Maambukizi ya Fangasi katika Sehemu za Siri (Vaginal Candidiasis)

Frumence M Kyauke

JF-Expert Member
Aug 30, 2021
630
1,260
Kati ya maambukizi yanayowasumbua wanawake wengi duniani ni maambukizi ya fangasi. Inakisiwa asilimia 75 ya wanawake wote duniani hupata maambukizi haya katika kipindi cha uhai wao.

Maambukizi ya fangasi katika sehemu za siri za mwanamke husababishwa na uwepo wa fangasi wanaojulikana kitaalamu kama Candida albicans. Maambukizi haya pia hujulikana kama yeast infection au thrush. Fangasi hupatikana kama vimelea vya kawaida katika mdomo, mpira wa kupitisha chakula sehemu inayojulikana kama pharynx, katika kibofu cha mkojo, uume na hata kwenye uke.

Mfumo mzuri wa kinga wa mwili pamoja aina fulani za bakteria wanaoishi pamoja na fangasi hawa husaidia sana katika kuthibiti maambukizi yanayoyosababishwa na aina hi ya fangasi.

Nini hutokea?
Kwa kawaida, Candida albicans huishi kwenye uke na sehemu nyingine (kama zilivyoelezewa hapo juu) bila kusababisha madhara yoyote yale isipokuwa pale mazingira ya eneo husika yanapobadilika kama vile mabadiliko katika hali ya pH ya eneo husika (ifahamike ya kwamba pH ya kawaida ndani ya uke ni 4.0 - 4.5) au uwiano wake na vimelea (microorganisms) wengine unapoharibiwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile matumizi ya madawa aina ya antibiotics, kupungua kwa kinga mwilini kutokana na magonjwa mbalimbali n.k.

Maambukizi haya ya fangasi yanaweza kugawanywa katika sehemu kuu mbili
Maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi mara moja hadi nne kwa mwaka na dalili zake huwa si mbaya sana na maambukizi haya husababishwa na fangasi wa jamii hii ya Candida albicans.

Maambukizi makali yaani complicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi zaidi ya mara nne kwa mwaka, dalili zake kuwa mbaya zaidi au kama maambukizi yatakuwa yametokea kipindi cha ujauzito, ugonjwa wa kisukari, upungufu wa kinga mwilini. Aina hii kusababishwa na vimelea vya aina nyingine tofauti na Candida albicans.

Vihatarishi
Watu walio katika hatari ya kupata maambukizi ya fangasi hawa ni wale wenye

Kutumia sana dawa aina ya detergents kwenye sehemu za siri au douches (vifaa vinavyotumiwa kusafishia uke kwa kutumia maji yaliyochanganywa na siki au antiseptic yoyote ile) kwa sababu hali husababisha kuharibika kwa uwiano wa fangasi na aina nyingine ya vinyemelezi kama bakteria aina ya lactobacilli

Kutumia sana madawa aina ya antibiotics, steroids ambayo yana tabia ya kushusha kinga ya mwili

Mabadiliko ya mfumo wa homoni mwilini ambayo husababisha mabadiliko katika s ehemu za siri na hivyo kufanya kuwepo kwa ukuaji wa kasi wa fangasi hawa

Ujauzito (kutokana na kubadilika kwa mfumo wa homoni mwilini na kupungua kwa kinga ya mwili). Hata hivyo ieleweke hapa kuwa si kila mjamzito hupatwa na maambukizi haya.

Matumizi ya dawa za kupanga uzazi (vidonge vya majira)

Upungufu wa kinga mwilini kutokana na magonjwa sugu kama kisukari, saratani aina yoyote ile, ugonjwa aina ya mononucleosis na nk.

Ugonjwa wa ukimwi (HIV/AIDS)

Matibabu ya homoni (hormonal replacement therapy) kutokana na sababu mbalimbali

Matibabu ya kusaidia kushika mimba kwa wale wenye matatizo ya uzazi (infertility treatment)

Msongo wa mawazo (stress)

Utapia mlo (malnutrition)

Kuvaa nguo au mavazi yanayoleta joto sana sehemu za siri kwa muda mrefu kama nguo za kuogelea (swimwear), nguo za ndani (chupi) zilizotengenezwa kwa kitambaa aina ya nylon, nguo za ndani zinazobana sana nk.

Kujamiana kwa njia ya kawaida mara tu baada ya kujamiana kupitia njia ya haja kubwa (anal sex) au matumizi ya vilainishi venye glycerin wakati wa kujamiana pia yamehusishwa na maambukizi haya.
Wanawake wenye umri wa miaka kati ya ishirini na thelathini wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi haya wakati wale ambao wameshaacha kupata hedhi au wale ambao hawajaanza kupata hedhi kabisa hawako kwenye hatari kubwa.

