Siku hizi, wimbi la kuacha kutumia sarafu ya dola ya kimarekani “dedollarization” limeibuka kila pembe ya dunia. Kutoka India, Brazil hadi China na Russia, kulingana na takwimu zisizokamilika, hivi sasa kuna zaidi ya nchi 60 ambazo zinachukua hatua za kuacha kutumia dola kwa njia mbalimbali. Tovuti ya Business Insider ya Marekani ilisema, "utawala wa dola ya kimarekani katika biashara ya kimataifa unakabiliwa na changamoto kubwa." Katika miongo kadhaa iliyopita, dola ya kimarekani imekuwa na nguvu kubwa kabisa katika biashara ya kimataifa na hifadhi za fedha za kigeni, lakini kwa nini sasa nchi nyingi zinatafuta njia mbadala za dola?
Kwa upande mmoja, tangu mwaka jana, Marekani imeongeza viwango vya riba mara kadhaa ili kushughulikia mfumuko wake mkubwa wa bei ndani ya nchi, hatua ambazo zimesababisha kushuka sana kwa thamani za sarafu nyingine, na nchi nyingi zinazoendelea hazina budi kukabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei. Afrika, eneo lililoathiriwa zaidi na hatua hizo za Marekani, ilishuhudia mfumuko wa bei wa wastani wa 13.5% mwaka 2022, kiwango ambacho ni cha juu zaidi katika muongo mmoja. Kwa hiyo, nchi nyingi zaidi zinajaribu kujiokoa, ikiwa ni pamoja na kufanya fedha za kigeni zilizohifadhi kuwa za aina mbalimbali na kutumia fedha zisizo za dola ya kimarekani katika biashara ya kimataifa. Hivi karibuni, kufilisika kwa benki za Marekani ikiwemo benki ya Silicon Valley, kumesababisha hofu ya imani za watu juu ya utaratibu wa kulipa biashara kwa kutumia dola ya kimarekani, na mwelekeo wa kuacha kutumia dola umezidi kukuwa kwa kasi.
Kwa upande mwingine, kuacha kutumia dola ya kimataifa inahusiana kwa karibu na matumizi ya muda mrefu ya dola kama silaha za kisiasa na kiuchumi za Marekani ili kutishia au kuziwekea vikwazo nchi nyingine. Hasa baada ya kuzuka kwa mgogoro kati ya Russia na Ukraine, uchumi wa Russia uliwekewa vikwazo vikali na Marekani na nchi nyingine za Ulaya, na watu wamegundua kuwa hifadhi zao za dola ziko hatarini kuporwa kihalali au kinyume cha sheria wakati wowote, hivyo wamezidisha makubaliano yao ya kupunguza kutegemea dola.
Kama "mshirika muhimu wa kimkakati"wa Marekani, Wizara ya Mambo ya Nje ya India Aprili mosi ilitangaza kwamba India na Malaysia zimekubali kutumia Rupia ya India katika biashara zao. Maelezo rasmi ya India kuhusu hatua hiyo ni kwamba nchi hiyo inajaribu kuepusha biashara yake isiathiriwe na mgogoro wa siasa za kijiografia. Ni wazi kuwa kadiri dola inavyotumika kama silaha, ndivyo itakavyoachwa kwa kasi.
Wakati China ikiendelea kuhimiza maendeleo yenye ubora wa juu na kushikilia mageuzi na ufunguaji mlango na ushirikiano wa kunufaishana, katika wimbi la "kuacha dola" duniani, nchi nyingi zimeanza kutumia RMB, na kwamba hadhi ya sarafu ya China inazidi kuimarika kimataifa. Mwishoni mwa mwezi uliopita, kampuni ya nishati ya Total ya Ufaransa na kampuni ya mafuta ya China CNOOC zilifanya biashara ya gesi asilia iliyoyeyushwa kwa RMB, na kuifanya Ufaransa kuwa nchi ya kwanza ya Ulaya kutia saini makubaliano ya kibiashara yanayolipwa kwa RMB badala ya dola au Euro. Kulingana na ripoti, zaidi ya nchi 30, ikiwa ni pamoja na Brazil, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Russia, na Iran, zinageukia RMB katika biashara au uwekezaji wao.
Imani ya dola imeshuka kufuatia Marekani kutumia vibaya utawala wa dola duniani. Kulingana na takwimu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, hifadhi za dola za kimarekani duniani zimeshuka kutoka zaidi ya 70% ya mwaka 2000 hadi karibu 56% kwa sasa. Ingawa dunia bado haijaepukana na utawala wa dola, nchi zimeona na kutambua hatari, na cha muhimu zaidi kuwa mara tu mchakato wa "kuacha dola" unapoanza, hautaweza kutenguliwa, isipokuwa tu Marekani itakapoacha sera zake za umwamba, kutatua vizuri migogoro yake ndani ya nchi, na kuchangia nguvu chanya kwa uchumi wa dunia.
Swali ni kuwa hii inawezekana?!