Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,807
- 13,575
Maelezo ya Prof. Kitila Alexander Mkumbo, Akihitimisha Hoja ya Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo
Ijumaa, 10 Novemba 2023, Dodoma
Ijumaa, 10 Novemba 2023, Dodoma
- Mheshimiwa Spika,
- Ninaomba kukushuru wewe pamoja na wasaidizi wako, Mheshimiwa Musa Zungu (Naibu Spika), Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mwenyekiti wa Bunge), na Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mwenyekiti wa Bunge), kwa jinsi mlivyoendesha mjadala huu kwa umakini na uwazi wa hali ya juu.
- Ninarudia tena kuwashukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa uchambuzi wao makini na jinsi walivyoibua maeneo mapya katika mapendekezo ya Mpango.
- Waheshimiwa Wabunge wote, na hususani wabunge 116 waliopata nafasi ya kuchangia, kwa kuongea ndani ya ukumbi huu, kutoa taarifa (29) na wengine waliochangia kwa maandishi.
- Kwa kweli kwangu binafsi wiki hii moja nilikuwa darasani. Nimejifunza mengi na kubainisha vyema zaidi kuhusu kile ambacho watanzania, kupitia kwa waheshimiwa wabunge, wanataka kutoka kwa Rais wao, kwa serikali yao na kwa nchi yao. Waheshimiwa wabunge itoshe tu kusema tumewasikia na tutazingatia maoni na ushauri wa watanzania kupitia sauti zenu.
- Mheshimiwa Spika, Kupitia mjadala huu, pamoja na mambo mengine, tumeweza kubaini zaidi vipaumbele vya nchi yetu. Jedwali la hapa chini linaonesha maeneo na kiwango (frequency) ambapo eneo hilo limeongelewa. Takwimu hizi zitatusaidia kupanga vizuri vipaumbele vyetu.
Eneo/Sekta | Frequency | % |
Miundombinu ya usafirishaji | 68 | 22% |
Kilimo, mifugo na uvuvi | 65 | 21% |
Nishati | 36 | 12% |
Utalii na hifadhi | 38 | 12% |
Viwanda | 33 | 11% |
Biashara na uwekezaji | 25 | 8% |
Sekta binafsi | 12 | 4% |
Mengine | 30 | 10% |
Jumla | 307 | 100% |
- Mheshimiwa Spika, Kupitai mjadala huu, tumeendelea pia kubaini baadhi ya kero za wananchi. Tumezipokea na tutazizingatia. Kwa kipekee, niwaambie wananchi wa Mbarali kwamba kupitia kwa Mbunge wenu mahiri, Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, tumewasikia. Aidha, tumewasikia wananchi wote wanaoishi karibu na hifadhi mbalimbali nchini.
- Kwa niaba ya Mheshimwa Rais na viongozi wetu wengine wakuu na kwa niaba ya waheshimiwa mawaziri wenzangu, niwaeleze wananchi kwamba Rais wetu anathamini maendeleo ya watu kuliko chochote.
- Kila kitu tunachokifanya nia na lengo letu ni hatimaye mwananchi mmoja mmoja, jamii na nchi yetu kwa ujumla inufaike.
- Hatutafanya jambo lolote ambalo hatima yake ni kuumiza wananchi. Hii ni Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. Pamoja na sifa zingine, Rais wetu ni muungwana na mpenda haki. Rais wetu ni mama mwenye huruma na mapenzi kwa watu wake. Rais wetu ni muadilifu na mzalendo. Maelekezo yake kwetu ni kwamba tuwatumikie wananchi, sio kuwaumiza. Zaidi ya yote, hii ni Serikali ya CCM.
- Kwa asili yake, panapotokea mgongano kati ya miradi ya maendeleo na utu/maisha ya watu, CCM siku zote hukaa upande wa utu na maisha ya watu. Kwa hiyo tunao mwongozo. Na katika jambo hili tutakaa na kujipanga ili kuona kwamba hifadhi zetu nchini haziwi kikwazo au kugeuka mateso kwa wananchi wetu. Hifadhi zetu lazima zithamani maisha ya wananchi wetu ili wananchi nao wazithamini. Tutajipanga na tutakuja na jibu endelevu.
- Mheshimiwa Spika, Katika mjadala huu, waheshimiwa wamebainisha au kusisitiza baadhi ya maeneo mapya ya kipaumbele. Tutayazingatia katika kuandaa Mpango. Maeneo haya ni pamoja na:
- Artificial Intelligence
- Uchumi wa Gesi
- Fursa za Jiografia yetu
- Utafiti na Maendeleo (R&D)
- Fursa za mabadiliko ya tabia nchi (hewa ya ukaa)
- Haja ya kuanzisha Mamlaka ya Ufugaji na Uvuvi
- Haja ya kuanzisha Mamlaka ya Maendeleo Vijijini
- Mheshimiwa Spika, Naomba kusisitiza na kutolea ufafanuzi kidogo maeneo mawili, ambayo pia yamesisitizwa sana na waheshimiwa wabunge:
- Maendeleo Vijijini: Nafurahi kuona kwamba waheshimiwa wabunge wameunga mkono na kuweka pia msisitizo mkubwa katika eneo hili. Tayari tuna msingi. Kupitia TARURA, mtandao wa barabara vijijini umeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni. Kupitia REA, vijiji vingi sasa vina umeme.
