Mamlaka zimulike yanayoendelea Manispaa ya Bukoba kuhusu mchakato wa ujenzi wa Stendi Mpya

Nyakijooga

JF-Expert Member
Dec 9, 2018
264
468
Licha ya kuwepo kwa mikakati mingi juu ya ujenzi wa Stendi Mpya ndani ya Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera lakini Stendi hiyo imekuwa sawa na kitendawili ambacho kimekosa kutekuguliwa kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Kwa kumbukumbu tu ni kuwa Aprili 2023 zilitoka taarifa kuhusu Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kumkabidhi Mkandarasi 'Kajuna Investment' eneo la mradi uliokuwa umesimama kwa muda mrefu eneo la Kyakairabwa.

Mwaka 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa Tsh. Bilioni moja za awali kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo wa awali, taarifa zilizokuwepo ni kwamba ilikuwa ikihitajika Tsh. Bilioni 18 ili kukamilisha Stendi hiyo eneo la Kyakairabwa, Kata ya Nyanga Manispaa ya Bukoba.

Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Steven Byabato alienda sehemu ya Mradi huo Aprili 2023 na kufanya makabidhiano na mkandarasi kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa mradi huo mbele ya Wananchi, ambapo alisema uendelezaji wa kituo hicho utasaidia kuepukana na adha ambayo wasafiri wamekuwa wakiipata.

Alisema fedha za ujenzi wa kituo hicho cha mabasi Kyakairabwa unatarajia kugharimu kiasi cha Sh. Bilioni 18 na fedha hizo zitakuja kulingana na awamu za ujenzi hadi kukamilika kwake.

Sanjari na kauli hiyo iliyoonesha Kitendawali hicho kuteguliwa kuwa matumaini zaidi kwa wakazi wa Mkoa huo yaliongezeka hasa baada ya kuhusihanisha na kauli ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ambaye Machi 2022 alinukuliwa akisema Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa stendi ya kisasa katika Manispaa ya Bukoba kwa kupeleka awamu ya kwanza Tsh. Bilioni moja kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 na kuelekeza Manispaa ya Bukoba nayo kutenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza mradi huo muhimu.

Licha ya matumaini hayo lakini mradi huo ulisimama bila kuendelezwa kama ilivyotarajiwa badala yake Mkandarasi aliishia kupeleka vifaa kwenye eneo la mradi na baadaye kuvitoa huku baada ya hapo ukimya kuhusu utekelezwaji wa mradi huo ukatawala.

Kufuatia ukimya huo, Agosti 2023 ilishuhudiwa Baraza la Madiwani kukutana kwa dharura na kutoa taarifa kuhusu ya kuridhia kubadilisha matumizi ya kiasi cha Tsh. Sh Bilioni 1 kuelekezwa katika kituo cha mabasi na magari madogo' kilichokuwa kikitumika kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita ambacho kipo katikati ya Mji Mtaa wa Uhuru kiwanja chenye hati Na.71712 kiwanja Na.164 kitalu (I )Kata Bilele ina ukubwa wa Mita za mraba (6620).

Uamuzi huo ulipitishwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa Bukoba ikiwa ni miezi minne baada ya Mbunge kufanya makabidhiano na Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi Stendi Kyakairabwa.

Kutokana na uamuzi huo Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Hamid Njovu, akieleza sababu ya kubadilisha matumizi hayo ni kuwa stendi hiyo ilijengwa wakati wa Mkoloni na ina umri zaidi ya miaka 60 lakini haijawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa hali inayoisababishia Halmashauri gharama kubwa za usimamizi na maboresho ya mara kwa mara na kuwa imekuwa kero kwa watumiaji kwa sababu ya uchakavu wake.

Alinukuliwa akisema kuwa Mkuu wa Mkoa huo akiwa ameambatana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa , Mstahiki Meya pamoja na wataalam wa halmashauri ya Manispaa ya Bukoba walitembelea stendi hiyo na kubaini changamoto kubwa.

“Ujumbe wa Mkuu wa Mkoa ulielekeza kwamba badala ya kutumia bilioni 1 kuanza ujenzi wa stendi mpya ya Kyakailabwa ambapo tayari anatafutwa mkandarasi mshauri badala yake itumike kufanya marekebisho makubwa ya stendi inayotumika sasa wakati taratibu za ujenzi wa stendi kubwa unaendelea" amesema Mkurugenzi.

Aidha, Mkurugenzi huyo alinukuliwa akisema "Baada ya kupata hiyo Bilioni moja tukasema tujenge stendi ya Kyakairabwa, wakati tukiendelea kujenga tulikuwa kwenye mchakato wa kupata Bilioni 10 na kuendelea chini ya Benki ya Dunia (World Benk) ambao ni TACTIC, (Tanzania Cities Transforming, Infrastructure, Competitive Project) wakati tunaendelea tumeshampa Mkandarasi na sisi tukawa kati ya Halmashauri tatu Manspaa zilizopata miradi hiyo ya, na wao wanachotaka wakute kitu ambacho akijaendelezwa sehemu yoyote.

