Maelekezo ya Waziri Ndejembi kushughulikia mgogoro wa ardhi wilayani Mlimba yaanza kutekelezwa

May 14, 2024
80
63
Morogoro

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Morogoro Bw. Idrisa Kayera ametekeleza maelekezo ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe. Deogratius Ndejembi kushughulikia mgogoro wa wananchi wa vijiji vya Msolwa Kalengakelo na kitongoji cha Mkuyuni katika kijiji cha Chisano kuhusiana na uvamizi wa maeneo yaliyotengwa na serikali kwa matumizi ya ufugaji pamoja na malisho ya mifugo.

Wananchi wa vijiji hivyo vilivyopo halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro walilalamikia serikali za vijiji kwa kupitisha mpango wa matumizi Bora ya ardhi bila kuwashirikisha.

Kufuatia malalamiko hayo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan hivi karibuni mkoani Morogoro alimuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Bw. Idrisa Kayera kufika eneo hilo kwa ajili ya kushughulikia mgogoro huo haraka.

Katika ziara yake aliyofanya tarehe 3 Oktoba 2024 katika vijiji vya Msolwa Kalengakelo na kitongoji cha Mkuyuni Kamishna Kayera aliwataka wananchi wenye vielelezo vya umiliki maeneo wanayolalamikia kuviwasilishe kwake ambapo baadhi yao waliwasilisha nyaraka za kununua maeneo.

Hata hivyo, wakati wa uwasilishaji nyaraka hizo kulibainika mapungufu kwenye vielelezo vilivyowasilishwa kwa kuwa hakuna mihutasari ya Halmashauri na mkutano mkuu wa vijiji iliyodhinisha kuwapatia maeneo hayo.

Kamishna Kayera aliwakumbusha wananchi wa vijiji hivyo kuhakikisha wanapata vielelezo vyote muhimu vya umiliki wa ardhi zao ili kuepusha migogoro ya ardhi ya mara kwa mara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Samora Bw. Deodatus Mngungusi amesema, migogoro ya ardhi asilimia kubwa inachochewa na wamiliki wenye maeneo makubwa wanayoyamiliki kinyume cha Sheria na kueleza kuwa, wengi wao wanatoka nje ya vijiji vyao ambapo huwashawishi wanavijiji kuvamia maeneo yaliyotengwa na kusababisha migogoro baina ya serikali za vijiji na wananchi.
 
Back
Top Bottom