Malalamiko yeyote dhidi ya kiongozi yeyote yafanyiwe uchunguzi kisha yawekwe wazi

Jul 6, 2024
90
64
MALALAMIKO YEYOTE DHIDI YA KIONGOZI YEYOTE YAFANYIWE UCHUNGUZI KISHA YAWEKWE WAZI

Nilisikika huko ndotoni nikiwa nakoroma kama simba nikaanza:

Nakumbuka Aprili 2019, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati huo akiwa Makamu wa Rais, akiwa katika kongamano la kumuenzi hayati Abeid Amani Karume alisema:

“Watu wanaosema ukweli mnawasemaje? Aambiwe nini naye, kimbelembele?”Mwisho wa kunukuu.

Nabii IPM wa Kanisa lililopo Mbezi Beach Mbuyuni, nakumbuka tarehe 07/12/2024 alisema:

“Mimi nitaendelea kuusema ukweli tu, hata kama ni ukweli mchungu. Hata kama watu hawaupendi, nitaendelea kuuzungumza, kwa sababu watu wanatamani kusikia maneno ya kweli na wala siyo kuwalaghai watu. Hakuna kitu mwanaadamu hapendi kama kumdanganya mtu mzima. Tuwaambie ukweli.”Mwisho wa kunukuu.

Tukisoma Mwongozo wa CCM 1981 uk. 102, ibara 107, inatueleza:

“Uhalali wa uongozi wa CCM na kukubalika na kuaminiwa kwake kwa umma kutategemea vitendo vya kimapinduzi vya uaminifu na ukweli kwa umma vya wanachama na hasa viongozi wa CCM katika harakati za kila siku.”Mwongozo wa CCM 1981 uk. 102, ibara 107.

Chama kiwe ndani ya umma na kiwe mwakilishi wa kweli na halali wa matumaini yao ya haki.Mwisho wa kunukuu.

Ndani ya nchi yetu, uwe mwananchi, uwe mwanasiasa, uwe mtumishi wa serikali, uwe sekta binafsi, uwe nani, unapaswa kuonyesha unyenyekevu wa kufuata na kuitii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 toleo 2005 na sheria zote zilizomo ndani ya Jamhuri huku ukiongozwa na Ibara 26(1)(2), Ibara 9(a)(b)(f)(h) ya Katiba ya Jamhuri.

Kwa mujibu wa Ibara 26(2), kila mtu aliye na utimamu wa akili anapaswa kuihifadhi, kuilinda, na kuitetea Katiba na sheria za Jamhuri.

Ndani ya sheria za Jamhuri, kuna kanuni na miiko ya uongozi. Kuna sheria zinazoelekeza kuchukua hatua dhidi ya uvunjifu wa mifumo. Inakuwaje watu wanalalamika kila kukicha huku viongozi na baadhi ya michawa ya viongozi ikiona malalamiko bila ya kuchukua hatua? Wanapokataa kuchukua hatua huo uhalali wa kuendelea kukalia vyeo walivyoviapia kuvitumia kulinda sheria za nchi unapatikana wapi? Wanatekelezaje takwa la Katiba ya Jamhuri Ibara ya 8(1)(a)(b)(c)(d)?

Wanaelewa nini kuhusu Ilani ya CCM 2020 uk. 01, ibara 04? Imani zetu na viapo vyetu kwa Mwenyezi Mungu viko wapi? Tukiambiwa sisi ni walaghai tunaotumia hila kuongoza, tutakuwa tumeambiwa uongo? Yako wapi mapenzi ya kweli ya kusimamia kauli na maandiko ya kimfumo?

Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa Makamu wa Rais, nakumbuka Aprili 2019 alisema:

“Sasa ndugu zangu, tabia hizi nazisema ili tujitathmini na kila mtu ajitathmini mwenyewe. Hatuwezi kufanya tathmini ya pamoja hapa kwa sababu kila mtu na roho yake, kila mtu na akili yake, kila mtu anavyofikiri. Kwa hiyo kila mtu ajitathmini mwenyewe. Ukishajirekebisha wewe, na kila mtu akajirekebisha, wote tutakwenda vizuri pamoja.”Mwisho wa kunukuu.

Tuishi kwa kadri tulivyoapa na kuahidi kwa Mwenyezi Mungu kuwa watu wa kutenda haki, tusiobebana kwenye maovu. Huu ndiyo utu uliojaa heshima, usiokuwa na utapeli wa kuwaza kutafuna fedha za mafukara kwa msaada wa sauti zinazopazwa na michawa itumiayo tumbo kufikiri.

Watu wanapolalamika lazima jitihada za kuchukua hatua za kisheria za kujibu malalamiko ziwepo, tena kwa uwazi usiobeba kupendeleana na mihali kwa kuangalia hali za watu. Haiwezekani tutangaze kuwa chama chetu ni chama kinachojali wanyonge kisha hatuwasikilizi wanyonge wenyewe malalamiko yao. Ni matapeli na majizi pekee ndiyo hupenda kujionyesha kuwa yana wema mbele za watu huku nyuma ya pazia yakiwa hayana utu na ma mbwa mwitu wenye njaa wasioacha kula hata mizoga inayonuka kuoza.

