SoC04 Magonjwa yasiyoambukizwa yatokanayo na mfumo wa maisha janga lililogeuziwa kisogo, iwekwe mikakati imara kupambana nayo

Tanzania Tuitakayo competition threads

Forever Queen

New Member
Jan 22, 2023
1
1
Magonjwa yasioambukizwa sio jambo geni masikioni mwetu, shuleni tumesoma baadhi ila kwa juu juu sana. Magonjwa yaliyopewa kipaumbele ni magonjwa ya kuambukiza, elimu yake imekua ikitolewa mpaka mtaani. Lakini kadiri ya siku zinavyosonga magonjwa yasioambukiza yamezidi kujinafasi na kua hatari zaidi. Uhatari wa magonjwa yasioambukiza hutokana na kukosa tiba sahihi.

Magonjwa yasioambukiza yanachangia 74% ya vifo vyote vinavyotokea duniani. Kwa makadirio ni vifo vya takribani watu milioni 41 kila mwaka hutokana na magonjwa hayo. Kwa maana hiyo ni nguvu kazi kubwa sana inapotea kutokana na mfumo wa maisha.

Hata hivyo, serikali na mashirika ya bima yanajikuta yakiingia gharama kubwa zinazoweza kuepukika. Hii ni kutokana na matibabu ya magonjwa hayo kuchukua muda mrefu na pia matibabu yake ni gharama kubwa

Magonjwa yasioambukiza yaliyochukua nafasi kubwa Tanzania na duniani kiujumla ni magonjwa ya moyo, kansa, magonjwa ya mfumo wa upumuaji, kisukari na magonjwa ya ini na figo. Magonjwa haya ambayo yanazidi kushika kasi ya ukatishaji wa maisha ya watu kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na mifumo ya maisha.

Mfumo wa maisha ya mtu inajumuisha anachokula, anachofanya na anachochangamana nacho kwenye mazingira. Mfumo wa maisha ya mtu huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye afya ya mwili, akili na kiroho ya mtu husika. Watu wengi hupendelea mfumo wa starehe bila kujali suala la afya yake mpaka pale itakapoathirika.

Uthibitisho wa hili ni tunayoshuhudia mitaani, idadi ya watu wenye unene uliopitiliza unazidi kuongezeka kila siku. Watu wanaolalamika kusumbuliwa na presha na kisukari ni wengi pia. Vifo vya ghafla vinavyotokana na presha na mshtuko wa moyo vinaongezeka pia. Wagonjwa wa saratani mbalimbali wanaongezeka siku hadi siku, jambo hili sio la kawaida wala sio la kufumbia macho ni jambo linaloepukika.
1715705321093.png
1715705588951.png

Chanzo: Lancet 2024
Mifumo ya maisha inayosababisha magonjwa yasiyoambukiza;
  • Matumizi ya tumbaku (uvutaji wa sigara)
  • Matumizi yaliyozidi ya pombe
  • Matumizi ya sukari na chumvi kupita kiasi
  • Ukosefu wa mazoezi ya mwili
  • Ulaji usio na mpangilio
  • Uchafuzi wa hewa
Haya ni mambo yanayoweza kuepukika, sio ya lazima kwenye maisha ya binadamu. Lakini watu wengi wameshindwa kuyaepuka iwe kwa kukosa elimu (kutokujua) au kwa kujua. Kutokana na hili inabidi serikali kuweka mikakati mathubuti ili kuhakikisha wanailinda nguvu kazi ya taifa, kutokana na waathirika wengi kua ni vijana ambao ndipo nguvu kazi ilipo.

