Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mwishoni mwa wiki imesaini mkataba na Kampuni ya CreditInfo Tanzania Ltd utakaowezesha taarifa za wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kufikishwa katika Kitengo Uratibu za Taarifa za Mikopo (Credit Reference Bureau) kilichopo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kampuni ya CreditInfo Ltd ina leseni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Hivyo basi, mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambaye ataomba mkopo kutoka kwenye taasisi yoyote ya kifedha hapa nchini, taasisi hiyo itakuwa na uwezo wa kuhakiki kama mwombaji huyo ni munufaika wa mkopo wa elimu ya juu na ikiwa ana nidhamu ya kurejesha mikopo.
Kwa mujibu wa mkataba huo, HESLB itawasilisha orodha ya wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kwa kampuni ya CreditInfo ambayo itahakikisha taarifa za wakopaji zinapatikana kwa taasisi zote za kifedha, yakiwemo mabenki, ili taasisi hizo zijiridhishe kabla ya kutoa mikopo mipya kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
“HESLB ina furaha kufanya kazi na CreditInfo kama mdau mpya. Tunawasihi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu waanze kulipa madeni yao ili wawe na hadhi ya kukopesheka na taasisi za kifedha,” amesema kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Jerry Sabi wakati wa hafla fupi ya kutia saini mkataba huo katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa CreditInfo Tanzania Ltd Bw. Davith Kahwa amesema lengo la kampuni yake ni kuhakikisha fursa za ukopaji zinazongezeka na wakopaji wanakuwa na nidhamu kwa mikopo waliyopata.
“Wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao wamekuwa wakilipa watapata fursa ya kipekee ya kujadiliana na taasisi za kifedha kuhusu viwango vya riba kwa sababu ya nidhamu wanayoionyesha kwa mikopo yao,” amesema Bw. Kahwa katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Meneja wa CreditInfo Tanzania Bw. Van Reynders.
”Tumedhamiria kuiunga mkopo HESLB katika kutekeleza majukumu yake hususan yale ya ukusanyaji mikopo iliyoiva,” ameongeza Mtendaji Mkuu huyo wa CreditInfo Tanzania Ltd.
HESLB ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi Julai 2005 ili kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji na pia kukusanya mikopo iliyoiva ambayo imekuwa ikitolewa na Serikali tangu mwaka 1994.
Hadi sasa, zaidi ya Tshs 2.1 trilioni zimetolewa kwa watanzania na, kati ya hizo, Tshs 258 bilioni zimeiva na hivyo kutakiwa kukusanywa kutoka kwa wanufaika. Kiasi kilichobaki kinajumuisha fedha walizopewa wanafunzi ambao bado wanaendelea na masomo na ambao muda wa kuanza kuwadai (miezi 12 baada ya kumaliza masomo) haujafika.
CreditInfo Tanzania Ltd ni sehemu ya Kampuni ya Kimataifa inayofanya kazi kwenye nchi zaidi ya 20 duniai na inayojishughulisha na usimamizi wa taarifa za mikopo. Ilisajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2013.