SULEIMAN ABEID
JF-Expert Member
- Feb 26, 2013
- 390
- 385
1. 0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya wazazi wangu na pia nichukue nafasi hii kuwashukuru sana waheshimiwa wabunge, Chama cha Mapinduzi, Viongozi wa Serikali, ndugu jamaa na marafiki, Baba Askofu Peter Phares Kisena, Mtume Boniface Mwamposa na viongozi wengine wa dini kwa namna mlivyonifariji na kunitia moyo katika kipindi kigumu cha msiba wa Mama yangu mzazi, Marehemu Kephrine Kabula Masaga aliyefariki Juni 1, 2022 na kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha Baba yangu mzazi Marehemu Mzee Mpina Gabisi Samweli Luchemba aliyefariki Juni 14, 2021, pumzikeni wazazi wangu hamkuwa wazazi tu bali marafiki wakubwa, Mungu awapumzishe kwa amani. AMEEN.
2.0 PONGEZI NA SHUKRAN
Mheshimiwa Spika, nimesoma hotuba za Waziri zote mbili ya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23 pamoja na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2022/23. Kwa moyo wa dhati niipongeze Serikali ya awamu ya sita chini Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia vyema mikopo ya sekta binafsi ambapo imekua kutoka 4.3% mwaka 2020 hadi 8.4% mwaka 2021, lakini pia maamuzi ya kununua ndege tano mpya kwa mpigo ikiwemo ndege moja kubwa ya mizigo ambapo malipo ya awali yameshatolewa tayari, sambamba na hilo Serikali imesimamia vyema mwenendo wa shilingi ambapo fedha yetu imeimarika kwa wastani wa 0.03%.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nimpongeze sana Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuwa muwazi na mkweli katika mambo yanayotukwaza kupiga hatua kama taifa, ameeleza wazi namna ambavyo baadhi ya watumishi wa umma walivyogeuza mali za umma kuwa mali zao binafsi, wanavyojinufaisha na sheria ya manunuzi kupora mali za umma, matumuzi ya hovyo serikalini mfano safari za mara kwa mara Dar es Salaam wakati Makao Makuu ya nchi yapo Dodoma.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha amevunja rekodi tofauti na baadhi ya mawaziri wenzake ambapo wabunge tulipoibua hoja hizi tulioambiwa hatuipendi Serikali ya awamu ya sita na niwapotoshaji. Leo Waziri wa Fedha ameeleza ukweli juu ya mapungufu yakiundeshaji yaliyoko serikalini, ni muhimu kusema ukweli juu ya changamoto zilizopo ili kwa pamoja kuzitafutia ufumbuzi. Ni dhahiri Mheshimiwa Waziri amebeba dhamira ya kweli ya kizalendo kwa taifa letu.
3.0 KUUNDA TUME YA BUNGE
Mheshimiwa Spika, kutokana na baadhi ya mambo kulalamikiwa kwa muda mrefu na baadhi ya mawaziri kutoa majibu mepesi, majibu tofauti tofauti na yanayokinzana kwenye jambo moja, kuomba kufanyika ukaguzi na uchunguzi wa CAG, PCCB na PPRA jambo ambalo pia halikutekelezwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Bunge lako Tukufu linayo mamlaka ya kikatiba na kikanuni kuisimamia Serikali nakuomba ukubali pendekezo langu la kuunda Tume za kibunge ili kupata ukweli uliojificha katika hoja zifuatazo:-
(i) Malimbikizo na mapingamizi ya kodi yaliyofikia Shilingi Trilioni 12.6, Tume pamoja na mambo mengine iangalie sababu za mapingamizi mengi ya kodi kutokutolewa maamuzi kwa wakati na kushikilia kodi ya Serikali, sababu za TRA kushindwa kukusanya kodi katika mwaka husika wa fedha na kubaki na malimbikizo ya kodi (arrears) hali inayopelekea kupunguza mapato ya Serikali.
(ii) Ucheleweshaji wa miaka miwili kwa Mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP - MW 2,115), Tume pamoja na mambo mengine ikaangalie sababu za kuchelewa kwa mradi, nani anayebeba gharama za ongezeko la muda wa kutekeleza mradi, hatua iliyofikiwa ya ulipwaji wa CSR kiasi cha Shilingi Bilioni 260 na hatua aliyofikia mkandarasi ya kulipa faini ya ucheleweshaji wa mradi kiasi cha Shilingi Trilioni 1.3 kama vifungu vya Mkataba wa mradi vinavyosema.
(iii) Kupanda kwa Bei za Mbolea, pamoja na mambo mengine Tume iangalie uhalali wa bei za mbolea zinazosemwa ni za soko la dunia, kuangalia uhalali wa bei za mbolea zinazotolewa na wafanyabiashara wakati wa kuagiza na kusambaza mbolea nchini, sababu za kufutwa kwa mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System- BPS) na sababu za Serikali kuacha kufanya ulinganifu na mchujo wa awali (pre-qualifications) pamoja na kujiridhisha pasipo shaka juu ya ubora wa mbolea na bei halisi (due diligence) badala ya kutegemea taarifa za bei kutoka kwa wafanyabiashara (middle men). Huko nyuma utaratibu huu ulisaidia mbolea kupatikana kwa bei nafuu.
(iv) Kupanda kwa bei za mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa, pamoja na mambo mengine Tume iangalie uhalali wa bei za mafuta zinazotolewa na waagizaji wa mafuta na pia kujiridhisha na uhalali wa mchakato wa manunuzi unaosimamiwa na PBPA.
4.0 DENI LA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kwamba Deni la Serikali limeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 60.72 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia Shilingi Trilioni 69.44 mwezi Aprili 2022, hili ni ongezeko la deni la Shilingi. Trilioni 8.72 ambalo ni ongezeko la 14.4%
Swali la kujiuliza kwanini deni la Serikali liongezeke kwa Shilingi Trilioni 8.72 wakati katika mwaka husika deni limelipwa kwa zaidi ya Shilingi Trilioni 7.2 na wakati huo huo shilingi ya Tanzania iliimarika kwa wastani wa 0.03%, kama hizi takwimu ni za kweli maana yake Serikali imekopa zaidi ya Shilingi Trilioni 15 katika mwaka husika zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge cha Shilingi Trilioni 9.89 katika mwaka wa fedha 2021/2022. Waziri atoe ufafanuzi wa kina katika eneo hili ili kuondoa mkanganyiko uliopo.
