikanisa hutumika kwa ajili ya kipindi cha Majilio, Kwaresima na Misa za wafu. Aidha, ni kwa msingi huo huo ndio maana hata SALA ya kumwomba sio ya hadhara na imeandikwa kabisa “kwa matumizi binafsi”.
Ni vema ikaeleweka pia ya kuwa, Kanisa haliwafanyi watu kuwa watakatifu, bali linatangaza tu ya kuwa mmoja amefikia utakatifu baada ya kuwa na viashiria vingi vinavyodhihirisha hilo – ikiwemo miujiza. Hivyo basi ndugu zangu, kiu yetu ya kutamani kumuenzi siku moja Mwl. kama Mt. isitufanye tukadhani pengine Kanisa ndilo linalotuchelewesha tu! La hasha! Tunachotakiwa kufanya ni kuendelea kusali kuomba ili utakatifu wa huyu Mtumishi wa Mungu uweze kudhihirikwa wazi. Leo inapotimia miaka 20 tangu kifo cha Mwl. Nyerere na tangu kuanza kwa mchakato, ni dhahiri ya kuwa swali hili litajitokeza:
HIVI MCHAKATO UMEISHIA WAPI? Japo mimi sio msemaji rasmi kwa sasa juu ya hatua mchakato ulipofikia, ILA kwa ridhaa na maelekezo ya Baba Askofu Michael Msonganzila nimetumwa niwaelezeni tu kwa uchache sana kinachoendelea kwa sasa, hususani juu ya mabadiliko yaliyofanyika: Kwanza kabisa, ni vema ikaeleweka wazi ya kuwa MCHAKATO wa aliyekuwa mwamini mwenzetu, mwanajimbo la Musoma J.K. Nyerere kutangazwa kuwa Mtakafitu, haujafa bado unaendelea.
Ni ukweli usio na shaka kuwa mchakato wa Mwalimu ulianzishwa na Jimbo la Musoma kupitia Askofu wa wakati huo Hayati Justin Tetemo Samba, kadiri miongozo inavyoelekeza. Tangu wakati huo ulikuwa chini ya Jimbo Katoliki la Musoma. Isipokuwa, baada ya tathimini kubwa na kwa ushauri kutoka kwa wasimamizi wakuu wa mchakato huu (yaani postulators) ilionekena ni vema mchakato kuwa sasa chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa kuzingatia ya kuwa Mwl. kwa nafasi yake alikuwa na mguso wa kitaifa na kijimbo kuhamishiwa Jimbo Kuu la DSM – mahali ambapo Mwl. aliishi zaidi wakati wa uhai wake na alifahamiwa na wengi hata kama kwa kuzaliwa alikuwa ni muumini wa jimbo la Musoma. Kwa vile, anayeongea sio msemaji wa TEC na wala wa Jimbo Kuu la DSM, kwa sasa itoshe tu kwa hayo machache kuhusu kinachoendelea kuhusu mchakato, na niache nafasi kwa wahusika wakuu kadiri ya nafasi na watakavyoona inafaa, basi wanaweza kutoa maelezo zaidi.
PILI, ninawaalika tuitumie nafasi hii kutafakari pamoja juu wito msingi kwa kila mbatizwa – kuwa watakatifu (Mt. 5:48) Angalisho: Kwa upande wa Mwl. J.K. Nyerere tunaamini na kutumaini kuwa yeye kama mkristo alitamani kufikia utakatifu na bidii yake yote kwa yale mazuri aliyoyafanya ktk maisha yake ilikuwa ni kufikia azma hiyo – hivi kwamba ushuhuda juu ya maisha yake uliotakiwa kutolewa kama sharti msingi la kuruhusu mchakato kuanza uliweza kuleta ushawishi na Vatican kuridhia. Kanisa bado halijamtangaza rasmi kuwa mtakatifu.
