Ma-DC, ma-RC wapya msimuangushe Rais JPM

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
TAYARI Rais John Magufuli amewaapisha rasmi wakuu wa mikoa wapya aliowateua hivi karibuni na kuhakikisha wakuu wa wilaya wapya wanaapa kiapo cha uadilifu ikiwa ni ishara ya kuanza kuwatumikia wananchi.

Wakati wa viapo hivyo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Salome Kaganda wakiongozwa na Dk Magufuli, walipata wasaa wa kutoa wosia kwa wateule hao.

Jambo kubwa lililojitokeza katika wosia huo ni kwa viongozi hao kuchapakazi bila uoga, kupambana na vitendo vya rushwa, kusimamia shughuli za maendeleo katika maeneo yao ikiwemo mapato lakini pia kujiepusha na vitendo visivyo na uadilifu.

Rais Magufuli katika wosia wake, alibainisha wazi kuwa alikabiliwa na wakati mgumu katika mchakato mzima wa uteuzi wa ma- DC kutokana na wengi wao hasa wale waliokuwa madarakani kutokidhi vigezo alivyovihitaji.

Vigezo alivyoviainisha kuwa ni msingi wa utendaji kwa viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, ni pamoja na historia ya mtu mwenyewe, uwajibikaji na anayeendana na kasi ya Hapa Kazi Tu. Kwa msingi huo, mkuu huyo wa nchi aliweka wazi sababu zilizomfanya awaache takribani wakuu wa wilaya 100 waliokuwepo madarakani kuwa hawakutimiza vigezo hivyo ndio maana ameteua wakuu wapya 100.

Kwa maana hiyo hoja yake kubwa kwa viongozi ni kuhakikisha wanawajibika kwa wananchi kwa kufuata misingi ya sheria hasa kutokana na ukweli kuwa wao ndio wanaomuwakilisha katika wilaya mbalimbali nchini.

Pamoja na wosia huo wa Rais Magufuli na viongozi wenziwe wa Serikali, Jaji Kaganda aligusia zaidi suala la maadili na kutolea mfano uzoefu wake ambapo amepokea malalamiko mengi yanayohusu manyanyaso na uvunjifu wa maadili unaowahusu viongozi wa wilaya.

Alikemea ulevi kupita kiasi, matumizi mabaya ya madaraka na tatizo la viongozi wa umma kujihusisha na wanafunzi kwa kutumia vibaya madaraka yao na kusisitiza kuwa kiongozi yeyote wa umma ni lazima aweke mbele suala la maadili.

Ukweli ni kwamba, kupitia wosia na kiapo cha uadilifu ambao tayari viongozi hao wameapa ni wakati sasa kutekeleza kwa vitendo kile wanachotarajiwa kukifanya na Watanzania lakini pia na viongozi waliowachagua.

Ni kweli kuwa Watanzania wengi hasa vijijini pamoja na kuwepo kwa rasilimali za kutosha bado wanakabiliwa na lindi kubwa la umasikini hivyo wanahitaji viongozi wabunifu, wachapakazi na wenye muono wa mbali ili kuwakwamua kutoka kwenye kadhia hiyo.

Licha ya umasikini pia zipo changamoto mbalimbali kama vile matatizo ya ardhi, migogoro baina ya wakulima na wafugaji, miundombinu mibovu na ukosefu wa huduma muhimu kama vile maji, umeme, elimu na afya.

Kutokana na wosia waliopewa na hali halisi ya uteuzi ilivyoainishwa na Rais Magufuli, ni funzo tosha kwa ma-DC, ma-RC na viongozi wengine wa umma kuwa, katika Serikali hii ya Awamu ya Tano uwajibikaji, uchapakazi, uadilifu na kujali maslahi ya wananchi ndio msingi mkuu wa uongozi.

Wananchi wanatarajia kuona mabadiliko katika maeneo yao kutokana na ukweli kuwa, uteuzi huo umezingatia mchanganyiko chanya wa viongozi wakiwemo vijana, wenye uzoefu katika eneo la ukuu wa wilaya na wasomi wa kada mbalimbali.

Kama alivyoomba Rais Magufuli kuwa msimuangushe, na ili kutekeleza ombi hilo, hakikisheni mnatekeleza kwa vitendo wajibu wenu na yale yote yaliyomo kwenye Ilani ya CCM, bila kujali, dhihaka, masimango na vikwazo mtakavyokumbana navyo kutokana na ukweli kuwa hakuna kazi isiyo na changamoto.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…