Sokomoko
JF-Expert Member
- Mar 29, 2008
- 1,915
- 129
Maregesi ni Jacob Zuma wa CCM?
Jumaa Mgwadu
UKITAJA jina la Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa uzuri au ubaya, unagusa hisia za watu wengi. Unaibua hoja hata ambazo zilikuwa zimeanza kusinzia.
Sababu ni moja; kwamba unataja chama tawala ambacho kinaleta msisimko kila mara, iwe kwa mema ama kwa mabaya.
CCM, ambayo mmoja wa waasisi wake, Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba ikienda vibaya ataihama kwa sababu chama hicho si mama yake, inakabiliwa na changamoto kubwa kwa sasa pengine kuliko wakati mwingine wowote wa uhai wake wa miaka 31.
Pamoja na mitihani mingine mikubwa ambayo kimevuka, chama hicho sasa kina wakati mgumu ambao ni ule wa kuhakikisha kuwa kinazika sura na sera za makundi miongoni mwa viongozi na wanachama wake.
Pamoja na kwamba wakubwa katika chama hiki wanakataa kwamba hakuna makundi, lakini ukweli unabaki wazi kuwa makovu ya siasa za makundi ndani ya CCM ni makubwa na kwamba kama uongozi wa juu hautaamua kuyazika, hali ambayo imevikumba vyama tawala katika nchi jirani zetu, inaweza kuikuta CCM wakati wowote.
Na wala jambo hili halihitaji akili ya ziada sana, ni jambo la kutazama sera, mwendo na tabia za baadhi ya viongozi na wanachama ambao ndio wananchi wa kawaida.
Kusema kwamba CCM inajiambukiza yenyewe virusi vitakavyokuja kukimaliza, wala si dhambi. Ni sawa tu na kumwambia mtu fulani kuwa wewe unaumwa ukimwi, kama kweli anaumwa ugonjwa huo.
Makundi yaliyotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 yalikuwa makubwa, na makovu yake yangali makubwa pia.
Makovu haya hayajafutika kwa sababu viongozi wameamua kuwa yaendelee kuwepo kama alama mpya ya CCM.
Kwamba huyu alikuwa mwanamtandao na yule alikuwa mtu wa kundi tofauti na mtandao, ni alama mpya ambayo imekuwa ikiwatambulisha wanachama na makada wote wa CCM kwa sasa hivi, alama ambayo kwa hakika inaleta utengano mkubwa.
Ukimtazama Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, unaona kuwa wakati wote anahubiri kifo cha makundi hayo.
Anaonekana kama ana dhamira ya kweli ya kuzika tofauti za makundi ndani ya chama anachokiongoza, kwa sababu anajua madhara yake wakati unapofika.
Mtandao ambao wakati ule unamwingiza Kikwete madarakani ulikuwa na nguvu moja, wenyewe umesambaratika, lakini kusambaratika ambako ni kubaya zaidi, kwani imezaliwa mitandao mingine.
Ni kama mti ambao hauna faida unapokomaa na kuanguka, lakini huku mbegu zake zikiwa zimeshasambaa katika sehemu mbalimbali na kuanza kuota tena.
Niliwahi kusoma mahali fulani kwamba kunguru hawa tunaowaona sasa hivi jijini Dar es Salaam, waliombwa kama mbegu kutoka nchini India na serikali kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la nzige katika mashamba ya wakulima, hasa visiwani Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya themanini.
Serikali, wakati ule haikujua kama kunguru hawa baada ya kazi yao ya kupambana na nzige, wangezaliana na kuwa kero kubwa kwa kiwango hiki, huku wakiwa wametapakaa katika maeneo mengi. Serikali sasa hivi haiwahitaji kunguru hawa na imekuwa ikitoa fedha kuwaangamiza.
Hali hii ndiyo ambayo inaikabili CCM. Wakati wakubwa fulani wanaanzisha kunguru-mtandao kwa kazi ya kupambana na wenzao, hawakujua kuwa kunguru hao watakuja kuwa kero kubwa kwao baadaye, na kwamba kuwaondoa itawagharimu muda na pengine hata fedha nyingi.