Tunachoalikwa kufanya kwajili yake ni kusali ili utakatifu wake uweze kudhihirika wazi na hatimaye Kanisa siku moja liweze kumtangaza rasmi kuwa Mt. Kwa upande wetu sisi wengine, ningependa tukumbushane ya kuwa wito wetu msingi wa kuwa watakatifu, na ningeomba tafakari yetu tujikite zaidi hapo: Fumbo la maisha ya mwanadamu: Ndugu zangu, tunapotafakari juu ya wito wetu msingi wa kuwa watakatifu, ninamualika kila mmoja wenu, kwanza kutafakari juu ya fumbo la maisha yetu: maisha yetu ni zawadi kutoka kwa Mungu kwetu na pia yanabakia kuwa ni mali ya Mungu mwenyewe, nasi tumepewa tu dhamana ya kutunza tunu hii kubwa hivi.
Kwa kuzingatia kuwa ndani ya kanisa hili tuko watu wa Imani mbalimbali, ila kati ya mambo ambayo tunafanana kwa tulio wengi na pia yanashuhudiwa katika vitabu vikubwa vya rejea za mafundisho (Mf. Biblia na Msahafu), ni juu ya chimbuko la kila mmoja wetu, ya kwamba chanzo chetu ni Mungu mwenyewe. Aidha, ni vizuri tukakumbushana kuwa Mwenyezi Mungu ametuumba kwa mpango/malengo maalumu, hivi kwamba hakuna mwanadamu yeyote ambeye ni matokeo ya bahati mbaya. Kwetu sisi Wakatoliki, fundisho letu ni kuwa: Mwenyezi Mungu ametuumba ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake mbinguni.
Hivyo, tunapokuwa hapa duniani wajibu wetu na kumjua Mungu, kumpenda na kumtumikia, na ni pale tu tutakapoyafanya hayo vema, ndipo tutaweza kustahilishwa maisha ya umilele. Ndivyo hivyo alivyofundisha pia Mt. Augustine kwa kusema: Yeye aliyekuumba bila wewe, hawezi kukukomboa bila wewe! Yaani, pamoja na kuwa ukombozi wa jumla umekwishaletwa na Bwana wetu Yesu Kristo, ILA ukombozi wa mtu binafsi ni matokeo ya juhudi zetu!
Hivyo basi, wapendwa familia ya Mungu, tunaposali leo katika kumbukumbu hii, kila mmoja wetu anaalikwa kutambua ya kuwa hapa duniani tunapita na tujitahidi kuitumia vema nafasi hii ya uwepo wetu hapa duniani kama fursa ya kujitayarishia makao ya milele huko mbinguni, kwa kudumu katika matendo mema. Tunaalikwa kuchukua tahadhari ili tusije tukaishi hapa duniani kana kwamba tumefika, kana kwamba ndo mwisho wa reli, bali tujibidishe kujiwekea hazina mbinguni…kusikoharibika kitu kwa nondo wala kwa kutu. Ndivyo hivyo anavyotukumbusha Mtume Paulo katika Somo la Kwanza tulilolisikia: “Sisi wenyeji wetu uko mbinguni” (Fil. 3:20-21).
Kila mmoja wetu ajione analo deni la kuacha kumbukumbu nzuri hapa duniani ya kuweza kuenziwa hali tukijua hakika ya kuwa: hatutakumbukwa kwa kuishi miaka mingi hapa duniani, bali kwa mchango tutakaokuwa (legacy) tumeuacha kwa vizazi vitavyotufuatia. Mwaliko wa kuchuchumilia utakatifu ndo wito msingi kwa wote (Mt. 5:48): Kama tulivyoainisha hapo awali, mpango wa Mungu katika kumwumba mwanadamu ni ili mwisho safari yake hapa duniani aweze kufika mbinguni.
Ndivyo hivyo ambavyo Bwana wetu Yesu Kristo anatukumbusha katika mafundisho yake kupitia Hotuba ya Mlimani – “Basi muwe wakamilifu (i.e. watakatifu) kama baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”(Mt. 5:48) na pia kupitia mwaliko wa kuishi MAISHA YA HERI (Injili ya leo – Mt.5:1-12). Wito huu wa kuwa watakatifu ni wa kila mmoja na ndio maana kadiri ya mafundisho ya Kanisa, huu tunauita “universal call to holiness”. Waamini wote wakristo wa hali yoyote au daraja lolote huitwa kufikia utimilifu wa maisha ya kikristo na ukamilifu wa upendo (LG n. 40), yaani, kila mmoja kwa nafasi yake atafute utakatifu…kupitia mazingira yake. Kwa namna ya pekee, ninapenda kutilia mkazo juu ya mwaliko huu kwa waamini walei (baba, mama, dada, kaka, shangazi, mjomba, n.k.).
