Rubawa
JF-Expert Member
- Dec 25, 2015
- 2,055
- 3,246
NA MOHAMMED ABDULRAHMAN
Suala la Libya bado limetugawa wengi. Tukijiuliza nini suluhisho, nini mustakbali wa taifa hili.
Majuma machache Yaliopita, viongozi wa karibu nchi 12 na Wakuu wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika waliungana na mwenyeji wao Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwa mkutano mjini Berlin, ulioitishwa kuijadili hali nchini Libya.
Lengo la mkutano huo wa siku moja lilikuwa ni kutafuta njia za kumaliza vita katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini. Mkutano huo wa siku moja katika mji mkuu wa Ujerumani ulimalizika kwa viongozi walioshiriki baadhi wakiwa wahusika wa moja kwa moja, kuzitaka pande zinazohusika nchini Libya, zisitishe uhasama na kuheshimu usimamishaji mapigano na mataifa ya kigeni yasijiingize kijeshi wala kuwasaidia kwa silaha wale wanaowaunga mkono.
Kwa maana hiyo kuunga mkono upnde mmoja au mengine kati ya serikali inayoelezwa kuwa inatambuliwa kimataifa ya Waziri mkuu Fayez Al Sarraj yenye makao yake mjini Tripoli na Jemedari Khalifa Haftar ambaye anaungwa mkono na serikali hasimu yenye makao yake makuu mashariki mwa Libya, akiwa na makao makuu nje ya mji wa Benghazi kulikoanzia vuguvugu la upinzani dhidi ya utawala wa Gaddafi na hatimaye kungolewa na kuuwawa 2011.
Ufaransa, Urusi, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu ni miongoni mwa mataifa yanayomuunga mkono Haftar na Uturuki inaiunga mkono serikali ya al Sarraj ikiwa imetuma wanajeshi kuinusuru isianguke kutokana na mashambulizi ya Haftar yalioanza Aprili mwaka jana kujaribu kuuteka mji mkuu Tripoli.
Rais Erdogan ameonya pia kwamba kuna hatari kuendelea mgogoro huo kunaweza kukazaa tatizo jengine kubwa litakaloitikiza Ulaya na mataifa mengine, nalo ni kuibuka makundi ya kigaidi ya Waislamu wa siasa kali kama Dola la Kiislamu-ISIS na Al-Qaida.
Mengine katika mpango huo uliofafanuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyehudhuria mkutano huo, ni kuheshimiwa kikamilifu sharia zinazolinda usalama wa binadamu na haki za binadamu na kusitishwa mtindo wa watu kamatwa kamatwa hovyo pamoja na kuvifunga vituo vyote vinavyotumiwa kuwazuwia wahamiaji na wataotafuta hifadhi ya ukimbizi.
Kuhusu uchumi, taarifa yao ikaelezea juu ya umuhimu wa kurejeshwa na kulindwa uhuru wa taasisi za dola na hasa Benki kuu ya Libya na Kampuni ya mafuta ya taifa, usalama wa sekta ya mafuta na matumizi kinyume cha sharia ya nyenzo zote za nishati.
Kama illivyokuwa Moscow Haftar na Sarraj pia hawakukutana ana kwa ana mjini Berlin , lakini Guterres alisema wamekubaliana kila mmoja wao ateuwe waakilishi watano watakaohudhuria mazungumzo yatakayofuata mjini Geneva.
Mkutano wa Berlin uliitishwa wiki moja baadaya mazungumzo ya Moscow Januari 13, chini ya udhamini wa mwenyeji Rais Vladimir Putin wa Urusi na Tayep Recip Erdogan wa Uturuki lakini yakashindwa kupata makubaliano, pale Haftar alipokataa kusaini waraka wa kusitisha mapigano.
Msimamo wake ulimkasirisha Erdogan aliyekwenda umbali wa kumuonya kwamba ikiwa ataendelea kuushambulia mji wa Tripoli, basi atamuonesha cha mtemakuni.
Haftar alikuwa mshirika wa Gaddafi akiwa mwanachama wa kikundi cha maafisa vijana waliompindua Mfalme Muhammad Idris 1969, kabla ya kukorofishana baadaye na Haftar akakimbilia Marekani.
Nilikuwa nikiyafuatilia matokeo ya mkutano wa Berlin na kuanza kuyatafakari hayo yote kama sehemu ya mpango uliokubaliwa na nikajikuta nikizongwa na maswali kadha wa kadhaa akilini.
Nianze na wito wa kusimamishwa mapigano na mataifa ya kigeni kuacha kuzipa silaha pande zinazopigana. Hapa ninajiuliza ikiwa kweli mataifa hayo yatakuwa na dhamira ya dhati kufanya hivyo.
Mgogoro wa Libya umekuwa mpana zaidi na idadi ya wahusika imeongezeka. Rais Erdogan wa Uturuki na Vladimir Putin Urusi ni washirika katika vita nchini Syria wakimuunga mkono Rais Bashar al- Assad, lakini wametengana panapohusika na Libya.
Ukiziweka kando Ufaransa na Marekani kuna Italia ambayo msimamo wake hauko wazi. Nchi zote zina maslahi yao ya kiuchumi na kisiasa katika Libya.
Upande wa kiuchumi ni utajiri mkubwa wa mafuta na gesi ya nchi hiyo unaogombewa. Kwa hiyo haikushangaza kuona siku chache kabla ya kuelekea Berlin, Haftar aliyafunga maeneo matano ya mafuta na hili ni pigo na kusababisha hali ngumu kwa wakaazi wa maeneo ya magharibi mwa Libya.