Na nzige ambao walilengwa wakati ule wanafahamika. Walikuwa John Malecela, Fredrick Sumaye, Dk. Salim Ahmed Salim, Profesa Mark Mwandosya na Dk. Abdallah Kigoda pamoja na wapambe wao wote. Hawa ndio walikuwa wanahatarisha kukubalika kwa Kikwete katika harakati zake za kuwa madarakani.
Mmoja wa watu ambao wameathiriwa na wanamtandao kwa kiwango kikubwa ni Abiud Maregesi. Huyu alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM hadi Julai mwaka jana aliposimamishwa na Kamati Kuu ya chama hicho, akituhumiwa kuwa ameisababishia jumuiya hiyo hasara kubwa.
Maregesi wakati ule wa mchakato wa kutafuta mgombea wa CCM hakuwahi kuficha hisia zake, alitamka wazi kuwa alikuwa anamuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu, Sumaye katika harakati zake za kuwania urais.
Na kwa kweli wakati ule ilikuwa inakuhitaji kuwa jasiri na mtu mwenye msimamo kutangaza hadharani kumuunga mkono mgombea yeyote.
Nakumbuka wengine walioondoa woga walikuwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Mashishanga ambaye naye alisema alikuwa anamuunga mkono Sumaye, na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Kagera, Pius Ngeze, pamoja na mzee Peter Kisumo ambao walisema bayana kuwa walikuwa mashabiki wa Kikwete.
Baada ya kupatikana kwa mgombea, kila mwanachama wa CCM alitegemea kuwa makundi haya yangekufa moja kwa moja.
Kila mpenda mema kwa nchi hii alikuwa anaamini hotuba ya Kikwete ya kushukuru kuteuliwa kwake kuwa mgombea, ingetosha kuwa kaburi la makundi.
Bahati mbaya haikuwa hivyo, na itachukua muda mrefu kuwa hivyo. Watu ambao hawakuwa kambi ya Kikwete walianza kuandamwa waziwazi.
Uteuzi mbalimbali uliofanyika uliingiza timu kubwa ya mtandao katika nafasi mbalimbali, na katika CCM panga kubwa liliwafyeka wale wote waliompinga Kikwete.
Hawa ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Philip Mangula, naibu wake, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi na mzee Paul Sozigwa. Sekretarieti nzima ya CCM ilifumuliwa na kuwatupa nje wale wote ambao walikataa kuwa waumini wa timu ya mtandao. Kilichotokea kila mmoja anakifahamu.
Ni kutokana na fumua fumua hii, Maregesi naye alijikuta akiondolewa pamoja na wasaidizi wake katika Jumuiya ya Wazazi kwa tuhuma kwamba kulikuwa na matumizi mabaya ya fedha na madaraka.
Ni kutokana na fumua fumua hii pia, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake, Halima Mamuya naye akalazimika kuachia ngazi kupisha kasi ya wanamtandao ifanye kazi yake ingawa alikuwa na tuhuma za msingi na alishindwa kuzithibitisha.
Lakini nini kimefanya Maregesi aondolewe madarakani? Tuhuma zinazomkabili zina ukweli?
Yeye mwenyewe anakanusha kwa kiwango kikubwa. Analalamika na hataki kuamini kama kusimamishwa kwake uongozi kulifuata taratibu.
Ingawa hataki mahojiano kwa wakati huu, lakini makala hii imenasa nakala ya barua ambayo Maregesi alimwandikia Rais Kikwete akimlalamikia kwamba alikuwa hatendewi haki kwa kusimamishwa bila kuandikiwa barua, kupewa nafasi ya kujitetea au kuhojiwa kuhusu kile anacholalamikiwa.
Na pengine ni kuamini kwake kuwa amekaangwa kutokana na kutokuwa mwanamtandao, ndiyo maana kada huyo wa CCM alipata uamuzi wa kuandika barua nzito kwa mwenyekiti wake. Hataki kuwa kondoo wa sadaka, kwamba kama hukumu itatoka basi iwe hukumu ya kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichaguliwa kuiongoza jumuiya hii kwa kura nyingi tarehe 06. 03. 2004, tangu nilipochaguliwa hadi Juni 2007 ni mambo mengi nimeyafanya katika kutoa michango yangu binafsi kwa chama, jumuiya, wakereketwa, wanachama katika ngazi mbalimbali.