Ndugu zangu waamini walei, tunaposali leo katika kumbukizi hii ya mtumishi wa Mungu J.K. Nyerere, ambaye alikuwa muumini mlei - kwa nafasi yake kama baba wa familia, kama wengi wenu mlivyo…kila mmoja wenu akumbuke ya kuwa ameitwa kuwa mtakatifu. Kwa kufanya ulinganifu, katika historia, wengi wa watakatifu katika Kanisa wanakutwa kati ya makundi mawili, yaani, wakleri na watawa, na waamini walei ni kwa uchache.
Hali hii, isiwafanye walei mjione ya kuwa utakatifu hauwahusu, la hasha! Mnaitwa kuwa watakatifu kwa namna ya pekee kwa njia ya kutakatifuza malimwengu – kama ambavyo kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Halmashauri ya Walei Tanzania ambavyo imewaalika kutafakari mwaka huu 2019. Katika kuitikia wito huu, hakuna kungoja kesho…tukumbuke anavyotukumbusha Mtakatifu Josefu wa Alamano: “Uwe Mtakatifu sasa”. Katika kuuchuchumilia utakatifu, ni vema waamini walei mkatambua ya kuwa UTUME WENU MSINGI NI KUTAKATIFUZA MALIMWENGU. Maana yake ni nini?
Turejee katika Mtaguso wa II wa Vaticano katika hati yake inayoitwa “MWANGA WA MATAIFA” n. 31, na nukuu: “Ni juu ya walei, kutokana na wito wao, kuutafuta ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadiri ya Mungu. Wanaishi ulimwenguni, yaani katika kazi zozote na shughuli za kidunia na katika mazingira ya kawaida ya maisha ya kifamilia na ya kijamii, ambayo maisha yao yamefungamanishwa nayo. Hapo wanaitwa na Mungu kusaidia kuutakatifuza ulimwengu, kama kutoka kwa ndani, mithili ya chachu, katika kuyatimiza majukumu yao wenyewe, wakiongozwa na roho ya kiinjili, na hivyo wamdhihirishe Kristo kwa wengine, wakingaa hasa kwa ushuhuda wa maisha yao, imani, matumaini na mapendo.” (LG n.31)
Aidha, hati hii inaongeza na kukazia: “kama vile roho ilivyo mwilini, ndivyo wakristo wawe ulimwenguni” (LG n.38),“kila mlei hupaswa kuwa mbele ya ulimwengu shahidi wa ufufuko na maisha ya Bwana Yesu na ishara ya Mungu aliye hai. Yawapasa wote kwa pamoja, na kila mmoja kwa upande wake, kuulisha ulimwengu matunda ya kiroho” (Gal.5:22). “Lakini walei huitwa kwa namna ya pekee kuonyesha uwepo wa Kanisa na utendaji wake mahali pale na katika mazingira yale ambamo lenyewe haliwezi kuwa chunvi ya dunia, isipokuwa kwa njia yao tu.” (LG n.33) Bila shaka mnaweza kujiuliza: Malimwengu tunayotakiwa kuyatakatifuza ni yepi hayo?
kukuza/kuhamasisha juu ya hadhi ya binadamu, kulinda na kutetea haki msingi za binadamu na haki ya uhai, kukiri na kuhimiza juu ya uhuru wa kuabudu, kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama mazingira msingi ya ushiriki wa maisha ya jamii, ukarimu (charity) kama kichocheo na tegenezo la ushirikiano, kushiriki katika siasa, nafasi ya msingi ya mwanadamu katika maisha ya kijamii na uchumi, kuziinjilisha tamaduni zetu (iwe ni kwa ujumla wake au kwa tamaduni moja moja).
Mama Kanisa anatualika na kutuhimiza:kulinda na kutunza mazingira (our common home) nk. Kwa naneno mengine hati hii inataka kuturejesha katika fundisho la Mt. Francis wa Sales anayesema: “chanua ulikopandwa” na pia fundisho la Mtakatifu Mama Theresa wa Calcuta anayesema: “fanya mambo madogo kwa upendo mkubwa”. Tuhitimishe kwa kukazia tu kwa maneno haya mazito/ya msingi: iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.