Nchi hii ni yetu sote. Tumetumia sana hekima kusema ila minyang’au haielewi. Inatumia udhaifu wa mtu mweusi kumnyonya kama vile alivyofanya mkoloni, kisha minyang’au inalindana. Mfano tu:

  1. Ofisi ya CCM iliuzwa kinyume na utaratibu. Sisi tulikuwa tumechanga ili ofisi ijengwe, tumeambiwa nini kupoza hasira zetu?
  2. Viongozi wasiposoma mapato na matumizi tafsiri yake wamehalalishwa kula fedha za mafukara bila ya kuhojiwa huku kibaka wa kuku mtaani akifuatiliwa na kukamatwa na watu walioapa kutokuwa wabaguzi wala wapendeleaji.
Tunaheshimishaje viapo na ahadi zetu kwa jamii? Typewriter za CCM zimeuzwa; ni hatua gani zimechukuliwa? Watu wamevuruga chaguzi na kukiuka kanuni; ni hatua gani zimechukuliwa? Mtu katoa taarifa za uongo kupata cheo ila kwa vile anasifika kwa utoaji wa rushwa bado yuko madarakani.

Tujiulize: hawa mafukara waliojaa jela kwa mashauri ambayo wangeonywa ni akina nani? Sio Watanzania? Watumishi wa umma wasomi wanaochukuliwa hatua kila kukicha ni akina nani? Sio Watanzania? Tulipoapa kuihifadhi, kuilinda, na kuitetea Katiba na sheria za Jamhuri zinazokataza ubaguzi na upendeleo, tuliapa ili iweje? Uadilifu wetu wa utumishi kwa umma unasomekaje mbele ya umma?

Tunapojionyesha kama tuna imani ya Mwenyezi Mungu huku tukiwa tumejawa viburi na majivuno ya matumizi mabaya ya vyeo, jamii inatutizamaje? Lazima tuambizane ukweli.

Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa Makamu wa Rais, nakumbuka Aprili 2019 alisema:

“Nimefundishwa na Karume ninaloliona silo niseme, na nitasema.”Mwisho wa kunukuu.

Tusome Katiba ya CCM 1977 toleo 2022, Ibara 8(2)(6), Ibara 15(4)(7), Ibara 12(1)(a) ili kwenda kusoma uk. 152, vifungu 1, 8, na 9.

Tukisoma kitabu Kujenga Ujamaa Tanzania: Miaka Kumi ya Kwanza, ambacho kati ya watunzi wake alikuwepo Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, uk. 3, ibara 8 kinatueleza:

“Kwa kadri inavyowezekana, viongozi lazima wawe wanaielewa siasa ya chama ili wawe na misimamo, uwezo wa kuieleza, na kuitekeleza, na kuhakikisha kwamba kazi za chama zinatendeka na malengo ya chama yanatimizwa.”Mwisho wa kunukuu.

Malengo mojawapo ya CCM kikatiba ni utii wa sheria ndani ya utawala bora ambamo hapaswi kuwepo vitendo vya kubebana kwenye maovu na kupendeleana.

Tusome Katiba ya CCM 1977 toleo 2022, Ibara 5(4) ili kupata idhini ya kwenda kusoma kitabu cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kiitwacho Ujamaa: Essays on Socialism, uk. 80, The Rule of Law.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anatusisitiza ya kuwa ni muhimu ikiwa utawala wa sheria utatumika kwa haki sawa kwa wote. Tukisoma kitabu kilichotolewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Agosti 2020, kiitwacho Mwelekeo wa Sera za Chama cha Mapinduzi Katika Kipindi cha Mwaka 2020-2030, uk. 194, ibara 144, kinatueleza:

“Mwelekeo wa chama katika miaka kumi ijayo ni kuhakikisha serikali zake zinaimarisha utawala wa sheria kwa kuzingatia misingi ya utu, haki, na usawa.”Mwisho wa kunukuu.

Ushauri wangu:Kwa vile tunajionyesha kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu, na ili kuepuka jamii kutuona watu wanafiki, naomba watu wanaolalamikiwa kukiuka sheria watolewe kwenye vyeo ili kutendeana haki kwa viapo na ahadi tulizoapa za kuwa viongozi wasiokuwa wabaguzi wala wapendeleaji. Tukishindwa hili, tujuwe kabisa hata watu waliojawa kwenye magereza nao ni Watanzania na wana haki sawa na hawa tunaojaribu kuwalinda. Matendo ya kulinda uovu yanatufanya jamii ituone nasi ni waongo na matapeli wenye kujitamkisha neno Mwenyezi Mungu huku tukiwa hatumaanishi.

Nabii IPM wa Kanisa lililo Mbezi Beach Mbuyuni, nakumbuka tarehe 07/12/2024 alisema:

“Hatuwezi kukubali kutokusema ukweli eti kisa tu tunamkwaza mtu fulani. Hapana. Bora mimi unichukie. Mimi bora nichukiwe na watu wote lakini niuseme ukweli wa Mungu unaotakiwa kusemwa.”Mwisho wa kunukuu.

Nakumbuka tarehe 17/11/2024, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema:

“Taarifa za uchunguzi zitakapopatikana, basi taarifa hizi zitawekwa wazi kwa wananchi wote. Na hatua za kisheria zitakazochukuliwa na serikali zitaelezwa kwa uwazi na kwa kina.”Mwisho wa kunukuu.

Kidumu Chama Cha Mapinduzi.

Mathias Mugerwa Kahinga.
 
Back
Top Bottom