Nasikitika kusikia kwamba Katibu Mkuu wa chama anatamka wazi wazi kama nimeua mashule, ni jambo la kusononesha mno, anasema Maregesi katika barua hiyo.
Wakati mwingine akitumia msemo kuwa shukurani ya punda ni mateke, Maregesi anasema kuwa alipoingia madarakani aliikuta jumuiya hiyo haina samani katika ofisi yake ya makao makuu, lakini aliibadili kwa kununua samani hizo pamoja na kompyuta kutokana na fedha zake mwenyewe.
Kada huyo anasema aliwakuta wafanyakazi wakiwa hohehahe kutokana na mishahara duni ya sh 48,000 hadi 60,000 waliyokuwa wanalipwa kwa mwezi.
Aliamua kuwaongeza sh 20,000 na 30,000 kila mmoja kutoka mfukoni mwake ili kupambana na maisha hadi CCM ilipoongeza ruzuku kwa jumuiya.
Hakuishia hapo tu, makao makuu ya jumuiya hakukuwa na gari hata moja. Aliinunulia jumuiya hiyo magari mawili aina ya Mahindra Oktoba 2005, ambayo yanatumika hadi sasa, magari ambayo anasema pamoja na kuyanunua yeye kama kiongozi, hakuwahi kuyatumia na kwamba katika shughuli zote za chama amekuwa akitumia magari yake binafsi ikiwemo hata mikoani.
Haishii hapo, kada huyo wa CCM anasema kuwa mara kadhaa amekuwa akitoa fedha zake mfukoni kunusuru mambo yaliyokuwa yanaikabili jumuiya na hata chama chake wakati mwingine.
Anakumbusha kuwa aliwahi kulipa sh milioni 10 kwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutokana na uzembe wa kutopeleka michango wa aliyekuwa katibu kabla yeye hajaingia madarakani, sawa na kiasi kama hicho kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutokana na malimbikizo ya kodi katika Ofisi ya Makao Makuu ya Wazazi.
Shule ambazo anadaiwa kuziibia ndizo ambazo anasema amezisaidia sana kwa kuzipa michango ya fedha taslimu au vifaa mbalimbali.
Maregesi hataki kuficha mambo, anazitaja shule hizo kuwa ni pamoja na Kaole Bagamoyo, Tabata, Gongolamboto, Tegeta za Dar es Salaam, Masibwe ya Iringa, Isango ya mkoani Mara, Bungu mkoani Pwani, Muhuwesi ya mkoani Ruvuma na Maregesi ya wilayani Newala mkoani Mtwara.
Shule nyingine ambazo kada huyo anadai kuwa amezichangia kwa kiwango kikubwa ni zile za mkoani Mbeya ambazo ni Chunya, Igorasi, Chimala, Ibungila na Tunduma, pamoja na Shule ya Sekondari Shemsanga iliyoko Korogwe mkoani Tanga.
Mambo ambayo kada huyu ameorodhesha katika waraka wake kwa Kikwete ni mengi, lakini kwa kifupi anasema kuwa ametoa zaidi ya sh milioni 200 kutoka mfukoni mwake kwa ajili ya CCM, na nyingine kiasi kama hicho kusaidia miradi mbalimbali, zikiwemo shule hizo zinazodaiwa kuwa amezihujumu.
Maregesi anasema haiingii akilini mtu ambaye amechangia mamilioni kama hayo ya fedha afanye hujuma ya fedha ambazo zinadaiwa kufikia sh milioni 63.
Kama ni kutazama mema ya mtu, kwa hakika Maregesi alipaswa kuenziwa na pengine hata kupewa tuzo kutokana na mchango wake mkubwa kwa Jumuiya ya Wazazi ya CCM kuliko kiongozi mwingine.