- Na kupitia RUWASA huduma ya maji inaendelea kusambaa. Aidha, huduma za afya na elimu zinazidi kusambaa katika vijiji vyote nchini. Sasa watu wetu wakishakuwa na afya, wakapata elimu, wakapata maji na umeme na wakaunganishwa katika mtandao wa barabara, tunahitaji kutumia haya yote kama nyenzo ya kuchochea uzalishaji ili hatimaye wananchi wetu huku vijijini wapate fursa za kiuchumi za kutengeneza kipato.
- Ndiyo nia yetu ya kusisitiza umuhimu wa kuvutia uwekezaji wa viwanda vidogo vijijini kwa ajili ya kufanya primary processing. Sio tu ni muhimu bali ni LAZIMA sasa kuweka nguvu zetu kwa Uchumi wa Vijijini ili kutomokeza umasikini nchini.
- Umuhimu wa kujenga Mwafaka wa Kitaifa: wataalam wa maendeleo wanakubaliana kwamba moja ya kikwazo cha maendeleo katika nchi yoyote ile ni pale ambapo panakuwa hakuna mwafaka kuhusu mipango na vipaumbele vya maendeleo miongoni mwa wananchi, na hususani watu wenye sauti katika jamii: viongozi wa makundi mbalimbali, wasomi, wafanyabiashara, wanasiasa, n.k. Ndiyo maana ni muhimu sana kushirikishana ili sote tukubaliane kuhusu tunapoenda na kama ni kubishana tubishane tu juu ya njia ya kufika tuendako.
- Baada ya mkutano huu wa Bunge Tume ya Mipango itaweka utaratibu wa kuanza mchakato huo wa kushirikisha makundi mbalimbali kwa ajili ya kupata maoni zaidi kuhusu maeneo ya kipaumbele ya kuzingatia katika Mpango .
- Mheshimiwa Spika, Nihitimishe kwa kujibu swali moja ambalo wabunge wengi wamelizungumzia sana. Katika hitimisho la hotuba yangu nilizungumzia umuhimu wa kuwa na watu wazuri katika utumishi wa umma, nikimnukuu Lee Kuan Yew , Waziri Mkuu wa zamani wa Singapore.
- Sasa swali limeibuliwa na waheshimiwa wabunge, je, tuna watu wazuri katika utumishi wetu wa umma, wakirejea mjadala wa wiki jana wa taarifa ya CAG. Jibu langu ni kuwa ndio tunao, tena wengi sana. Ninaposema Ndiyo ninazingatia walimu 258,291 katika nchi hii wanaowafundisha na kulea watoto wetu; ninazingatia madakatari na wauguzi 48,579 katika vituo vya afya na zahanati ambao wameifanya Tanzania kuwa na kiwango kidogo zaidi cha vifo vya akina mama wazazi katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara; Ninazingatia wahandisi na mafundi zaidi ya 9000 wanaopambana kusambaza maji kwa wananchi huko vijijini. Ninazingatia uadilifu, uzalendo na umakini wa Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Baraza lake la Mawaziri.
- Ninazingatia umakini na uzalendo wa Mheshimiwa Dkt Hussein Ali Mwinyi, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mheshimiwa Dkt. Dotto Mashaka Biteko. Naam ninazingatia umakini, uzalendo na umahiri wa Spika wangu, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, pamoja na ubora wa wabunge hawa waliopo hapa.
- Mheshimiwa Spika, Tunachopaswa ni kuimarisha mifumo yetu ya uwajibikaji na kuendelea kujengea uwezo wa watu wetu kwenye utumishi wa umma. Hatuwezi kukata mwembe wote kwa sababu ya kuoza kwa maembe mawili. Tutayaondoa maembe yaliyooza lakini lazima mwembe ubaki.
- Mheshimiwa Spika, Ninakubaliana na waheshimiwa wabunge kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili kwa watoto wetu. Hata hivyo, tunapoendelea na kuelimisha vijana wetu kuhusu maadili tusije tukawaondolea haki yao ya kuwa watoto.
- Ni muhimu watoto wabaki kuwa watoto kwa sababu bila hivyo watakuja kufanya utoto wakiwa watu wazima. Aidha, utoto wa watoto wetu hauwezi ukawa ulivyokuwa utoto wetu!
- Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, niseme tena kuwa tumepokea maoni na ushauri wa waheshimiwa wabunge na tutauzingatia katika kuandaa mpango wa mwaka ujao.
- Ahsante kwa fursa hii.
Mungu Ibariki Tanzania; Mungu Ibariki Tanzania.