tutafikatu
JF-Expert Member
- Dec 17, 2011
- 3,304
- 4,580
- Kitundu si msemaji wa Baraza au Faragha ya Maaskofu
- Taarifa aliyoitoa kwenye vyombo vya habari, ilikuwa ya uongo kwa sababu maamuzi yaliyofanywa na Askofu Shoo kumuondoa Mwaikali kwenye Uaskofu, hayakufuata katiba ya KKKT Dayosisi ya Konde na wala hayakupewa baraka kwenye mkutano wa Maaskofu.
- Kitundu ni mwajiriwa ambaye yupo kwenye probation period
- Kitundu amepora usemaji wa Baraza na Faragha ya Maaskofu.
- Askofu Mkuu hana mamlaka ya kuitisha mkutano wa dayosisi yeyote kwa nia ya kufanya uchaguzi wa Askofu hata kama Askofu wa Dayosisi husika amefariki.
- Askofu Mkuu hana mamlaka hata ya kuitisha mkutano wa uchaguzi kwa dayosisi mpya.
- Kitundu amevunja amri ya nane dhidi ya Mhimili wa KKKT.
- Kitundu anadaiwa kutomshauri vizuri Askofu Shoo.
- Kitundu kashauriwa akanushe tamko lake au aachie ngazi.
RAIA MWEMA, JUMATANO, Aprili 13-19, 2022
KATIBU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT), Robert Kitundu, anatuhumiwa na waajiri wake, "kuvunja amri ya nane dhidi ya mhimili wa Kanisa, kwa kauli yake kuwa mkutano wa Baraza la Maaskofu, uliridhia hatua zilizochukuliwa kwenye mgogoro unaofukuta Dayosisi ya Konde.
Taarifa kutoka makao makuu ya KKKT, Arusha na baadhi ya marafiki wa Kitundu, zinasema hatua ya maaskofu hao kumtuhumu Katibu Mkuu wao, kwamba amejipa mamlaka yasiyokuwa yake na "kuwalisha maneno," alipozungumzia mgogoro wa Dayosisi ya Konde inaiweka rehani ajira yake.
Barua ya maaskofu ya Aprili 8 mwaka huu, kwenda kwa Kitundu inasema, hatua yake ya kutoa tamko kuhusu mgogoro wa Dayosisi ya Konde, imelenga kulichonganisha Kanisa na kuwagombanisha na waumini wao.
"Kuna tamko umelituma kwenye vyombo vya habari na linaendelea kuzunguka, likijulisha umma kwamba, katika faragha tajwa. maaskofu tulikubaliana kwa umoja wetu na kauli moja, kuridhia hatua zilizochukuliwa Dayosisi ya Konde.
"Kwa niaba ya wenzangu walio wazi na wasio wazi tunapinga taarifa yako hiyo, kwa sababu imejaa uongo na hatuwezi kuwa sehemu ya uongo huo," inaeleza sehemu ya barua hiyo ambayo gazeti hili limeiona.
Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kichwa cha kuhusu faragha ya maaskofu - Dodoma, 28-29 Machi 2022" maaskofu wanasema, Kitundu si msemaji wa KKKT na kwamba kitendo alichokifanya, ni kuvunja amri ya nane dhidi ya mhimili wa Kanisa hilo.
Haya yanaibuka takribani wiki mbili, tangu Kitundu kutoa taarifa kwa umma, kwamba Mkutano wa Baraza la Maaskofu la KKKT uliofanyika Dodoma, kwa kauli moja, uliridhia kung'olewa mamlakani kwa Mkuu wa sasa wa Doyosisi hiyo, Askofu Dk Edward Mwaikali na majukumu yake kukabidhiwa Mchungaji Mwakihaba.
Aidha, Katibu Mkuu huyo alisema, mkutano wa taratibu za kumsimika Askofu Mteule, Geofrey Mwakihaba zinaendelea na kwamba kazi hiyo itafanywa na Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Dr. Fredrick Shoo.
Hata hivyo, baada ya Kitundu kutoka kauli hiyo, maaskofu wanane walipiga simu gazeti hili, kupinga madai kuwa mkutano wa Baraza la Maaskofu, ulimalizika kwa makubaliano ya kuvuliwa uaskofu Dk. Mwaikali.
Mmoja wa maaskofu ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema, "kinacholeta mgogoro Konde, ni utaratibu uliotumika na Mkuu wa Kanisa kuitisha mkutano nje ya utaratibu."
Alisema: "Hata mahali ambapo Askofu amefariki dunia, si Mkuu wa Kanisa anayeitisha mkutano wa uchaguzi wa Askofu. Hata katika Dayosisi zinazoanza, si Mkuu wa Kanisa anayeitisha mkutano. Hiki kilichofanyika hakikubaliki.
Maaskofu hao, walioshiriki mkutano wa Baraza la Maaskofu, mmoja baada ya mwingine, waliliambia gazeti hili, kuwa kazi anayoifanya Kitundu, haifanani na wito wa Kanisa lao, na kwamba anachokisambaza kwa umma, "ni uongo wenye dhamira ya kulimega."