Ni nadra kwa viongozi kufanya mambo makubwa kama ambavyo amefanya kada huyu, halafu waje kuhukumiwa tu kwa sababu hawakuwa upande wa kiongozi wa nchi wakati wa kampeni.
Katika sakata hilo, Maregesi anajifananisha na Jacob Zuma aliyekuwa Makamu wa Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.
Zuma ambaye sasa ni Rais wa chama tawala cha ANC, amefanyiwa mizengwe mingi na bado amekuwa akiandamwa na mambo ya ajabu nchini mwake Afrika Kusini.
Watu wasiomtaka wamekuwa hawalali usingizi, wakitaka afutike katika siasa za nchi hiyo. Hivi ndivyo CCM ya Kikwete na Katibu Mkuu Yussuf Makamba inavyotaka kumfanya Maregesi?
Lakini hapa ndipo umma unapotakiwa kufahamu kama kweli dhamira ya Rais Kikwete kuzika makundi katika chama chake ilikuwa inatoka moyoni mwake.
Kama jibu linaweza kuwa kweli, kwanini wale ambao hawakumuunga mkono wanakaangwa ndani ya chama? Hivi kama kila mwanachama wa CCM angekuwa anataka Kikwete awe rais, kulikuwa na haja gani kuwaomba makada wengine wajitokeze kugombea nafasi hiyo?
Ipo haja kwa sasa kuangalia maslahi ya chama badala ya kuendekeza chuki na makundi ambayo hayana faida kwa CCM na serikali yake.
Viongozi ambao wanatakiwa kuwaunganisha wanachama wakianza tabia ya kuwabagua, CCM inaweza ikajikuta katika wakati mgumu kwa kuzingatia kuwa akili za wanachama wa leo ni tofauti na wale wa miaka ya uhuru, ambapo kila mmoja alikuwa anaimba wimbo unaofanana na mwenzake; kidumu chama, zidumu fikra za mwenyekiti.
Mambo yaliyotokea bungeni Dodoma kwa baadhi ya wabunge wa CCM kutokubali kuburuzwa, ni ushahidi mkubwa kwamba wana CCM wenyewe sasa hivi wamebadilika. Hawana sababu ya kulindana, na kwamba baadhi yao wanaangalia maslahi ya umma kwanza, kuliko kuwatetea viongozi wao.
Hapa ndipo ninapomkumbuka Mwalimu Nyerere, kwa hakika angekuwa hai leo hii angekihama chama hiki, angetafuta chama mbadala ambacho hakina makundi, hakina visasi na chenye misingi ya kukosoana kwa mambo ya kweli kabisa.
Leo hii kuna habari ambazo hazina shaka kwamba juhudi ambazo Maregesi alifanya kuhakikisha shule za sekondari za Jumuiya ya Wazazi zinakuwa miongoni mwa shule kumi bora, zinataka kuzikwa rasmi.
Sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM, inapeleka pendekezo katika kikao cha Halmashauri Kuu kwamba shule hizo zirejeshwe serikalini. Huu ni usaliti kwa wanachama wa CCM hasa wale wa Jumuiya ya Wazazi, kwa sababu shule hizo ndio mradi pekee wa jumuiya hiyo.
Ni shule zaidi ya 100 zilizosambaa katika mikoa yote nchini zenye walimu na wafanyakazi wengi, zinazoingizia chama mamilioni ya shilingi. Wakubwa wanadai kuwa shule hizi zimekuwa na matokeo mabaya. Jambo hili halina ukweli hata kidogo! Ukweli ni kwamba wakubwa katika CCM wanataka kuzika mafanikio yaliyopatikana ili kuhalalisha uchaguzi mkuu wa jumuiya hiyo mwaka huu kwa wanamtandao.
Lakini swali la msingi hapa ni kwamba, nini hatma ya wanachama wake? Nini hatma ya walimu na wafanyakazi wengine? CCM imetenga kiasi gani cha fedha kulipa mafao ya wafanyakazi hawa, hasa ikizingatiwa wengine hawatapenda kufanya kazi chini ya mwajiri mpya?
Hii ndiyo CCM mpya!