Mheshimiwa Spika, Waziri anaeleza sababu za ongezeko la deni la Serikali limesababishwa na utoaji wa hatifungani maalum yenye thamani ya Shilingi Trilioni 2.18 kwa ajili ya kulipa deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Waziri aeleze ni kiasi gani kiliruhusiwa kwenda kukopwa kwa ajili ya deni la PSSSF katika Mwaka wa Fedha 2021/2022.
5.0 MAPATO YA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali imeshindwa kuainisha kwa kina mikakati ya kuziba mianya ya upotevu na ukwepaji kodi nchini licha ya eneo hili kupoteza mapato mengi ya Serikali na kuisababishia Serikali kushindwa kugharamia na kukidhi mahitaji muhimu kwa maendeleo ya wananchi. Waziri ameishia kutoa onyo badala ya kutueleza hatua alizochukua kwa watu wote waliofuja mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ukusanyaji wa mapato ya Serikali umeshuka kwa 0.2% katika mwaka wa 2020/2021, Serikali kupitia TRA hadi Aprili 2022 imekusanya mapato Shilingi Trilioni 17.20 katika lengo la mwaka la kukusanya Shilingi Trilioni 21.78 sawa 78.9%.
Aidha kiwango cha mapato ya kodi kwa uwiano wa pato la taifa ulipungua kutoka 12.1% mwaka 2019/2020 hadi kufikia 11.4% mwaka 2020/2021. Pia Tanzania iko nyuma sana katika ukusanyaji wa mapato kwa uwiano wa pato la taifa ikilinganishwa na nchi jirani za Kenya na Rwanda ambazo zina wastani wa zaidi ya 16%.
Hali hii ya ukusanyaji wa mapato inatupa picha kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na wizara na taasisi nyingine zinazokusanya mapato zina changamoto nyingi ambazo hazijabainishwa na hazijatafutiwa ufumbuzi hali inayopelekea kudorora kwa ukusanyaji wa mapato nchini. Nitumie nafasi hii kueleza maeneo matatu yanayopoteza mapato ya Serikali kwa kiasi kikubwa kama ifuatavyo:-
5.1. Malimbikizo ya madeni ya kodi
Mheshimiwa Spika, TRA kushindwa kukusanya kodi iliyohakikiwa na badala yake kubaki deni hadi kumalizika kwa mwaka wa fedha, takwimu zinaonyesha kuwa malimbikizo ya madeni yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka, mwaka 2018/2019 ilikuwa Shilingi Trilioni 2.1, mwaka 2019/2020 ilikuwa trilioni 3.87 na mwaka 2020/2021 ilikuwa Shilingi Trilioni 7.54, kwa takwimu hizi malimbikizo ya kodi yameongezeka kwa 94.6% lakini pia uwezo wa kukusanya kodi za malimbikizo nao unashuka ambao mwaka 2019/2020 ilikuwa 23% na mwaka 2020/2021 ni 10.4% tu
5.2 Kodi zilizoshikiliwa katika mamlaka za rufani
Mheshimiwa Spika, Mapingamizi ya kesi za kodi katika mwaka wa fedha 2020/2021 ilifikia kiasi cha Shilingi Trilioni 5.19, mapato haya yanashikiliwa kwenye mamlaka za rufani za kodi kwa muda mrefu katika Mahakama ya Rufaa (CAT), Baraza la Rufani za Kodi (TRAT) na Bodi ya Rufani za Kodi (TRAB) zikisubiri kesi zake kutolewa maamuzi ili mapato ya Serikali yakusanywe.
Sababu za kuchelewa kutolewa maamuzi ya rufaa za kesi hizi za kodi eti inaelezwa kuwa ni pamoja na upungufu wa wataalamu, bajeti ndogo, kukosekana kwa akidi ya wajumbe wa kusikiliza kesi za kodi katika mamlaka za rufani na kuchukua muda mrefu wa mazungumzo nje ya Mahakama.
Mheshimiwa Spika, ukichukua malimbikizo ya madeni ya kodi na mapingamizi ya kesi za kodi katika mamlaka za rufani inafikia jumla ya kiasi cha Shilingi Trilioni 12.6, kutokukusanywa kwa fedha hizi kunaifanya Serikali ikose uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu katika Taifa.
5.3 Uhamishaji wa bei ya mauziano ya bidhaa na huduma baina ya makampuni yenye mahusiano kimataifa (Transfer Pricing-TP)
Mheshimiwa Spika, TRA kupitia kitengo chake cha International Tax Unit (ITU) ina uwezo mdogo wa kufanya ukaguzi wa miamala ya kimataifa ambayo inafanywa na makampuni yenye mahusiano katika uhamishaji wa bei ya mauziano ya bidhaa na huduma (Transfer Pricing Audits). Hivyo ni vigumu kwa nchi kutambua na kukusanya kodi stahiki inayotakiwa kulipwa katika miamala ya TP. Hali inayopelekea Serikali kushindwa kukusanya mapato stahiki.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG miamala ya Transfer Pricing iliyofanyiwa ukaguzi katika mwaka wa fedha 2019/2020 ni makampuni 6 kati ya makampuni ya kimataifa (MNC’s) 504 sawa na asilimia 1.2 tu ya makampuni yote yaliyotakiwa kufanyiwa tathmini na ukaguzi na TRA. Makampuni ya kimataifa (MNC’s) hapa nchini ni makampuni ya simu, madini, nishati ya mafuta, gesi, mbolea nk. Eneo hili ndipo waliko walipa kodi wakubwa (Large Taxpayers) na kama lisipofanyiwa tathmini ya kina taifa letu litaendelea kupoteza mapato makubwa.
Lakini kila tunapouliza ni sababu gani hasa zinazotufanya tushindwe kukagua miamala ya TP unaambiwa ni ukosefu wa fedha na wataalamu wa kutambua miamala ya aina hii. Majibu ambayo hayaingii akilini hata kidogo.