Aliongeza: "Hakuna makubaliano tuliyofikia na kama unasoma hiyo taarifa si mapatano ya maaskofu na nisihusishwe na tamko hilo Nadhani labda anataka kuligawa tu Kanisa."
Maaskofu wametaja sababu tano za kumwandikia barua Katibu Mkuu huyo, ikiwamo kusema uwongo, uchonganishi, kutokuwa msemaji wa Baraza wala faragha ya maaskofu na kuanzisha mgogoro mpya katikati ya migogoro mingi iliyopo.
Barua imesainiwa na Dk Benson Bagonza, Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Karangwe. Wengine waliojumuishwa kwa kuwekwa majina yao, ni Emmanuel Makala, Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria; Ambele Mwaipopo Mkuu wa Dayosisi ya Ziwa Tanganyika na wengine ambao hawakutajwa majina.
"Taarifa yako hiyo imejaa uongo na hatuwezi kuwa sehemu ya uongo huo," wanaeleza maaskofu na kuongeza, "hatukuzungumza na wala kuamua, kuhusu kilichofanyika Konde."
Maaskofu waliendelea kusisitiza katika barua hiyo, kwamba "wewe (Kitundu) si msemaji wa Baraza wala faragha ya maaskofu. Umepora madaraka ya usemaji wa Baraza na faragha na kutuchonganisha na umma."
Walisema: "Unatuchonganisha na msemaji wetu (Askofu Shoo) aliyeendesha faragha hiyo na si ajabu unamshauri vibaya."
Kwa mujibu wa taarifa hizo, hatua ya Kitundu kuwasingizia maaskofu, wakati bado hajathibitishwa kazini, yaweza kusababisha kupoteza ajira yake.
Katika hili, barua ya maaskofu inasema: "Kwa kuwa ni mwanzoni mwa utumishi wako na umevunja amri ya nane dhidi ya mhimili wa KKKT nakushauri ama ukanushe tamko hilo au ujitathimini ikiwa unatosha kwa nafasi hiyo.
Usipokanusha ndani ya siku mbili tutalazimika kujitenga nalo kwa kutumia njia ulizotumia kulitamka. Tafadhali zingatia.
Usimshuhudie mwenzio uongo
Raia Mwema ilishindwa kumpata Kitundu kwa njia ya simu kutokana na simu yake kuita bila kupokewa kwa zaidi ya saa moja na dakika 12.
Tofauti na huko nyuma, ambako alikuwa akitoa taarifa kadhaa kwa gazeti ikiwamo kutuma yeye mwenyewe alichoita "taarifa kwa umma katika sakata la Konde, Kitundu aligoma kujibu hata ujumbe mfupi wa maneno, aliotumiwa kwa WhatsApp.
Kitundu alituma kwa mwandishi wa gazeti hili, taarifa iliyodai kuwa Askofu Mwalkali si Askofu wa Konde tena, baada ya mkutano wa Baraza la Maaskofu kuridhia kuvuliwa madaraka.
Mgogoro ndani ya Dayosisi ya Konde, umezidi kushikasi, kutokana na hatua ya Askotu Shoo na wenzake, kutaka kumng'oa Askofu Mwaikali, kugomewa na maaskofu wengi, wachungaji wa Dayosisi ya Konde na baadhi ya waumini kwa madai kuwa "ni mradi binafsi."
Dk Shoo ndiye aliunda Kamati Maalumu ya KKKT kutatua alichokita, "mgogoro wa Dayosisi ya Konde. Kamati iliongozwa na Askofu Dk Alex Malasus Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, ambaye amekuwa akituhumiwa kuzidisha mpasuko.
Kupitia Kamati ya Askofu Malasusa, alikusanya wapinzani wa Askotu Mwaikali na kuutangazia umma, kwamba amevuliwa madaraka ya uaskofu na kuhamishiwa makao maku ya Dayosisi kutoka Mbeya Mjini kwenda Tukuyu.
Katikati ya mgogoro huo Askofu Malasusa, alitumia polisi kumfukuza kwenye msiba wa baba yake mzazi Askofu Mwaikali.
Vilevile, kupitia mkutano huo unaodaiwa kufanyika kinyume cha Katiba ya Dayosisi ya Konde. Askofu Shoo alimwagiza Askofu Mwaikali, kukabidhi ofisi za Dayosisi na alama za uaskofu, jambo lililopingwa na kiongozi huyo, wachungaji wake na maaskofu kadhaa.
Ni kupitia unaoitwa, "Mkutano Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Konde" wa 22 Machi 2022, Mchungaji Mwakihaba, ambaye alishafukuzwa uchungaji, tangu Agosti 13 mwaka jana kuwa Askofu Mteule wa Dayosisi hiyo.
Hadi sasa, Mwakihaba hajatawazwa kuwa Askofu kamili, kutokana na wafuasi wa Mwaikali na baadhi ya maaskofu, kujiapiza kulinda mamlaka halali ya Dayosisi ya Konde.
Barua ya Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Konde, Mchungaji Ikupilika Mwakisimba ya Agosti 13 mwaka jana, kwenda kwa Mwakihaba, inataja makosa matano yaliyomfuta uchungaji na kumsimamisha kazi.