Kwa wanaume vihatarishi vya maambukizi haya ni
Kujamiana na mwanamke mwenye tatizo hili au maambukizi haya

Upungufu wa kinga mwilini

Matumizi ya madawa aina ya antibiotics kwa muda mrefu bila ushauri wa daktari

Magonjwa sugu kama kisukari, saratani ya aina yoyote ile na nk.

Dalili na viashiria kwa wanawake

Kuwashwa sehemu za siri (kwenye tupu ya mwanamke)

Kuhisi kuwaka moto sehemu za siri (burning sensation)

Kufanya kama vidonda katika sehemu za siri (soreness)

Maumivu wakati wa kujamiana (superficial dyspareunia)

Maumivu au usumbufu wakati wa kujisaidia haja ndogo (wakati mtu anakojoa)

Kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwa mdomo wa nje wa tupu ya mwanamke (labia minora)

Kutokwa na uchafu wa rangi nyeupe au nyeupe kijivu, unaoweza kuwa mwepesi, majimaji au mzito na ambao umefanana na jibini (cottage cheese like discharge) wenye muonekano unaojulikana pia kama curd-like appearance. Kwa kawaida, uchafu huu haumbatani na harufu yoyote isipokuwa panapokuwa na tatizo la ziada kama ugonjwa wa zinaa aina ya Bacteria vaginosis. Uchafu huu unaotoka hapa unaweza kuenea kwenye maeneo mengine yaliyokaribu na tupu ya mwanamke kama kwenye mitoki (groin area) au perineum na kusababisha kuharibika kwa ngozi katika sehemu hizo.

Dalili na viashiria hivi huwa mbaya zaidi wakati mwanamke anapokaribia kupata hedhi.

Dalili na viashiria kwa wanaume ni
Kuwashwa sehemu za siri

Kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwenye ncha ya uume

Kuwepo kwa uchafu wa rangi nyeupe (kama nilivyoeleza hapo juu) kwenye sehemu ya juu ya uume.

Kuwa na vidonda vidogo kwenye uume (sore on the glans)

Hata hivyo, mara nyingi wanaume hawaoneshi dalili zozote zile, ni vizuri kwa mwanamke kumueleza mwenza wake pale anapopata maambukizi haya ili naye pia apate kutibiwa.

Vipimo vya uchunguzi
Kabla ya vipimo vya uchunguzi, ni muhimu kwa daktari kuchukua historia ya mgonjwa kwa usahihi kabisa. Vipimo vitahusisha:

Uchunguzi wa uke (per Vaginal Examination (PV exam)
Daktari huvaa gloves, na kuzilainisha gloves hizi kwa jelly maalum, mgonjwa hulala kwenye kitanda na kutanua miguu yake ili njia itanuke na kumrahisishia daktari kumfanyia uchunguzi, wakati akiwa tayari, daktari ataingiza vidole vyake viwili (cha shahada na cha kati) ukeni kwa dhumuni la

Kuhisi kama kuna uvimbe wowote ndani ya tupu ya mwanamke
Kuangalia kama anapata maumivu wakati wa kujamiana
Kuangalia kama kuna uchafu wowote unaotoka, wingi wake, rangi yake, harufu yake, uzito wake (mwepesi, majimaji au mzito), na aina ya uchafu unaotoka kama ni sahihi kutokana na maelezo ya mgonjwa au ni tofauti
Kuangalia kama sehemu ya siri ipo kawaida

Kuangalia kama kuna uvimbe wowote wa tezi za sehemu ya siri (mitoki)
Kuangalia nywele za sehemu za siri zilivyo na jinsi zilivyokaa
Kuangalia shingo ya kizazi, bartholin glands nk.
Kuangalia sehemu ya haja kubwa kama kuna skin tags, bawasiri (haemorrhoids) nk.
Kuangalia kwenye kinembe (clitoris) kama kuna tatizo lolote lile.
Hayo ni baadhi tu ya malengo na faida za kipimo hiki kwa vile humuwezesha daktari kugundua tatizo au maradhi mengine ya ziada ambayo hayajaanza bado kuonesha dalili zake kwa mgonjwa au mgonjwa mwenyewe hafahamu kama hali aliyo nayo ni tatizo. Hata hivyo inashauriwa sana kabla ya kufanya kipimo hiki, daktari amjulishe mgonjwa aina ya kipimo, lengo lake na jinsi kitakavyofanyika ili kumuandaa mgonjwa kisaikolojia. Aidha ni muhimu pia kumtaarifu wakati anapoanza kuingiza vidole.