Mheshimiwa Spika, Tumeshuhudia hapa baadhi ya wizara kupata mgao wa 3.6% tu ya fedha za maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge na baadhi ya wizara kushindwa kutekeleza miradi mipya ya maendeleo lakini pia tumeshuhudia hapa bungeni wabunge wengi wamelia juu ya shida zinazowakabili wapiga kura wao, tumeshuhudia hadi sarakasi kupigwa ndani ya Bunge, wabunge wengine waliangua vilio bungeni kwa uchungu na wengine kupiga magoti huku wengine wakihoji kwa hisia kubwa na kutaka kuondoa shilingi ya mawaziri. Hii yote ilikuwa ni kuonyesha na kuthibitisha ukubwa wa mateso waliyonayo wapiga kura wetu. Hongereni sana waheshimiwa wabunge tuungane kwa pamoja kuishikiza Serikali kuondoa changamoto zote za ukusanyaji mapato ili kuongeza mapato ya Serikali.
6.0 RANCHI YA TAIFA YA KONGWA KUGEUZWA SHAMBA LA ALIZETI
Mheshimiwa Spika, Ranchi ya Kongwa ilianzishwa kwa ajili ya mifugo tangu enzi za ukoloni ili kuendeleza Koosafu bora za mifugo, biashara na kuwa shamba darasa kwa wafugaji, leo linageuzwa kuwa shamba la alizeti kwa kisingizio cha kuwa na mifugo michache. Kama mifugo ni michache kwanini isiongezwe? Je hakuna mashamba yaliyowazi ya kuendeleza zao la alizeti? Au ndio njama za kutaka kuuza mali za taifa kwa watu binafsi? Shamba hili lina miundombinu muhimu kama majosho, maji, mabwawa, mazizi na malisho leo mnakwenda kubomoa miundombinu hiyo muweke shamba la alizeti HAPANA!!.
7.0 CHANGAMOTO ZA MANUNUZI YA UMMA NCHINI
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni zake za Mwaka 2013 (na marekebisho yake ya Mwaka 2016), Sheria hii imekuwa ikivunjwa kwa makusudi na baadhi ya watumishi wa umma kwa masilahi binafsi, lakini pia yapo mapungufu ya kisheria ambayo yanapelekea kutokupata bei halisi ya bidhaa au huduma hali inayopelekea hasara na matumizi makubwa ya Serikali yasiyokuwa na tija. Naomba kufanya uchambuzi mdogo kama ifuatavyo:-
(i) Sheria inataka mzabuni au mkandarasi achaguliwe kwa njia ya ushindani na awe na bei ndogo kuliko wengine (The lowest evaluated bidder) hata kama bei zake ni kubwa kuliko bei za soko (Market price) Hali hii inapelekea kutokupata bidhaa au huduma kwa wakati na kwa bei halisi (Value for Money). Suala hili limelalamikiwa kwa muda mrefu lakini marekebisho ya Sheria hayajafanyika mpaka sasa.
(ii) Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Manunuzi kwa visingizio mbalimbali kama maamuzi ya kutumia utaratibu wa manunuzi wa moja kwa moja bila ushindani (single source) na force account hata kwa miradi isiyokidhi matakwa. Mfano mchakato wa manunuzi unaondelea wa ujenzi wa Reli ya SGR kipande cha Tabora- Kigoma Km 514, ambapo ametenda mkandarasi mmoja tu Kampuni ya CCECC kwa utaratibu wa single source, kwa maelezo yoyote yale mradi huu hauwezi kutolewa kwa utaratibu wa single source na huu ni uvunjifu mkubwa wa Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPA) na Sheria ya Ushindani (FCA).
Lakini jambo jingine kuhusiana na mchakato huu linaloleta mkanganyiko ni Waziri wa Fedha kueleza kuwa Serikali imeanza mchakato wa kutafuta mkandarasi huku akiweka bayana thamani ya mradi kuwa ni Dola za Marekani Bilioni 2.1, Waziri amewezaje kupata gharama za mradi kabla mkandarasi hajapatikana na kama ni makisio ya wahandisi (Engineering Estimates) kwa nini yametangazwa hadharani wakati huwa ni siri ya Serikali.
(iii) Taarifa za ukaguzi wa Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) haiwasilishwi na kujadiliwa bungeni kama inavyofanyika kwa Taarifa ya CAG licha ya umuhimu wake na takribani 70% ya bajeti ya Serikali ni manunuzi. Taarifa ya ukaguzi ya PPRA hueleza kwa kina namna ambavyo taasisi nunuzi zimezingatia matakwa ya Sheria (compliance) lakini pia hueleza kama manunuzi yaliyofanyika yana thamani halisi (value for money), kitendo cha taarifa za ukaguzi za PPRA kutofanyiwa kazi kuna acha ufa mkubwa wa kupigwa mali za umma. Sheria ya Ukaguzi wa Umma (PAA) ifanyiwe marekebisho ili kuwezesha taarifa ya ukaguzi wa PPRA kuwasilishwa bungeni.
8.0 UTEKELEZAJI WA MAAMUZI YA MH. RAIS
Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa Mheshimiwa Rais baada ya kuwa tumepitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo hapa bungeni aliagiza fedha za ruzuku ya mbolea zipunguzwe na zipelekwe kwenye kilimo kikubwa nanukuu maelekezo yake kupitia Taarifa kwa Vyombo vya Habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Mei 19, 2022 “ Rais Samia amesema kilimo cha maeneo makubwa kitasaidia kuondoa uhaba wa bidhaa mbalimbali kama mafuta ya kula hivyo amemuagiza Waziri wa Kilimo kupunguza bajeti ya matumizi ya mbolea na kuelekeza fedha hizo kwenye kilimo kikubwa” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango haijaonyesha namna yalivyoshughulikiwa maagizo ya Mheshimiwa Rais ili kupata umbile halisi la bajeti ya Wizara ya Kilimo na baadaye kupitishwa na Bunge.