Mikakati ya kupambana na magonjwa yasioambukizwa;
1. Somo la lishe kufanywa la lazima kwa shule za msingi na sekondari
Wapo wanaopatwa na mazila haya kutokana na kutokua na elimu ya lishe. Hajui aina za vyakula wala madhara yatokanayo na ukosefu au uzidishaji wa aina fulani ya chakula. Hivyo, wakipata elimu hii kiundani kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari wataepukana na magonjwa hayo
2. Kuongeza ushuru kwenye bidhaa zinazochangia magonjwa yasiyoambukiza
Zipo bidhaa nyingi (vyakula, vinywaji na sigara) zipatikanazo kirahisi na kwa bei nafuu jambo ambalo hupelekea watu wengi kutumia kwa kiwango kikubwa bila kuelewa janga wanalojitengenezea. Vinywaji vyenye sukari nyingi kama soda na juisi za makopo, vinywaji vyenye ‘caffein’ kama ‘energy drinks’, vinywaji vyenye vilevi kwa kiwango kikubwa vyote hivi vinapatikana mtaani kwa urahisi na bei ndogo. Vinywaji hivi vinachangia kwenye magonjwa ya moyo, kisukari, figo na ini.

Sigara zinapatikana mitaani kirahisi na kwa bei ndogo ambazo zinateketeza mapafu ya vijana chungu nzima mitaani lakini hakuna anayejali. Pia vyakula vya makopo vinapatikana mitaana lakini madhara yake kiafya ni makubwa pia.

Uraisi wa upatikanaji na bei ndogo za bidhaa hizi hupelekea kutumiwa na watu wengi bila kuelewa madhara wanayojipatia. Serikali kwa kutambua hili iongeze ushuru kwa kiasi kikubwa kwenye bidhaa hizi ili bei yake iongezeke. Bei ikiongezeka matumizi yatapungua. Matumizi yakipungua madhara yake pia yatapungua. Ikibidi baadhi ya bidhaa kama za ‘energy drinks’ na sigara zizuiliwe kuuzwa kwenye maduka ya kawaida na watakaouza wawe na vibali maalumu ili kupunguza matumizi yake.

Serikali isihofie kupoteza mapato yanayotokana na bidhaa hizi kwani pesa inayopotea kutokana na vifo na magonjwa yatokanayo na bidhaa hizo ni nyingi zaidi ukilinganisha na mapato yatakayopotea.

3. Kuhamasisha mazoezi ya mwili kwa wananchi.
Ukosefu wa mazoezi ya mwili huchangia uzito mkubwa wa mwili ambapo husababisha magonjwa ya moyo. Ni vyema kuhamasisha mazoezi ya mwili kwa raia ili kuepukana na unene uliopitiliza. Uhamasishaji sio tu kwa kuweka matangazo na kuandaa mashindano mbalimbali. Bali pia kwa kuhakikisha serikali inapojenga miundombinu mbalimbali kuhakikiasha na miundombinu ya mazoezi inapewa kipaumbele.

Barabara za magari zinapojengwa itengwe na sehemu za waendesha baiskeli na sehemu za mazoezi ya kukimbia. Kuhakikisha kila kituo cha elimu (shule na vyuo) vinakua na viwanja vya michezo. Pia kwenye ofisi kubwa za serikali watenge sehemu ya kufanya mazoezi ya mwili, kutokana watumishi wengi wa maeneo hayo kutumia muda mwingi wakiwa wamekaa sehemu moja.

