Habari zenu wakuu,
Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, gwiji wa muziki wa Dansi nchini Tanzania, Shaaban Ally Mhoja Kishiwa maarufu kama Tx Moshi William alitutoka ghafla na kuacha pengo kubwa katika bendi yake ya Msondo Ngoma na Muziki wa dansi kwa ujumla.
Tangu kifo chake miaka 10 iliyopita, Muziki wa dansi umeshuka sana kama si kupotea kwenye ramani na huku bendi yake ya Msondo ngoma ikifa kimya kimya hii yote ni kudhihirisha pengo lake aliloacha ni kubwa sana.
Unamkumbuka vipi Tx Moshi William katika miaka hii 10 ya kifo chake?
Lakini kuna simulizi yenye mchanganyiko wa simanzi na burudani, akaonekana kwake katika anga za muziki kitaifa, akiwa mkazi wa Jiji la Dar es Salaam, Keko Machungwa, alikoanzia maisha hadi kifo.
Kwa vipi? Kuna simulizi zinazoeleza kuwa siku moja majira ya jioni akiwa na rafiki yake huko kwao, Hale mkoani Tanga katika matembezi yao ya jioni rafiki yake huyo alichokozwa na mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ‘mlevi’, akaamua kumpiga. Kwa bahati mbaya yule ‘mlevi’ alifariki dunia.
Moshi na rafiki yake, kila mmoja alitimka kivyake usiku huo na hapo ndipo ukawa mwanzo wa Moshi kuhamia Dar es Salaam kuanza maisha mapya, pia kuachana na jina la Shabani Ally Mhoja Kishiwa na kuwa Moshi William.