Kuchunguza uchafu unaotoka kwa kutumia hadubini (microscope)
Mara tu baada ya kuchukua sehemu ya uchafu kwa kutumia swab, kipimo hicho humwagiwa tone la 10% potassium hydroxide ambayo huyeyusha chembechembe za ngozi na kubakisha seli za Candida albicans. Kuwepo kwa pseudohyphae (mfano wa aina fulani ya mizizi au miguu ya fangasi hawa) pamoja na budding yeast cells (yaani seli za fangasi zinazojigawa kwa ajili ya kuzaliana) ni uthibitisho wa maambukizi ya fangasi aina ya Candida albicans.

Kuchukua kipimo na kuotesha kwenye maabara
Ili kuangalia aina ya uoto huo kama ni wa fangasi aina ya Candida albicans, ama la.

Kipimo cha mkojo (Urinalysis)

Vipimo vingine hufanyika kulingana na dalili zinazoashiria uwepo wa magonjwa mengine kama vile ugonjwa wa kisukari, HIV/AIDS, ugonjwa wa kuvimba tezi la koo (goiter), saratani ya tezi koo (thyroid cancer) nk.

Matibabu
Matibabu ya fangasi huusisha dawa za kutibu fangasi (antifungal drugs) kama vile dawa za kupaka za topical Clotrimazole, topical Nystatin, Fluconazole au topical Ketoconazole.

Wagonjwa wenye maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated vaginal candidiasis wanaweza kutumia dawa za kupaka (cream) kutoka dawa za fangasi za jamii ya -azole kama vile Butoconozale, Miconazole, Clotricomazole nk. Dawa hizi hutumika kwa muda wa siku 3-7 kulingana na aina ya dawa. Mgonjwa anashauriwa kupaka dawa ndani ya uke pamoja na maeneo yote yanayozunguka sehemu hiyo. Jinsi ya kupaka dawa hizi ni kuanzia mbele kuelekea nyuma.

Aidha mgonjwa anaweza kupewa dawa za kutumbukiza ukeni ambayo atatumia kwa muda wa siku 3-14 kulingana na aina ya dawa. Dawa hizo ni pamoja na Miconazole, Tiaconazole, Terconazole, Nystatin nk.

Kidonge cha kumeza aina ya fluconzole pia huweza kutolewa. Dawa hizi nilizotaja hapa juu zina kawaida ya kuharibu ubora wa mipira ya kondomu zilizotengenezwa na mpira aina ya latex (latex condoms) pamoja na vifaa vya upangaji uzazi aina ya diaphragms.

Ni vizuri kwa daktari kabla ya kumpa mgonjwa dawa hizi kumfahamisha kwa ufasaha jinsi ya kuzitumia na tahadhari anayotakiwa mgonjwa kuchukua. Inashauriwa kama baada ya matumizi haya bado mgonjwa ana dalili za maambukizi au mgonjwa akapata tena maambukizi haya ndani ya miezi miwili baada ya matibabu ya awali, basi anashauriwa kwenda kumuona daktari ili apate matibabu zaidi.

Kwa wale wenye maambukizi makali yaani complicated vaginal candidiasis, kabla ya kupewa tiba, ni muhimu kwanza kufanyiwa kipimo cha kuotesha sehemu ya uchafu unaootoka ukeni ili kuwa na uhakika kama kweli fangasi wanaosababisha maambukizi haya ni Candida albicans ama la, kwani fangasi aina ya Candida glabrata pia wanaweza kusababisha aina ya maambukizi haya na huwa siyo rahisi kutibika kwa kutumia matibabu ya kawaida ya kutibu fangasi pamoja na pia si rahisi kuonekana kwa kutumia hadubini (microscope).

Matibabu ya wagonjwa wenye aina hii ya fangasi hujumuisha matumizi ya dawa za kupaka au vidonge vya kuweka ukeni kwa muda mrefu yaani kwa muda wa siku saba hadi kumi na nne (7-14) au dawa aina ya fluconazole ambayo hutumika kila baada ya siku tatu (yaani siku ya 1, siku ya 4 na siku ya 7).

Mara baada ya kumaliza tiba hii, mgonjwa hutakiwa kuendelea nayo mara moja kwa wiki kwa muda wa miezi sita. Ikiwa matibabu haya hayatasaidia basi mgonjwa anaweza kushauriwa kutumia mchanganyiko wa fluconazole pamoja na dawa ya kupaka ya Clotrimazole mara mbili au moja kwa wiki kulingana na dozi ya dawa, au fluconazole na dawa nyingine za kupaka kwa wakati mmoja.