9.0 UKUAJI WA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa IMF uchumi wa dunia umekua na ukuaji hasi wa 3.1% (2020) ikilinganishwa na ukuaji chanya wa 6.1% (2021), SADC uchumi wake umekua ukuaji hasi wa 4.3% (2020) ikilinganishwa na ukuaji chanya wa 4.2 (2021), EAC uchumi umekua na ukuaji hasi wa 1.1% (2020) ikilinganishwa na ukuaji chanya wa 5.9% (2021).
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania ukuaji wa uchumi wa taifa mwaka 2021 ulikuwa kwa 4.9% ikilinganishwa na ukuaji wa 4.8% mwaka 2020. Tanzania imekuwa ni kati ya nchi chache Afrika na duniani ambazo uchumi wake uliendelea kuwa imara licha ya changamoto ya janga la Uviko-19.
Mheshimiwa Spika, hii ilitokana na msimamo wa mkuu wa nchi kukataa masharti magumu ikiwemo lockdown katika kupambana na janga la Uviko-19. Na hapa nashindwa kujizuia kumpongeza Bulldozer Hayati Dk. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa misimamo yake ambayo imeleta neema kubwa katika Taifa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio haya makubwa yako maswali ya kujiuliza, inakuaje leo baadhi ya nchi za Afrika ambazo zilikuwa na ukuaji hasi kuwa na ukuaji wa uchumi mkubwa zaidi kuliko Tanzania ambayo uchumi wake ulikua kwa ukuaji chanya wa 4.8% kipindi cha janga la Uviko-19? Lakini pia nini kinachosababisha kudorora kwa ukuaji wa uchumi Tanzania?
10.0 MFUMKO WA BEI
Mheshimiwa Spika, pamoja na sababu zinazotajwa za Uviko-19 na Vita vya Ukraine na Urusi kuwa ni sababu ya mfumko wa bei unaondelea hivi sasa lakini zipo sababu nyingine ambazo zinatokana na kukosekana kwa uadilifu na usimamizi makini kutoka kwa baadhi ya watendaji na viongozi wa Serikali na kwa bahati mbaya bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha haina mikakati madhubuti ya kushughulika na mfumko wa bei unaowatesa watanzania kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, mkakati pekee ulioelezwa na Waziri wa Fedha ni wa kikodi, misamaha ya tozo na kodi pekee haiwezi kutatua tatizo kubwa la mfumko wa bei lililopo nchini. Ili kutatua tatizo hili kunahitaji usimamizi makini wa biashara za bidhaa na huduma zote muhimu ikiwemo chakula, mbolea, mafuta ya kula, nishati ya mafuta na gesi na vifaa vya ujenzi.
Mheshimiwa Spika, ni muhimu kupata bei halisi ya bidhaa na huduma muhimu kutoka kwenye chanzo kwa kufanya ziara, ulinganifu na mchujo wa awali kwa wazalishaji katika viwanda mbalimbali duniani (pre-qualifications) na kujiridhisha pasipo shaka juu ya bei na ubora kabla ya kuagiza (due diligence) badala ya kutegemea taarifa za bei kutoka kwa wafanyabiashara pekee (middle men) ambao baadhi yao wamekuwa wakidanganya na kupandisha bei kiholela. Pia Kuwepo na usimamizi imara wa michakato ya manunuzi yenye uwazi, bila upendeleo na isiyogubikwa na rushwa.
11.0 KUCHELEWA KUKAMILIKA KWA MPANGO WA CREDIT RATING
Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuifanya Tanzania kuingia katika mpango wa kimataifa wa credit rating ulianza tangu Serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi ya Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ni nini kinachopelekea mpango huu mzuri kusuasua utekelezaji wake?.
12. 0 MISAMAHA YA KODI
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Waziri wa Fedha haijatoa tathmini ya misamaha ya kodi iliyokwishatolewa miaka ya nyuma ili kuendelea kujenga uhalali wa kuendelea kusamehe, kuanzisha au kufuta na kutoza kodi husika. Zipo taarifa kuwa misamaha mingi ya kodi haitoi unafuu wa bei kwa wananchi kama lengo la kutolewa misamaha hiyo ambapo pia hili Waziri amelieleza katika hotuba yake. Lakini pia inaonyesha hakuna usimamizi thabiti wa misamaha ya kodi inapotolewa. Eneo hili lisiposhughulikiwa kikamilifu haliwezi kuleta tija tarajiwa na badala yake litaendelea kutumika kama uchochoro cha kujipatia rushwa na kufanya ufisadi kwa baadhi ya watumishi wa umma wasio waadilifu, Kuleta ushindani usio sawa na kuikosesha Serikali mapato.
13. 0 MAREKEBISHO YA SHERIA
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha amependekeza kufanyiwa marekebisho baadhi ya Sheria ili kuleta mazingira bora ya ufanyaji biashara na utozaji kodi nchini, kwa sehemu kubwa naunga mkono mapendekezo yake lakini baadhi ya mapendekezo hayo yana changamoto kubwa na kama yatapitishwa na Bunge yataleta athari kubwa kwenye Taifa. Naomba kutaja baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:-
(a) Waziri wa Fedha kupewa mamlaka ya kusamehe Kodi ya ongezeko la thamani na Kodi ya mapato kwa wawekezaji mahiri baada ya kuidhinishwa na NISC, changamoto ya maamuzi haya ni kama ifuatavyo:-
(i) Misamaha kutolewa kwa baadhi ya wawekezaji walioko katika sekta husika kutaondoa ushindani wa haki na usawa baina yao, hali hii inaweza kupelekea kufungwa kwa viwanda vingine kutokana na kushindwa kushindana na viwanda vilivyopewa msamaha. Maamuzi haya pia ni kuvunja Sheria ya Ushindani Na 8 ya mwaka 2003 lakini pia tufahamu suala la ushindani ni global principle.
(ii) Misamaha ya kodi ya mtu mmoja au kikundi cha watu kinaweza kupelekea kufanyika upendeleo, rushwa na ufisadi mkubwa na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
(iii) Vivutio vya wawekezaji sio misamaha ya kodi pekee isipokuwa ni uboreshaji wa miundombinu muhimu ya kiuchumi kama umeme wa uhakika na wa gharama nafuu, bandari, barabara, reli, upatikanaji wa malighali na masoko pamoja na usalama wa nchi .
(b) Waziri wa Fedha na Mipango kupitia marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi amepewa mamlaka ya kusamehe faini na riba ya madeni ya kodi, changamoto ya mapendekezo haya kama yatakubaliwa na Bunge ni kama ifuatavyo:-
(i) Tunazo mamlaka za rufani za kodi ambazo kazi yake ni kutathmini kisheria maombi ya mrufani na kutolea uamuzi wa haki na bila upendeleo, kwanini jukumu hili linapelekwa kwa Waziri?
(ii) Waziri wa Fedha anayo majukumu mengi ya kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali hawezi kujigeuza tena kuwa Mahakama ya warufani.
(iii) Kama eneo la utozaji faini na riba ya madeni ya kodi lina changamoto kiasi cha walipakodi kushindwa kulipa kwanini lisifanyiwe marekebisho badala ya kufanya kusubiri kuombwa kutoa msamaha
(c) Waziri wa Fedha amependekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ambapo 5% ya mapato ya Halmashauri yatumike kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na masoko ya wamachinga na hivyo kubakiza 5% tu ya mikopo ya kinamama, vijana na wenye ulemavu, endapo maamuzi haya yatakubaliwa na Bunge yataleta athari zifuatazo:-
(i) Suala hili lilihitaji tathmini kwanza kabla ya kuanza utekelezaji, huwezi kuridhiria 5% ya mapato ya Halmashauri bila kujiridhisha mahitaji ni kiasi gani, unao machinga wangapi unaowajengea hiyo miundombinu, wanahitaji soko au miundombinu yenye ukubwa gani?
(ii) Shughuli zinazofanywa na machinga wanaotembeza bidhaa ndogo ndogo huku na kule za soksi, ice cream, korosho, maji, soda, mahindi ya kuchoma, wauza magazeti, mama ntilie wanahitaji hiyo miundombinu na masoko? Maana yasije kufanyika maamuzi ambayo yatalitia hasara Taifa na mwisho wa siku masoko na miundombinu hiyo ikaishiwa kutelekezwa bila kutoa huduma na mifano mingi ya masoko yaliyotelekezwa tunayo.
(iii) Uamuzi wa kupunguza fedha ya mikopo ya mitaji ya akina mama, vijana na wenye ulemavu kutoka 10% hadi 5% kunapunguza wigo wa utoaji mikopo kwa makundi hayo muhimu na hivyo kukwamisha dhamira njema ya Serikali kuyakwamua kiuchumi makundi hayo.
Fedha za mikopo inakuwaje zibadilishiwe matumizi na kupelekwa kwenye ujenzi wa miundombinu na masoko ya wamachinga kinyume na sheria iliyoanzisha mfuko huo. Kupunguzwa kwa mikopo hiyo kunawaathiri hata machinga wenyewe waliotegemea kupata mitaji kupitia mikopo hiyo, jambo la kusikitisha mambo haya yanafanyika kukiwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.
(d) Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Korosho kwamba fedha za ushuru wa usafirishaji wa korosho nje ya nchi zigawanywe 50% ipelekwe Wizara ya Kilimo na Mfuko wa Kilimo (ADF) na 50% nyingine ipelekwe Mfuko Mkuu wa Serikali, changamoto zilizopo ikiwa pendekezo hili litapitishwa na Bunge ni kama ifuatavyo:-
(i) Serikali iliweka utaratibu wa kisheria kuondoa retention zote kwenye wizara na taasisi za Serikali, haya maamuzi yanayopendekezwa na Waziri wa Fedha ya kupeleka 50% ya mapato yatokanayo na ushuru wa usafirishaji korosho nje ya nchi kupelekwa Wizara ya Kilimo yana msingi gani kisheria.
(ii) Tunayo mazao mengi yanayotozwa ushuru wa usafirishaji nje ya nchi (export levy) kama mazao ya mifugo na uvuvi, kwanini mgawanyo wa mapato unapendekezwa kwa zao moja tu la korosho?
(e) Waziri wa Fedha anapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Bima kwa kuongeza wigo wa bima ya lazima (mandatory insurance) kwa kujumuisha masoko ya umma, majengo ya biashara, bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje, vyombo vya baharini na vivuko. Hatua hii inalenga kuimarisha ushirikishwaji wa kifedha (financial inclusion) na kuongeza matumizi ya bima. Maamuzi haya yana changamoto zifuatazo:-
(i) Suala hili linaongeza bajeti katika Serikali za mitaa ambapo kwa sasa zimekwishapitisha bajeti yake hivyo kitendo cha kuingiza masoko na minada bila maandalizi ya kutosha kukatiwa bima kunaweza kuathiri bajeti zilizopitishwa katika Serikali za Mitaa
(ii) Kuamua bidhaa zote kutoka nje ya nchi kukatiwa Bima huku Storage na Transportation facilities zikiwa zimekatiwa bima ni jambo halieleweki hiyo bima inayokatwa katika bidhaa ni kwa ajili ya nini, lakini pia suala hili linaongeza gharama kwa walaji wa mwisho. Tunafanya maamuzi haya huku tukijua taifa liko kwenye mfumko mkubwa wa bei na ugumu wa maisha kwa wananchi wetu.
14.0 MWENENDO WA BEI ZA MBOLEA NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hapo awali sababu za kupanda kwa bei ya mbolea ukiacha sababu za vita ya Urusi na Ukraine na janga la UVIKO – 19, hazikuweza kuelezwa kikamilifu. Kwa kuwa wewe ndiye Waziri wa Fedha mwenye dhamana ya kusimamia sera za fedha na bajeti (Fiscal and Monetary Policies) naomba leo tupate maelezo ya kina kwa nini Serikali imeshindwa kudhibiti upandishaji holela wa bei za mbolea unaoongezeka kila uchao, naomba kufanya uchambuzi katika eneo hili kama ifuatavyo:-
Taarifa zinazotolewa na Serikali kuhusu kuongezeka kwa bei katika soko la dunia zinakinzana mfano Waziri wa Kilimo wakati akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 alikuja na takwimu za vyanzo viwili vya taarifa Wizara na Kilimo na World Bank alisema katika chanzo cha Wizara ya Kilimo bei ya mbolea ya DAP kwa sasa ni Dola za Marekani 1,012 lakini katika Chanzo cha World Bank ni Dola za Marekani Dola 948 (bei hizi ni tofauti kwa Dola za Marekani 64). Upande wa Mbolea ya UREA alisema bei ya mbolea kwa sasa ni Dola za Marekani 1,214 katika chanzo cha Wizara ya Kilimo wakati katika chanzo cha World Bank alisema bei ya mbolea kwa sasa ni Dola za Marekani 723 (tofauti ya Dola za Marekani 491).
Kutokana na due diligence pamoja na zabuni za BPS, TFRA iliweza kufanikiwa kupata bei ndogo sana za mbolea viwandani ikilinganishwa na bei ambazo wafanyabiashara walikuwa wakizisema. Licha ya hapo, kutokana na kurahisishwa sana kwa taratibu za uagizaji wa mbolea ambao uliwezesha hata wasio na uzoefu kabisa na mifumo ya uagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi vikiwemo vyama vya ushirika kushiriki kuagiza mbolea lakini pia ingewezesha ukawepo hata mpango wa wakulima kupata mbolea kupitia mazao yao katika utaratibu wa mikataba ya utatu (tripartite contracts) kama ulivyoshauriwa katika utafiti wa shirika la chakula na kilimo la umoja wa Mataifa (FAO) mwaka 2017 kwenye tovuti ya FAO Publication card | FAO | Food and Agriculture Organization of the United Nations.
(iii) Kusitishwa kwa bei elekezi na usimamizi dhaifu wa bei elekezi ya mbolea. Hali hii imepelekea kukosekana kwa bei inayozingatia gharama halisi ya kununua kiwandani, kuondosha bandarini na kuisambaza mbolea hadi kwa wakulima ambapo kumewafanya baadhi ya wafanyabiashara kupanga na kupandisha bei kiholela/watakavyo kwa maslahi binafsi na baadaye kusingizia UVIKO -19 na Vita huku tukiwaumiza wakulima wetu nchini.
Waraka wa mwisho wa bei elekezi ulitolewa Novemba, 2020 ambapo ilipofika Julai 2021 Waziri wa Kilimo wa kipindi hicho alifuta bei elekezi na kuruhusu wafanyabiashara waingize na kusambaza mbolea nchini bila kufuata bei elekezi na mfumo wa zabuni wa BPS. . Hata hivyo ilipofika Machi 2022 ulitolewa waraka mwingine na Wizara ya Kilimo ingawa pamoja na kuwepo bei elekezi hizo hazifuatwi na Serikali haisimamii kikamilifu kuzuia hali hiyo. Kitendo cha Serikali kufuta na kushindwa kusimamia bei elekezi ya mbolea ni kuvunja kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya mbolea ya mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea za mwaka 2011 zilizopitiwa upya mwaka 2017.
Hivyo kinachoendelea kwenye soko la mbolea ni ukiukwaji wa bei elekezi za mbolea kwani mara tu baada ya kuacha usimamizi wa bei elekezi, bei zilifumka kama mara mbili ya bei elekezi zilizokuwepo na hazijawahi kushuka tena. Wakati Serikali inaanza kusimamia bei elekezi na mfumo wa BPS bei za mbolea zilizokuwepo zilipungua kutoka wastani wa shilingi 100,000 hadi shilingi 40,000 kwa mfuko wa kilo 50 msimu wa kilimo 2017/2018.
Katika kikao alichofanya na wafanyabiashara wa mbolea mwezi Machi, 2022 Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amekiri mwenyewe kwamba wafanyabiashara wamekuwa wakipandisha bei holela kwa sababu Wizara kupitia TFRA iliacha kusimamia bei elekezi za mbolea (Taarifa hii ilichapishwa Machi 15, 2022 kwenye YouTube channel ya Wizara ya Kilimo https://youtu.be/jqhud_PYR-o )
Mheshimiwa Spika, Tumeuliza maswali kwenye Wizara husika ambayo yamekosa majibu, tuambiwe kuna maslahi gani ya umma yaliyotokana na kusitishwa bei elekezi? Kwa lugha nyingine, wakulima wamenufaika nini na kusitisha bei elekezi za mbolea? baada ya kufuta BPS na bei elekezi, bei ya mbolea imeshuka? Kinachodhihirika wazi baada ya kufuta BPS na bei elekezi bei za mbolea zilianza kuongezeka kwa kasi kubwa na hii ilikuwa kabla ya vita vya Urusi na Ukraine havijaanza.
(iv) Nchi jirani na zingine zinatumia bandari yetu ya Dar es Salaam kama Malawi, Zambia, DRC, Burundi na Rwanda lakini bei za mbolea ziko chini ikilinganishwa na sisi wakati tunanunua sehemu moja kwenye soko la dunia.
Maelezo ya kwamba bei katika nchi hizo ni ndogo kwa sababu zina ruzuku yanatiliwa mashaka kwa kuwa kabla ya kufuta BPS na bei elekezi hapa nchini kwetu bei ilionekana kuwa chini kuliko hizo nchi jirani na ndiyo maana kipindi hicho kulikuwa na presha kubwa ya utoroshaji wa mbolea kutoka nchini kwenda nchi jirani. upo ushahidi kutoka kwa wakuu wa Wilaya zinazopakana na nchi hizo kuonesha kwamba mbolea za Tanzania zilikuwa zikikamatwa wakati zikitoroshwa kwenda nchi hizo kwa vile bei ya mbolea za Tanzania ilikuwa ndogo kuliko bei katika nchi hizo mfano ni Taarifa ya TBC saa mbili usiku Januari 25, 2018 zilizochapishwa kwenye YouTube ya Global TV .
Usimamizi dhaifu unathibitishwa pia na hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Kilimo kwenye ibara ya 89 ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ilipokwenda kufanya ukaguzi iliibua mambo mazito ikiwemo kuuzwa kwa mbolea zisizosajiliwa aina 9, mbolea kuuzwa bila vibali, kuuzwa mbolea zilizofunguliwa na uwepo wa mbolea zenye uzani mdogo ikilighanishwa na vipimo.
