Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mikataba mbali mbali ya Kikanda na Kimataifa ya kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya Wanawake, kama mkataba wa Cedaw ambao umeanzishwa mwaka 1987 na kuheshimu haki za Wanawake kama Haki za Binaadamu.
Licha ya kuwa Katiba ya nchi inatambua haki za raia wote, bado Wanawake kama walivyo raia wengine, hawajui haki zao na namna ya kuzitafuta hii inatokana na sheria kuandikwa kwa lugha ya kigeni na ya kisheria.
Katika ulimwengu wa sasa suala la usawa wa kijinsia, limekuwa suala muhimu sana hasa linapozungumziwa ushiriki wa Wanawake katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi.
Miongoni mwa mambo yanayowarudisha nyuma Wanawake katika kugombea nafasi za uongozi ni mifumo dume, mila na desturi lakini pia mgawanyo wa majukumu kijinsia jambo ambalo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025 Wanawake wamejipanga, na majukumu ya nyumbani sio kikwazo tena kwa Wanawake kugombea nafasi za uongozi.
Pavu Juma Abdallah, Naibu Katibu Mkuu wa Haki za Binadamu kutoka Chama cha ACT Wazalendo ambae alishawahi kugombea nafasi mbalimbali katika chama hicho ni mmoja wa Wanawake wanaoona kuwa, majukumu ya nyumbani sio kikwazo tena kwa Wanawake kuwa viongozi.
Amesema kwenye siasa kuna changamoto nyingi zinazowakumba Wanawake ikiwemo ukosefu wa fedha za kujikimu wakati wa kampeni lakini majukumu ya nyumbani hawayachukulii tena kama kikwazo cha wao, kushiriki na kugombea nafasi za uongozi, majukumu ya nyumbani haisi kama ni kikwazo kwani ni lazima ujipange vizuri katika majukumu na mikakati yako.
Anaweleza kuwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni vizuri Wanawake wakagombea katika majimbo nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo Udiwani, Uwakilishi na Ubunge kwani huko bado kuna upungufu wa wagombea wanawake.
Maryam Ali Mussa, Diwani wa Viti Maalum kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema kuwa majukumu ya nyumbani ni mujibu kwa Mwanamke mfano mzuri ni kwa mama Samia yeye ni Rais lakini tunamuona siku anayokuwa na muda anaingia jikoni anapika kwasababu ni kazi za mwanamke.
"Kazi za nyumbani tunafundishwa tangu tuko wadogo majumbani kwetu, vipi ziwe kikwazo zitufanye tusishiriki katika kugombea nafasi za uongozi ambazo ni haki yetu ni kujipanga tu,” amehoji Maryam.
Amesema hayo sio kikwazo tena kwa Wanawake kwani upo mfano mzuri Tanzania wa Rais Mwanamke ambae amejipanga hadi kufika pale, kuelekea Uchaguzi Mkuu ni muhimu Wanawake wakawa na uthubutu kujitupa majimboni kugombea.
Anaongeza kuwa Wanawake katika uongozi sio tu sauti za mabadiliko, bali ni chachu ya kufikia Dunia yenye usawa na matumaini.
Sensa ya watu na makaazi ya Mwaka 2022 inaonesha Zanzibar ina Watu milioni 1.8 kati ya hao Wanaume ni 915,492 na Wanawake ni 974, 281, hii inamanisha kwamba Wanawake ni asilimia 51.6 ya wakaazi wote wa Zanzibar lakini wingi wao huo hauonekani katika nafasi za uongozi.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa upande wa Zanzibar kutoka CCM, Tunu Juma Kondo amesema licha ya Wanawake kuwa ni wengi bado kumekuwa na upungufu wao kushiriki katika nafasi za uongozi.
Akizungumzia kuhusu majukumu ya nyumbani kwa Wanawake amesema sio kikwazo kabisa, kwani wapo watu ambao ni Wafanyakazi wanaenda kazini lakini wakirudi nyumbani wanaihudumikia familia na hawaoni kama ni kikwazo.
Amesema kuwa, takwimu zinaonesha Wanawake wapo kidogo katika nafasi za uongozi Hali hiyo inaonesha haja ya Wanawake kuongezeka katika nafasi za uwakilishi katika majimbo, ifikapo uchaguzi wa 2025, kwani idadi ya Wanawake ni kidogo katika majimbo.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) idadi ya wajumbe wote ni 78 kati yao Wanawake ni 29 na Wanaume 48, huku Wanawake wawakilishi wa majimbo kupitia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 ni wanne tu, Wanaume wakiwa 42 na Wanawake wa Viti Maalum ni 18 na Wajumbe waliobakia ni nafasi za kuteuliwa na Rais.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul amesema tathimini iliyofanywa na wizara hiyo, katika taasisi mbalimbali imeonesha kuwa Wanawake bado wapo kidogo katika nafasi za Uongozi, ukilinganisha na Wanaume jambo ambalo linahitaji kuangaliwa.
‘’Takwimu zilizokusanywa na wizara kutoka taasisi mbali mbali kwa mwezi machi mwaka 2024, zinaonesha ni asilimi 30 tu ya Wanawake ambao wako katika uongozi, ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 70," amesema Naibu Waziri Anna.
Anna, ameongeza Serikali inaendelea na jitihada katika kufikia malengo yaliyowekwa kupitia Dira ya 2050 na mpango wa Maendeleo (ZADEP) 2021/2026 ambapo lengo katika nafasi za uongozi ni kufikia 50/50. “ Serikali imejipanga kuhamasisha ushiriki wa Wanawake katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi na lengo ni kufikia 50/50,” amesema Anna.
Mohamed Ali Ahmed, ni Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania kwa upande wa Zanzibar amesema kuongezeka kwa Kifungu cha 10 C ndani ya Sheria ya Vyama vya Siasa, kinatoa nafasi kwa Wanawake kuongeza ushiriki wao na kuwajibika kwa vyama kwa kuwa na sera ya jinsia muda wote kwani hapo awali havikupaswa vyama kuwa na sera hiyo,” amemaliza naibu msajili huyo.
Na Maryam Nassor, Zanzibar