Matibabu ya wagonjwa wenye maambukizi hatari sana yaani severe vaginal candidiasis ambayo kwa kawaida huambatana na dalili kama uke kuwa mwekundu sana, uke kuvimba, michubuko ya ngozi ya ukeni (excoriation) na kutokea kwa mifereji kama vidonda (fissure formation) huwa ni dawa zozote za kupaka zilizotajwa hapo juu kwa muda wa siku 7 mpaka 14 au dawa ya fluconazole ambayo hutolewa mara mbili, ambapo dozi ya pili hutolewa siku ya tatu baada ya kutolewa kwa dozi ya awali (second dose 72hrs after initial dose).

Matibabu ya maambukizi ya fangasi ambayo hayasababishwi na Candida albicans kwa mfano Candida glabrata nk ni matumizi ya dawa za kupaka jamii ya nonfluconazole azole groups kama vile Posaconazole, Voriconazole nk zitolewazo kwa muda wa siku 7 mpaka 14 pamoja na kidonge cha Boric acid kwa muda wa siku 14. Mtu mwenye maambukizi haya pia anashauriwa kuonana na daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama.

Kwa vile maambukizi ya fangasi hutokea sana kwa wanawake wajawazito, hivyo basi wanashauriwa kutibiwa kwa kutumia dawa za kupaka tu kwa muda wa siku 7.

Aidha dawa aina ya Itraconazole haipaswi kutumiwa na mwanamke mjazito au anayekusudia kushika mimba. Dawa ya Ketoconazole haipaswi kutolewa bila ushauri wa daktari kwani ina madhara ya kusababisha ugonjwa hatari wa Ini (Fulminant hepatitis). Usugu wa fangasi dhidi ya dawa za jamii ya azole groups hutokea baada ya matumizi ya dawa za vidonge (vya kumeza) za kutibu fangasi kwa muda mrefu.

Maambukizi ya fangasi pia huonekana sana kwa wagonjwa wenye Ukimwi. Tiba ya maambukizi haya ni sawa na tiba ya watu ambao hawana ugonjwa wa Ukimwi. Hata hivyo, kwa wale wagonjwa wa ukimwi ambao wamepata maambukizi ya fangasi mara kwa mara wanashauriwa kunywa dawa aina ya fluconzole mara moja kwa wiki kama kinga dhidi ya maambukizi haya au kama njia ya kupunguza fangasi hawa.

Kadhalika dawa za kutibu fangasi aina ya Itraconazole, Voriconazole, Posaconazole huingiliana sana katika utendaji kazi na dawa za kurefusha maisha za ugonjwa wa Ukimwi (Antiretroviral drugs, ARVs) aina ya Protease Inhibitors, PIs (rotinavir nk.) na Nonnucleoside Reverse Trancriptase Inhibitors, NNRTI (maraviroc nk).

Wakati mwingine, maambukizi ya fangasi yanaweza kuambatana na magonjwa ya zinaa (Bacterial vaginosis nk), hivyo dawa zitatolewa kulingana na dalili na historia ya mgonjwa.

Kinga ya maambukizi ya fangasi
Kuosha sehemu ya siri kwa kutumia kitambaa kisafi kila siku na kuosha kuanzia mbele kuelekea nyuma, epuka kurudia ukishafika nyuma.

Epuka matumizi ya sabuni zenye manukato, bubble baths, vaginal deodorant products, feminine hygiene, na bath powder.

Vaa chupi ambazo hazibani sana na zilizotengenezwa kwa kutumia pamba au hariri (silk), epuka synthetic underwear.

Epuka mavazi yoyote ya kubana kama jeans za kubana nk.

Badilisha nguo za ndani (chupi) kila zinapopata unyevunyevu.

Fua chupi zako kwa maji yenye nyuzi joto 90 na kuendelea.

Tumia pad wakati tu unapozihitaji (kama umeingia kwenye mzunguko wako wa hedhi)

Kula mlo wenye virutubisho vyote kamili (balanced diet)

Epuka kufanya mapenzi na mpenzi wako ambaye amepata maambukizi ya fangasi.

Epuka kuoga maji moto sana (hot baths) tumia maji ya uvuguvugu, hii kwa wale ambao wanaishi kwenye ukanda wa joto (tropical climate).

Matumizi ya vifaa vya ngono (sex toys), vifaa vya upangaji uzazi (diaphragms, cervical caps) yanaweza kuleta kujirudia kwa maambukizi ya fangasi kama havitaoshwa na kukaushwa vizuri baada ya kutumiwa.

Baadhi ya tafiti zilizofanyika, zimethibitisha ya kwamba unywaji wa maziwa ya mtindi (yoghurt) yenye live culture, husaidia kupunguza maambukizi ya fangasi.

images.jpeg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom