Pili Mwinyi
Waislamu kote duniani bado wanaendelea kutekeleza nguzo ya nne ya Usilamu yaani kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hivyo leo tena napenda kuendelea kuzungumzia nguzo hii, na vilevile kuwafahamisha watu waliopo nje ya China, jinsi mimi na waislamu wenzangu wa hapa China tunavyoishi kama waislamu, hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Tangu nifike nchini China, sasa inapata miaka 14. Katika kipindi chote hicho nimeshuhudia mambo mengi pamoja na mabadiliko makubwa mazuri yanayojitokeza katika kila nyanja. Lakini zaidi nikiwa kama mwislamu sina budi pia kufuatilia nyanja hii ya Uislamu na kufahamu taratibu za Waislamu wa China jinsi zinavyokuwa, ili kuweza kwenda nao sambamba.
Katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani wageni wa mataifa mbalimbali ambao ni waislamu tuliopo China, tunapata fursa ya kutekeleza ibada hii tukufu, kama wanavyotekeleza waislamu wengine kote duniani.
Ieleweke kwamba kila mgeni lazima atakuwa na mazoea na desturi zake, yaani kufunga kulingana na utaratibu wa nchi yake, lakini jambo moja ambalo tunafanana wageni sote, ni kuanza kufunga siku moja kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu ya China, bila kujali nchi yako inaanza na kumaliza lini mfungo wa Ramadhani.
Uzuri ni kwamba desturi hizi za wageni tunaoishi pamoja hapa China huwa tunazichanganya na kupata desturi moja nzuri sana. Mimi nina bahati ya kuishi na Waislamu wageni kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo wafanyakazi wenzangu na marafiki zangu kutoka nchi za Afrika, Asia, Kiarabu, Ulaya na hata Marekani. Kawaida katika kipindi hiki huwa tunapanga kukutana na kuftari pamoja, ambapo kila anayeshiriki kwenye futari ya pamoja “analazimika” kupika vyakula vyenye asili ya nchi yao au vinavyopendwa nchini kwao. Nasema tunalazimika kupika na si kwenda kununua migahawani, kwasababu ni lazima tuwe na uhakika na kile tunachokula, nikimaanisha kuwa ni lazima tule chakula kilicho halali.
Wakati wa futari ya pamoja, hapa utaona utamaduni wa vyakula vya nchi mbalimbali ukikutana pamoja na kuifanya China kuwa kama jukwaa la kutambulisha tamaduni hizi.
Ni muda mrefu sasa nipo China lakini, kuna baadhi ya mambo ya nyumbani huwa nayakumbuka sana katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwanza kwa msomaji wangu, unatakiwa kufahamu kuwa mimi ni mwislamu ninayetoka Kisiwa chenye asilimia kubwa sana ya Waislamu yaani Zanzibar, hivyo ikifika kipindi hiki, mazingira ya kuingia kwa mwezi wa Ramdhani huwa yanaonekana wazi. Kwasababu huu ni wakati ambao migahawa yote hufungwa wakati wa mchana, na kufanya hata wale wasio kuwa waislamu kujizua kula hadharani. Tofauti na hapa China kwa kuwa asilimia ya waislamu sio kubwa sana hasa hapa Beijing, hivyo hakuna mabadiliko makubwa kati ya siku za kawaida na siku za Ramadhani.
Pili ifikapo jioni kila mtaa unaopita basi harufu nzuri ya futari zinazoandaliwa inahanikiza kila pembe. Katika mwezi wa mfungo, muda wa jioni mara nyingi wanawake wanakuwa jikoni kuandaa vyakula vya aina mbalimbali, na hapa ndio naikumbuka desturi ya Wachina kula vyakula vya aina mbalimbali katika kila mlo wao.
Tatu wakati wa jioni ama wakati wa kufungua, kawaida barabarani huoni gari wala baiskeli, kwasababu watu wengi wanazama majumbani kwao wakipata futari kwa pamoja. Na hata kama utaona watu njiani ama gari basi zinakuwa moja moja tu, nazo zinakimbilia nyumbani ili watu wapate kuwahi kufutari.
Katika Makala yangu iliyopita nilitaja kitu kimoja kwamba Waislamu Wachina wanaoishi karibu na misikiti huwa wanaandaa vyakula ili kuwakirimu wasafiri na watu wasiojiweza. Lakini bahati mbaya kwa kule ninakotoka ni kwamba watu wanaamua tu kuwa siku fulani nitakwenda kuwafutarisha watu wa aina fulani, lakini hakuna utaratibu wa watu wanaoishi karibu na msikiti kupika futari kila siku na kupeleka msikitini.
Katika maisha yangu kama muislamu hapa China, ibada nyingi naweza kuzitekeleza kama ipasavyo tena bila kizuizi chochote. Ila kwa wanaume ambao wamezoea kusali msikitini, inakuwa vigumu kwao kwenda msikitini kwa kila swala kutokana na umbali wa maeneo tunayoishi na ilipo misikiti. Hivyo sala ya magharibi na isha, ambazo ni muhimu sana kuswaliwa msikitini wakati wa Ramadhani, inawalazimu kuziswali nyumbani tu.
Kitu kimoja nilichojifunza ni kwamba unapokuwa ugenini ni lazima ufuate taratibu za wenyeji wako. Ndio maana Waislamu wageni sote tunaoishi China, hadi sasa tumeweza kutangamana vizuri na wenzetu wenyeji hasa katika kutekeleza ibada mbalimbali za dini ya Kiislamu. Nawatakia Mfungo Mwema wa Ramadhani. “Kai Zhai Jie Kuai Le”