Kwako Paul Makonda, mkuu wa mkoa wa Dar es salaam,
Hongera na pole kwa jukumu ulilopewa la kuongoza jiji kubwa kuliko yote Tanzania. Ni imani yangu unalimudu jiji vizuri kabisa hata kuiridhisha mamlaka yako ya uteuzi na kufikia hatua ya kukupongeza hadharani tofauti na wateule wengine.
Napenda kukupongeza tena kwa ujasiri uliouonyesha wa kupambana na madawa ya kulevya kitu ambacho wengi waliopita katika nafasi yako hawakuwahi hata kujaribu japo kwa kunong'oneza tu, kwa hilo nakupongeza hadi hapo ulipofikia ingawa kuna makosa uliyoyafanya ila naamini ni ujana tu na ndio wanasemaga 'ujana maji ya moto'
Mheshimiwa mkuu wa mkoa,baada ya kukupongeza sasa niende moja kwa moja katika kile kilichonishawishi kuandika waraka huu kwani sikuandika ili kukupongeza tu,kuna jambo..
Mheshimiwa mkuu wa mkoa,ni siku kadhaa sasa tangu uanze kutuhumiwa mitandaoni eti wewe umeiba/umenunua jina la mtu aliyesoma kwa bidii na kufanikiwa kupasua vyema kunako darasa na umetumia cheti chake kujiendeleza kimasomo,kwani wewe cheti chako kimedhoofu sana na hakikuweza kukubeba ufike kule unakotaka kufika.
Mheshimiwa mkuu wa mkoa,wengine wamefika mbali kabisa na kuonesha kukujua kupitiliza na kudai eti wewe sio Paul Makonda eti Paul Makonda ni huyo wanaedai wewe unatumia cheti chake, eti wamekutaja kwa jina la Daudi Bashite wakidai ndio jina lako halali.
Mheshimiwa mkuu wa mkoa, tuhuma hizi zinazoelekezwa kwako zimeshika kasi kuliko moto wa kifuu pale kinapokolea na hazikomi siku hadi siku na sioni zikikoma bila kuwepo wa kukanusha.
Mheshimiwa mkuu wa mkoa, wewe kama kiongozi ni jambo la busara sana kujitokeza ukiwa na vyeti vyako vyote pamoja na cheti chako cha kuzaliwa ili kuwaziba midomo wale wote wanaodai ulitumia jina lisilo lako kujiendeleza kielimu..sio busara wewe kuendelea kudai hizo ni tuhuma za mtandaoni eti tuziache mitandaoni,ni kwanini tuziache mtandaoni zikiendelea kukuchafua wakati upo hai na unaweza kuita vyombo vya habari vikafika na ukamwaga ushahidi wote wa kuwaziba mdomo wale wanaokutuhumu kila siku?
Mheshimiwa mkuu wa mkoa, pia ni vizuri ukamtafuta huyo bwana wanaedai unatumia jina lake ili uwadhihirishie mbele ya wanahabari kwamba ni mfanano wa majina tu!
Mheshimiwa mkuu wa mkoa, sioni kama ni vizuri kila unapotuhumiwa ujifiche katika mwavuli wa madawa ya kulevya, eti kwamba kila wanaokutuhumu ni wale uliowaumiza katika vita yako ya kupambana na madawa ya kulevya, hapana tuhuma nyingine ni rahisi sana kuzimaliza na sio kutumia vita dhidi ya madawa ya kulevya kutafuta huruma ya wananchi.
Mheshimiwa mkuu wa mkoa, kamwe usiwasikilize wale wanaokudanganya eti kukutaka uendelee kunyamazia tuhuma kama hizi za kutumia cheti cha mtu kujiendeleza. Hao kaa ukijua kabisa hawakutakii mema, wanakuharibia! Kila inapokuja tuhuma dhidi yako wanakukingia kifua kwa kudai hao wanaokutuhumu ni miongoni mwa walioumizwa na vita yako dhidi ya madawa.. Tuhuma kama hizi ni vizuri sana kutokujificha chini ya mwavuli wa madawa ya kulevya na ukajitokeza kizijibu kwa ushahidi ili kuwanyamazisha hao ambao unaamini wanakutuhumu kwa kuwa uliwaumiza kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya.
Mbali na hapo mheshimiwa mkuu wa mkoa nategemea utapitia waraka huu, na kama utaelewa basi utafanya vyema kuzimaliza kabisa tuhuma zinazoelekezwa kwako, kwani tuhuma hizo sio ndogo na pia sio nzuri kwa kiongozi.
Jipange, jitokeze, uyamalize!