(v) Utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi, hakuna mkazo wa kutumia mbolea za asili kama Samadi na Mboji zitokanazo na vinyesi vya mifugo na mabaki ya mazao mashambani. Mifugo yetu inazalisha matani kwa tani ya samadi kila siku lakini aina hii ya mbolea haitumiki kikamilifu na tuko bize kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi. Katika hotuba ya Waziri sijaona mkazo, mkakati wala bajeti katika tasnia hiyo ambapo mifugo yetu ndio kiwanda cha malighafi na uzalishaji unafanyika kila siku, mbolea inapatikana kiurahisi na kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema ya Serikali ya kutenga ruzuku ya mbolea kwa wakulima kiasi cha Shilingi Bilioni 150 lakini kwa vile mfumo wa ruzuku huko nyuma ulisitishwa kutokana na kugubikwa na rushwa, upendeleo na taarifa za kughushi (malipo hewa ya mbolea), Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa changamoto zilizosababisha mfumo wa ruzuku kusitishwa zimeshughulikiwa kabla ya kuanza utaratibu mpya wa utoaji wa ruzuku ili kuhakikisha kuwa ruzuku itakayotolewa na Serikali itumike kulipia ‘bei halisi’ ya mbolea na kuleta unafuu mkubwa wa bei kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Spika, hiyo fedha ya ruzuku iliyotolewa na Serikali kiasi cha Shilingi Bilioni 150 kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa bei ya sasa itaweza kuingiza tani 64,000 tu ambayo itatosheleza 25% ya mahitaji ya mbolea aina DAP na UREA ambayo ni tani 250,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, ruzuku pekee haiwezi kupunguza bei za mbolea nchini na pengine inaweza kupanda zaidi na wananchi kukosa unafuu wowote hivyo ni lazima Serikali ipitie upya mfumo wa uagizaji na usambazaji wa mbolea nchini ili kurekebisha kasoro zote zinazosababisha bei ya mbolea kupanda kila uchao. Mfumo wa BPS na bei elekezi ambao umefutwa kinyume cha sheria urejeshwe. Aidha ni muhimu kuweka mikakati thabiti ya kuongeza kasi ya uzalishaji katika viwanda vya mbolea nchini, pia kuweka mkazo katika uzalishaji na usambazaji wa mbolea za asili.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ushauri mwingi umekuwa ukitolewa kuhusu mwenendo wa bei za mbolea nchini lakini Serikali imekuwa na kigugumizi kusimamia na kutekeleza ushauri huo nakuomba uridhie kuundwe kwa Tume huru ya Bunge ili kuchunguza mambo yote kwa kina yanayosababisha kupanda kwa bei za mbolea nchini na Bunge lako Tukufu kutoa maelekezo kwa Serikali hatua za kuchukua.

- Mheshimiwa Spika, Kitendo cha Waziri wa Kilimo kuwasilisha taarifa mbili tofauti za mwenendo wa bei za mbolea katika soko la dunia kwenye Bunge lako tukufu alikuwa ana maanisha nini? Ni takwimu zipi zichukuliwe kama taarifa rasmi za Bunge, Kwa nini kila tunapouliza bei za mbolea zinatumika takwimu za soko la dunia pekee badala bei halisi ya makampuni yanayoagiza mbolea kutoka viwandani na nchi husika kama Falme za Kiarabu, Qatar, China, Misri, Norway, Morroco, Ubelgiji nk.
- (ii) Kufutwa kwa mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System - BPS) mwezi Julai 2021, ambapo Waziri wa Kilimo wa kipindi hicho alieleza kuwa mfumo huo ulikuwa unasababisha bei ya mbolea kuwa juu na mbaya zaidi Zabuni za BPS zilizokuwa kwenye mchakato zilifutwa na hii ni kinyume cha Kanuni ya 7(4) ya Kanuni za Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja za mwaka 2017.
Kutokana na due diligence pamoja na zabuni za BPS, TFRA iliweza kufanikiwa kupata bei ndogo sana za mbolea viwandani ikilinganishwa na bei ambazo wafanyabiashara walikuwa wakizisema. Licha ya hapo, kutokana na kurahisishwa sana kwa taratibu za uagizaji wa mbolea ambao uliwezesha hata wasio na uzoefu kabisa na mifumo ya uagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi vikiwemo vyama vya ushirika kushiriki kuagiza mbolea lakini pia ingewezesha ukawepo hata mpango wa wakulima kupata mbolea kupitia mazao yao katika utaratibu wa mikataba ya utatu (tripartite contracts) kama ulivyoshauriwa katika utafiti wa shirika la chakula na kilimo la umoja wa Mataifa (FAO) mwaka 2017 kwenye tovuti ya FAO Publication card | FAO | Food and Agriculture Organization of the United Nations.
(iii) Kusitishwa kwa bei elekezi na usimamizi dhaifu wa bei elekezi ya mbolea. Hali hii imepelekea kukosekana kwa bei inayozingatia gharama halisi ya kununua kiwandani, kuondosha bandarini na kuisambaza mbolea hadi kwa wakulima ambapo kumewafanya baadhi ya wafanyabiashara kupanga na kupandisha bei kiholela/watakavyo kwa maslahi binafsi na baadaye kusingizia UVIKO -19 na Vita huku tukiwaumiza wakulima wetu nchini.
Waraka wa mwisho wa bei elekezi ulitolewa Novemba, 2020 ambapo ilipofika Julai 2021 Waziri wa Kilimo wa kipindi hicho alifuta bei elekezi na kuruhusu wafanyabiashara waingize na kusambaza mbolea nchini bila kufuata bei elekezi na mfumo wa zabuni wa BPS. . Hata hivyo ilipofika Machi 2022 ulitolewa waraka mwingine na Wizara ya Kilimo ingawa pamoja na kuwepo bei elekezi hizo hazifuatwi na Serikali haisimamii kikamilifu kuzuia hali hiyo. Kitendo cha Serikali kufuta na kushindwa kusimamia bei elekezi ya mbolea ni kuvunja kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya mbolea ya mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea za mwaka 2011 zilizopitiwa upya mwaka 2017.
