Na Mwandishi Wetu,Arusha
MFANYABIASHARA mkubwa wa Utalii nchini na mmiliki wa kampuni ya utalii ya Leopard Tours, Zuher Fazal amejitokeza na kuweka hadharani nyaraka mbalimbali zinazohalalisha umiliki wake wa kiwanja kilichopo katika eneo la Kijenge mkabala na shule ya msingi Kijenge ya jijini Arusha .
Kutolewa kwa nyaraka hizo za wizara ya Ardhi sasa kunaondoa tuhuma zilizokuwa zimeelekezwa kwenye Halmashauri ya jiji la Arusha kuwa Halmashauri hiyo kupitia kwa maafisa ardhi kwa kushirikiana na mfanyabiashara huyo walimega eneo la shule kinyemela.
Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Fazal alisema asingeweza kununua eneo hilo kama lingekuwa ni mali ya shule hiyo kwa kuwa anaelewa maana ya elimu na kwamba yeye ni mmoja wawalezi wa shule hiyo.
Fazali ambaye ni mkurugenzi na mmiliki wa kampuni kubwa ya utalii nchini ya Leopard Tours alisema kuwa eneo hilo lilikuwa na umiliki wa ardhi tangu mwaka 1974 kwa mtu binafsi na halijawahi kuwa la shule.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa yeye siyo mmiliki wa kwanza wa eneo hilo na alilikuta tayari lina umiliki wa mtu mwengine ambaye ndiye aliyemuuzia hivyo eneo hilo haliwezi kuwa mali ya shule.
"Eneo hili linazungumziwa sana kwenye vyombo vya habari kwamba ni la shule ukweli ni kwamba namiliki kihalali na mipaka yake na shule inapakana na lilitolewa mwaka 1974 kama ramani inavyoonyesha chukueni hii ramani muweke mambo wazi," alisema Fazali.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kijenge Elihaki Mzava alifafanua kwamba eneo la mipaka ya shule imepakana na majeego ya Leopard Tours na hayajaingia kwenye eneo shule.
Ingawa Mzava alikiri kuwepo kwa mgogoro wa mipaka upande wa kaskazini wa shule hiyo na hoteli maarufu ya 40/40 alisema kuwa Leopard Tours ambaye pia ni mlezi wa shule hiyo hajaingilia popote kwenye eneo la shule hiyo zaidi ya kuweka Jenereta.
"Sasa hivi tunapambana kuhakikisha eneo la kaskazini linawekwa mipaka na wavamizi wote tutahakikisha wanaondoka kwenye eneo hilo la shule ambako ndipo zilipo nyumba za walimu," alisema Mzava.
Meya wa Jiji la Arusha Calist Lazaro akizungumzia suala hilo alisema kuwa Jiji linafahamu mipaka ya shule ya msingi Kijenge na eneo zima linalizunguka eneo hilo na wanafahamu mgogoro wa shule hiyo na eneo kaskazini lililopo eneo la hotel ya 40/40.
Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari vilinukuliwa vikidai mmiliki huyo wa Leopard Tours alidaiwa kupewa eneo la shule kinyemela na halmshauri ya jii la Arusha.
ends.