Hata hivyo itakumbukuwa June 15, 2023 Serikali kupitia Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kabla ya kugawanywa, Atupele Mwakibete (MB) akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (NGO's), Neema Rugangira lililohoji lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi mpya ya Bukoba Mkoani Kagera.

Naibu Waziri huyo alijibu kwa kusema "Suala la ujenzi wa stendi katika Mkoa wa Kagera tutawasiliana na wenzetu TAMISEMI Bukoba ambao wanasimamia Jambo hili ambao naamini kwenye bajeti yao mwaka huu uenda wamepanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa stendi hii."

Kufuatia kauli hizo zenye mkindhano baadhi ya wananchi wameonesha kutokulizishwa na michakato inayoendelea wakionesha wasiwasi wao juu ya ujenzi wa stendi mpya iliyopangwa kujengwa eneo la Kyakairabwa.

Nyuma ya Pazia Kuna Nini Kinachotajwa Kukwamisha Mradi wa ujenzi wa Stendi mpya Kyakairabwa?

Ikumbukwe michakato ya ujenzi wa stendi mpya ya Manispaa ya Bukoba ulianza Mwaka 2010, lakini ilitajwa kuwepo kwa mvutano baina ya vigogo waliokuwa na ushawishi kwenye Manispaa hiyo, ambapo baadhi ya vigogo hao ni aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dr. Anatory Amani na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Balozi, Hamis Swedi Kagasheki.

Mvutano huo uliodaiwa kughubikwa na maslahi binafsi umekuwa ukitajwa kuwa ulipelekea dhamira ya ujenzi wa stendi mpya kuota mbawa huku ikitajwa kuzaa makundi kwa watendaji mbalimbali katika Idara tofauti ndani ya Manispaa hiyo.

Mwaka 2014 taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh ilitupia jicho na kubaini uwepo wa mgogoro ndani ya Manispaa hiyo ambao ulipelekea Meya Anatory Amani kujiuzulu huku Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Khamis Kaputa na wakuu wa idara tatu ambao ni Mhandisi Nimzihilwa, Ofisa Ugavi Baraka Marwa na Mweka Hazina Ulomi wakivuliwa uongozi baada ya kutajwa kwenye ripoti ya CAG iliyosomwa Januari 17,2014.

Ripoti hiyo ilitokana na maagizo ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye aliagiza ufanyike ukaguzi kwenye masuala mbalimbali ndani ya Manispaa hiyo ikiwemo suala la ujenzi stendi mpya.

Hata hivyo katika uchunguzi unaonesha bado kuna migogoro ya baridi (ndani kwa ndani) inayoibua mivutano na kukwamisha uwajibikaji hasa kwenye miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa stendi mpya. Mdau anatueleza kuwa migogoro hiyo imekuwa ikitengeneza mipasuko ambayo ni kikwazo cha ushirikiano.

Kumekuwepo na itikadi za kusiasa pamoja na ufuasi ambao unatokana na mvutano wa vigogo mbalimbali ambao wamewai kushika nyadhifa ndani ya Serikali pamoja ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) sambamba na baadhi Wafanyabiashara wenyewe

Pia kuna maslahi binafsi (personal interest) kwa baadhi ya watu walioko kwenye mamlaka za kimaamuzi.

Chanzo kutoka Manispaa ya Bukoba kimesema "Kinachokwamisha miradi mingi ya kimkakati hapa Manispaa yetu ya Bukoba ni maslahi binafsi ya baadhi ya watu. Kuna Mtu akiona hilo jambo linaloenda kutekelezwa anufaiki nalo moja kwa moja bahati nzuri au mbaya akaona anao uwezo wa kutengeza mazingira jambo hilo likakwama basi anafanya hivyo, ndivyo ilivyo katika stendi yetu.

"Pia wapo wanaopiga debe mradi upelekwe maeneo ya Kibeta ambapo huko napo kuna watu watanufaika.

Itakumbukuwa Manispaa ya Bukoba ndio kitovu cha Mkoa wa Kagera ambao una jumla ya Wilaya nane ambazo ni Bukoba Mjini, Bukoba Vijijini, Missenyi, Muleba, Biharamlo, Ngara, Karagwe na Kyerwa.

Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022 Mkoa huo una jumla ya watu 2,989,299 nyuma ya Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Morogoro na Dodoma.

Taarifa ya Mamlaka ya Takwimu nchini (NBS) kwa Mwaka 2022, Kagera ndio Mkoa wenye umaskini zaidi ikilinganishwa na mikoa mingine (GDP), katika takwimu hizo za kila mwaka Mkoa huo kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo umekuwa ukitajwa kuwa kati ya mikoa mitano ya mwisho.

Wito unatolewa kwa mamlaka za Serikali kupitia vyombo mbalimbali, ikiwemo mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama kufanya uchunguzi wa fedha mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa stendi mpya hususani Bilioni moja iliyotolewa na Rais Samia.
 
Back
Top Bottom