Hivyo kinachoendelea kwenye soko la mbolea ni ukiukwaji wa bei elekezi za mbolea kwani mara tu baada ya kuacha usimamizi wa bei elekezi, bei zilifumka kama mara mbili ya bei elekezi zilizokuwepo na hazijawahi kushuka tena. Wakati Serikali inaanza kusimamia bei elekezi na mfumo wa BPS bei za mbolea zilizokuwepo zilipungua kutoka wastani wa shilingi 100,000 hadi shilingi 40,000 kwa mfuko wa kilo 50 msimu wa kilimo 2017/2018.
Katika kikao alichofanya na wafanyabiashara wa mbolea mwezi Machi, 2022 Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amekiri mwenyewe kwamba wafanyabiashara wamekuwa wakipandisha bei holela kwa sababu Wizara kupitia TFRA iliacha kusimamia bei elekezi za mbolea (Taarifa hii ilichapishwa Machi 15, 2022 kwenye YouTube channel ya Wizara ya Kilimo https://youtu.be/jqhud_PYR-o )
Mheshimiwa Spika, Tumeuliza maswali kwenye Wizara husika ambayo yamekosa majibu, tuambiwe kuna maslahi gani ya umma yaliyotokana na kusitishwa bei elekezi? Kwa lugha nyingine, wakulima wamenufaika nini na kusitisha bei elekezi za mbolea? baada ya kufuta BPS na bei elekezi, bei ya mbolea imeshuka? Kinachodhihirika wazi baada ya kufuta BPS na bei elekezi bei za mbolea zilianza kuongezeka kwa kasi kubwa na hii ilikuwa kabla ya vita vya Urusi na Ukraine havijaanza.
(iv) Nchi jirani na zingine zinatumia bandari yetu ya Dar es Salaam kama Malawi, Zambia, DRC, Burundi na Rwanda lakini bei za mbolea ziko chini ikilinganishwa na sisi wakati tunanunua sehemu moja kwenye soko la dunia.
Maelezo ya kwamba bei katika nchi hizo ni ndogo kwa sababu zina ruzuku yanatiliwa mashaka kwa kuwa kabla ya kufuta BPS na bei elekezi hapa nchini kwetu bei ilionekana kuwa chini kuliko hizo nchi jirani na ndiyo maana kipindi hicho kulikuwa na presha kubwa ya utoroshaji wa mbolea kutoka nchini kwenda nchi jirani. upo ushahidi kutoka kwa wakuu wa Wilaya zinazopakana na nchi hizo kuonesha kwamba mbolea za Tanzania zilikuwa zikikamatwa wakati zikitoroshwa kwenda nchi hizo kwa vile bei ya mbolea za Tanzania ilikuwa ndogo kuliko bei katika nchi hizo mfano ni Taarifa ya TBC saa mbili usiku Januari 25, 2018 zilizochapishwa kwenye YouTube ya Global TV .
Usimamizi dhaifu unathibitishwa pia na hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Kilimo kwenye ibara ya 89 ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ilipokwenda kufanya ukaguzi iliibua mambo mazito ikiwemo kuuzwa kwa mbolea zisizosajiliwa aina 9, mbolea kuuzwa bila vibali, kuuzwa mbolea zilizofunguliwa na uwepo wa mbolea zenye uzani mdogo ikilighanishwa na vipimo.
(v) Utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi, hakuna mkazo wa kutumia mbolea za asili kama Samadi na Mboji zitokanazo na vinyesi vya mifugo na mabaki ya mazao mashambani. Mifugo yetu inazalisha matani kwa tani ya samadi kila siku lakini aina hii ya mbolea haitumiki kikamilifu na tuko bize kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi. Katika hotuba ya Waziri sijaona mkazo, mkakati wala bajeti katika tasnia hiyo ambapo mifugo yetu ndio kiwanda cha malighafi na uzalishaji unafanyika kila siku, mbolea inapatikana kiurahisi na kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema ya Serikali ya kutenga ruzuku ya mbolea kwa wakulima kiasi cha Shilingi Bilioni 150 lakini kwa vile mfumo wa ruzuku huko nyuma ulisitishwa kutokana na kugubikwa na rushwa, upendeleo na taarifa za kughushi (malipo hewa ya mbolea), Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa changamoto zilizosababisha mfumo wa ruzuku kusitishwa zimeshughulikiwa kabla ya kuanza utaratibu mpya wa utoaji wa ruzuku ili kuhakikisha kuwa ruzuku itakayotolewa na Serikali itumike kulipia ‘bei halisi’ ya mbolea na kuleta unafuu mkubwa wa bei kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Spika, hiyo fedha ya ruzuku iliyotolewa na Serikali kiasi cha Shilingi Bilioni 150 kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa bei ya sasa itaweza kuingiza tani 64,000 tu ambayo itatosheleza 25% ya mahitaji ya mbolea aina DAP na UREA ambayo ni tani 250,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, ruzuku pekee haiwezi kupunguza bei za mbolea nchini na pengine inaweza kupanda zaidi na wananchi kukosa unafuu wowote hivyo ni lazima Serikali ipitie upya mfumo wa uagizaji na usambazaji wa mbolea nchini ili kurekebisha kasoro zote zinazosababisha bei ya mbolea kupanda kila uchao. Mfumo wa BPS na bei elekezi ambao umefutwa kinyume cha sheria urejeshwe. Aidha ni muhimu kuweka mikakati thabiti ya kuongeza kasi ya uzalishaji katika viwanda vya mbolea nchini, pia kuweka mkazo katika uzalishaji na usambazaji wa mbolea za asili.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ushauri mwingi umekuwa ukitolewa kuhusu mwenendo wa bei za mbolea nchini lakini Serikali imekuwa na kigugumizi kusimamia na kutekeleza ushauri huo nakuomba uridhie kuundwe kwa Tume huru ya Bunge ili kuchunguza mambo yote kwa kina yanayosababisha kupanda kwa bei za mbolea nchini na Bunge lako Tukufu kutoa maelekezo kwa Serikali hatua za kuchukua.
Naomba kuwasilisha,
Luhaga Joelson Mpina (Mb)
Mbunge wa Jimbo la Kisesa
Luhaga Joelson Mpina (Mb)
Mbunge wa Jimbo la Kisesa