4. Kutoa semina na matangazo kwenye vyombo vya habari kuhusu magonjwa yasiyoambukiza
Kuhakikisha semina zinatolewa mitaani, mashuleni, hospitalini na maeneo mengine ya umma juu ya magonjwa yasioambukiza, visababishi, madhara na njia za kuepuka magonjwa hayo. Pia kupitia vipindi maalumu na matangazo kwenye vyombo vya habari na mitandaoni watu wafahamishwe kuhusiana na magonjwa yasiyoambukizwa. Hii itasaidia elimu hii kuwafikia watu wengi zaidi na kuwaepusha kukumbwa na magonjwa hayo kutokana na kukosa elimu
5. Kutoa huduma ya upimaji wa bure wa magonjwa yasiyoambukiza
Serikali kuhakikisha vipimo vya mwili vinafanyika bure kwa raia wote. Itasaidia watu wengi kufanya vipimo vya mwili na kutambua kama wapo hatarini kupatwa na magonjwa yasioambukizwa. Watapewa na elimu zaidi ya namna ya kujikinga na kulinda afya zao kutokana na mifumo yao ya maisha.
6. Wafanyakazi wa serikali na sekta binafsi kuwekewa utaratibu wa kupima afya za kila baada ya kipindi fulani
Hili litawezekana kwa kuweka sheria itakayowataka wafanyakazi wote wa serikalini na sekta binafsi kufanya vipimo vya afya zao kila baada ya muda fulani (kila baada ya miezi mitatu au sita). Itasaidia magonjwa haya kubainika mapema na kuweza kutibiwa mapema na kwa gharama ndogo ili kuepusha kuleta madhara makubwa kwa mhusika.

Mwisho kabisa inabidi tutambue afya bora ni msingi imara wa taifa bora. Kulinda afya zetu liwe jukumu letu la kwanza kabisa ili kuepuka madhara na gharama zinazoweza kuepukika. Kila kitu kikizidi mwilini kina madhara, starehe tunazozifanya leo zisijekututesa siku zijazo. Siku hizi watu kwa kutokutambua au kwa kupuuzia wanatumia gharama kubwa sana kuharibu afya zao.
 
Barabara za magari zinapojengwa itengwe na sehemu za waendesha baiskeli na sehemu za mazoezi ya kukimbia. Kuhakikisha kila kituo cha elimu (shule na vyuo) vinakua na viwanja vya michezo. Pia kwenye ofisi kubwa za serikali watenge sehemu ya kufanya mazoezi ya mwili, kutokana watumishi wengi wa maeneo hayo kutumia muda mwingi wakiwa wamekaa sehemu moja.
Nimeipenda hii ya kuwepo visehemu maalumu kwa baiskeli, sema nawaza bodaboda nao wakipitapo mmmmh!🤒.

Mwisho kabisa inabidi tutambue afya bora ni msingi imara wa taifa bora. Kulinda afya zetu liwe jukumu letu la kwanza kabisa ili kuepuka madhara na gharama zinazoweza kuepukika. Kila kitu kikizidi mwilini kina madhara, starehe tunazozifanya leo zisijekututesa siku zijazo. Siku hizi watu kwa kutokutambua au kwa kupuuzia wanatumia gharama kubwa sana kuharibu afya zao.
Queen tunakubaliana, sema tu watu labda hawajaamua kuweka kipaumbele katika masuala ya afya zaidi. Ona mfano wa elimu anayojitahidi kuitoa Prof. Janabi huwa inapokelewa vipi mitandaoni?

Na haya magonjwa kuna watu kama Ellen White huyaita magonjwa yanayotokana na kukiuka kanuni za asili kundi moja na dhambi. Na ni kuna kaukweli kwamba watu hawapaswi kuteseka isipokuwa wanapokuwa wamefanya makosa fulani. Ujinga ni makosa na upumbavu ni dhambi kabisa!

Ujinga na upumbavu unaozungumziwa hapa ni ule ambao elimu tayari ipo lakini mtu anaikataa kwa kutojua vizuri au kimakusudi kabisa
Screenshot_20240514-195214_Chrome.jpg

Ahsante kubwa kwa mnaojitahidi kizidi kuisambaza elimu kwa jamii. Rai kwa jamii kuikubali elimu hiyo na kuitumia kujikinga na magonjwa haya.

Magonjwa yamegusa eneo la mtindo wa maisha, eneo ambalo serikali haina utawala mkubwa kwa kanuni za uhuru na faragha. Tunapimwa mtu mmoja mmoja hapa zaidi, tujitahidi.
 
Back
Top Bottom