Ni hivi karibuni tu dunia imetoka kuadhimisha siku ya Tiba Asilia, ambapo mchango wa matibabu haya ya jadi kwa sasa umekuwa ukisaidia sana katika sekta ya afya. Kwa karne nyingi, maarifa ya kimapokeo kuhusiana na matibabu ya jadi yamekuwa nyenzo muhimu kwa afya katika jamii mbalimbali, na yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya huduma ya afya katika maeneo mengi.
Kwa kuwa nchi nyingi zinatambua kuwa tiba asilia ni chanzo muhimu cha huduma ya afya na kuchukua hatua za kuunganisha matibabu yake katika mifumo yao ya kitaifa, hivyo dawa za jadi kwa sasa zimekuwa jambo la kimataifa, ambapo mahitaji yake yanaongezeka kila siku.
China ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwenye mbinu za Matibabu ya Jadi ya Kichina (TCM) na tiba mbadala katika kupambana na magonjwa mbalimbali. Matibabu haya ambayo ni mbinu kamili ya kutibu matatizo ya afya ya akili na kimwili ya mtu, yalianzia miaka elfu tatu iliyopita wakati wa enzi ya Shang, japokuwa kwa sasa kimsingi matibabu yake yamebadilika kidogo tangu wakati huo, na hii ni kutokana na kuboreshwa baada ya kufanya tafiti mbalimbali.
Mbali na kwamba China inaendelea kutafiti matibabu na dawa zake za asili, hata hivyo bado haijasita kufanya uchunguzi zaidi wa aina mpya za dawa. Kwa mujibu wa Sensa ya Nne kuhusu Matibabu ya jadi ya Kichina, aina za dawa za jadi za Kichina zilizothibitishwa zimefikia 18,817. Aina hizi za dawa zinajumuisha 3,151 ambazo ni za kipekee nchini China, na kuwa mali yenye thamani katika hazina ya dawa na tiba za jadi za Kichina. Mbali na hayo, kuna aina nyingine 464 za dawa za jadi za Kichina ambazo zimeorodheshwa kama aina za dawa zinazohitaji kuhifadhiwa.
Hatua hii imeonesha nia ya China katika kulinda bioanuai na rasilimali za dawa za jadi za Kichina.
Jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa, Sensa ya Nne ya Kitaifa kuhusu Matibabu ya Jadi ya Kichina vilevile imegundua spishi mpya 196, ambapo kati ya hizi karibu spishi 100 zinaweza kutumiwa kama dawa.
Ugunduzi huu sio tu unaimarisha aina za dawa za jadi za Kichina, bali pia umeweka mustakabali mkubwa zaidi kwa maendeleo ya tiba na dawa za Kichina na kufufua hatua kwa hatua bioanuai ya dawa za jadi nchini China.
Kwa mamilioni ya watu wa China, iwe wanaishi mijini ama maeneo ya mbali na vijijini, matibabu ya jadi yanaendelea kuwa chaguo lao kubwa katika kutunza afya zao na ustawi wa maisha yao.
Matibabu haya yanawapatia Wachina huduma inayoaminika na kukubalika.
Hadi kufikia sasa mataifa 170 kati ya 194 Wanachama wa WHO tayari yameripoti kutambua na kutumia dawa za mitishamba, akyupancha, yoga, tiba asilia na aina nyinginezo za dawa za kienyeji.
Kazi ya WHO kuhusu tiba asilia ni kushughulikia na kujibu maombi ya nchi husika ambayo yana ushahidi na data zinazofafanua sera, matibabu, viwango vya dawa na kanuni za kimataifa ili kuhakikisha usalama, ubora na ufikiaji sawa.
Azimio la Astana la 2018 kuhusu huduma ya afya ya msingi linatambua haja ya kujumuisha maarifa ya matibabu ya jadi na teknolojia katika utoaji wa huduma ya afya ya msingi ili kuweza kufikia huduma ya afya kwa wote.
Wakati tiba za asili zikionekana kuweza kuondoa pengo la upatikanaji wa huduma za afya hasa katika nchi ambazo zina mifumo dhaifu ya afya, bado zinakuwa na thamani tu pale zitakapotumika kwa usahihi, ufanisi na zaidi ya yote usalama wake unapaswa kuzingatia ushahidi wa kisayansi wa zama za sasa.
Kwa Afrika tunafahamu kuwa tiba za asili zimeanza tangu enzi na dahari kama alivyo binadamu mwenyewe, ambapo watu katika nchi na tamaduni mbali mbali wametumia waganga wa kienyeji, tiba za asili na maarifa ya kale juu ya dawa hizi kukidhi mahitaji yao ya kiafya na ustawi wa maisha yao.
Kama WHO inavyosisitiza kila mara umuhimu wa kuzifanyia utafiti na kusajili dawa hizi za asili, lakini kwenye baadhi ya nchi waganga wa tiba asilia wanaonekana kutojali suala hili.
Ili kufanya matibabu haya yaweze kuwa mchango kwa nchi ambazo bado mifumo ya afya inasuasua ni vyema zikasajiliwa na baadaye kufanyiwa utafiti wa kina na mamlaka husikana hatimaye kuweza kuleta manufaa kwa afya ya watu.