Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,524
- 1,173
MBUNGE MAVUNDE AZINDUA SHULE YA SEKONDARI MKOYO-HOMBOLO JIJINI DODOMA
-Ni Shule iliyojengwa na Mbunge Mavunde na Serikali
-Shule yapewa Jina la Anthony Mavunde
-Watoto wanusuriwa kutembea kilomita 15 kufuata Shule
-Serikali ya Rais Samia yapongezwa kwa usikivu
đź“ŤHombolo,Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde leo amefungua Shule ya Sekondari Anthony Mavunde iliyojengwa katika Mtaa wa Mkoyo-Hombolo Jijini Dodoma.
Shule hiyo imejengwa na Mbunge Mavunde kwa ushirikiano na Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji Dodoma ambapo Mbunge Mavunde alianzisha ujenzi huo kwa madarasa ya awali na kuahidi kwamba serikali sikivu chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan itasikia hitaji hivyo kuwaunga mkono ili kuwanusuru watoto kutembea kilomita 15 kufuata Shule Sekondari ya Hombolo Bwawani.
“Leo ninajisikia furaha ile ndoto yetu ya kuwapunguzia mwendo wanafunzi wa sekondari kutembea kilomita 15 hatimaye tumeitimiza.
Watoto wengi wa kike walishindwa kumaliza masomo yao kwa kupata ujauzito kutokana na vishawishi mbalimbali kwa umbali waliokuwa wanatembea.
Nilikuja hapa pakiwa pori,tukachimba msingi pamoja na kuanza ujenzi,naishukuru serikali chini ya Rais Dkt. Samia kupitia Halmashauri ya Jiji kutuunga mkono kwa kuongeza madarasa mawili na pia tunatarajia kujenga madarasa mawili mengine.
Nitasaidia kuingiza umeme shuleni pamoja na kuwaletea kompyuta na photocopier,nitachangia malipo ya walimu wanaojitolea na nitawanunulia pikipiki mbili (2) mzitumie kama kitega uchumi cha kukidhi baadhi ya mahitaji”Alisema Mavunde
Diwani wa Kata ya Hombolo Mh. Assedi Ndajilo amemshukuru Mbunge Mavunde kwa uanzishaji wa ujenzi wa Shule hiyo na kuwataka wazazi kuhakikisha wanawasimamia vizuri wanafunzi ili shule ilete matokeo tarajiwa.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe amesema Jiji la Dodoma litaendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Mbunge Mavunde na kuahidi upatikanaji wa maabara shuleni hapo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya Dodoma Cde Charles Mamba amesema ujenzi wa Shule hiyo ya Sekondari ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya kusogeza huduma kwa wananchi.