Kampuni ya mafuta ya taifa ilisema hatua hiyo iliathiri asilimia 50 ya uchimbaji mafuta kwa jumla, ikizingatiwa majeshi ya Jemedari Haftar yanadhibiti karibu theluthi mbili ya ardhi ya nchi hiyo.
Pili, hali inayoendelea Libya kwa upande mwengine imegeuka mtihani mgumu kwa nchi za Ulaya. Tatizo la wakimbizi limezitia msukosuko nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya zikikumbwa na kuzidi kwa hisia za upinzani miongoni mwa raia na ndio maana Ujerumani imechukua nafasi ya usoni kuandaa mkutano huo.
Wengi miongoni mwa raia katika nchi Ulaya wanahisi wakimbizi wanasababisha kuporomoka kwa tija zao za kijamii na kusababisha ukosefu wa ajira.
Hayo yamezusha chuki na ubaguzi na kuongezeka kwa uungaji mkono kwa vyama vya siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia, vinavyoitumia hali hiyo.
Miongoni mwa nchi zilizoathirika ni Ujerumani ambako chama cha Alternative für Deutschland-AFD (mbadala kwa Ujerumani ) sasa ni chama kikuu cha Upinzani ndani ya bunge la Shirikisho Bundestag.
Nina wasiwasi kama Ufaransa, Uingereza, na Marekani kweli ni mataifa yakutegemewa kuleta amani katika taifa hilo la Afrika kaskazini. Nchi hizo tatu ndizo zilizosaidia kuuwasha moto kama sio chanzo cha janga linaloikumba Libya.
Ndizo zilizowaunga mkono waasi kuuangusha utawala wa Muammar Gaddafi na kukiuka azimio la Umoja wa mataifa. Waliouwacha moto wanaweza kugeuka wazima moto, lakini kwa wakati huu hailekei kuwa ni jambo rahisi.
Kwa mtazamo wa kiadilifu, wakutafuta suluhisho wangekuwa zaidi wale ambao si sehemu ya mgogoro, kwasababu kwa vyovyote itakavyokuwa masilahi ya wahusika pamoja na ahadi walizotoa bado yapo palepale.
Ninakubaliana na wadadisi wenye shaka shaka. Itakumbukwa tayari kulifanyika mkutano kuhusu Libya mjini Paris Ufaransa na Palermo Italia, na pakatolewa ahadi ya kuimarisha vikwazo vya silaha, ili kudumisha Umoja wa kitaifa na paachwe mtindo wa kutumia silaha kwa manufaa ya kisiasa.
Lakini hayakuheshimiwa. Kiroja cha mambo mkutano wa Berlin uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ujerumani na Umoja wa Mataifa, na Ufaransa moja wapo ya nchi ziliomo katika mkasa huo wa silaha ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja huo.
Halikadhalika wakati Umoja huo unaitambua serikali mjini Tripoli kuwa serikali halali, Ufaransa inamuunga mkono Jemedari Haftar.
Utata mwengine panapohusika na matumaini ya kupata suluhisho, ni kutengwa kwa nchi jirani katika mazungumzo ya Berlin. Libya inapakana na karibu na nchi saba. Algeria, Chad, Misri, Morocco Niger, Sudan na Tunisia.
Lakini ni Misri na Algeria pekee zilizoalikwa. Halikadhalika kuwepo kwa Rais Denis Sassou Nguesso kuliwashangaza wengi, kwani sio tu Jamhuri ya Congo ambayo kijiografia iko Afrika kati iko mbali , lakini haipakani na Libya na wala kiongozi wake si miongoni mwa wenye uzito hivyo katika siasa za Afrika au Kimataifa.
Zaidi ya hayo Umoja wa Afrika uliwakilishwa na Rais wa Halmashauri Kuu Moussa Faki Mahmat. Siku chache baadaye likafahamika kwanini Nguesso alikuweko Berlin.
Kamati yake ya ngazi ya juu ya Umoja wa Afrika kuhusu Libya ilioundwa 2011 ilitakutana katika mji mkuu wa Congo-Brazzaville, tarehe 30 iliopita kutathmini hali nchini Libya kabla ya mkutano wa kilele wa wa Viongozi wakuu wa taifa na serikali wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia mwezi huu wa Februari.
Rais Nguesso ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo ni miongoni mwa viongozi wa mkoloni ya zamani ya Ufaransa mwenye uhusiano wa karibu sana na dola hilo.
Jeeni sadfa tu kwamba kikao cha Brazzaville kitafuatia yaliomuliwa na Wakubwa (mataifa ya kigeni) mjini Berlin? Baadhi ya viongozi wa Afrika wameanza kuiona hatari ya Libya kushindwa kupata suluhisho la haraka.
Wiki iliopita Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliyekuweko mjini London kuhudhuria Mkutano wa kilele kati ya Uingereza na Afrika alisema katika mahojiano na mwandishi wa BBC, kwamba lilikuwa kosa kubwa kwa Afrika kushindwa kuilinda Libya.
Alisema bara hilo lilikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya hivyo lakini likagawika na kuyalaumu mataifa ya kigeni kwa kusababisha janga linaloendelea hadi leo.
Amani ni muhimu na Libya inahitaji usalama na utulivu, lakini sidhani ikiwa yaliofikiwa mjini Berlin yanatia moyo kuwa ndio ufunguo wa kupatikana suluhisho. Bado kuna utata, giza lingali limetanda nchini Libya.
Sent using Jamii Forums mobile app