Nimekuwa Mbunge kipindi cha pili sasa ,nimeona Wabunge wakidhalilishwa kwa njia mbali mbali nje na ndani ya Bunge nimeona Wabunge wakina mama wakichaniwa nguo na askari ndani ya Bunge, nimeona Wabunge wakipewa kesi za uzushi na uongo. Nimeona Uchaguzi ukiporwa kwa nguvu na mabavu, nimeona Mawaziri watuhumiwa na wahalifu wa fedha za umma wakilindwa na Bunge na wengine wakishika nafasi mbali mbali za Serikali na Bunge.
Ndio maana ninasema, je Bunge lililokosa heshima na haki, linaweza kutegemea vitendo tofauti na vilivyo tokea kwa Kitwanga? Vyombo vya habari na watu mbali mbali wamesifu kwa njia tofauti uamuzi huu uliochukuliwa na Rais lakini Mimi nauliza maswali yafuatayo: Ni wakati gani Rais alipaswa kuchukua hatua dhidi ya Mh Charles Kitwanga?
- Je , ni wakati Kambi Rasmi ya Upinzani ilipotoa Maoni yake kwa Wizara ya Mambo ya Ndani juu ya Kitwanga na Infosys na Jeshi la Polisi au ni wakati au Kitwanga alipoingia akiwa amelewa? Je, wakati gani ulikuwa na masilahi kwa Taifa?
- Ni wakati gani Rais alipaswa kuonyesha ujasiri wake ,je ni wakati Mh Andrew Chenge anachaguliwa kuwa Kiongozi ndani ya Bunge wakati ana historia ngumu ya matumizi mabaya ya ofisi alipokuwa Mwanasheria Mkuu au ni wakati Kitwanga ameingia akiwa amelewa Bungeni?
Tabia hii ya Kitwanga haikubaliki na haipaswi kuungwa mkono, lakini nitakishangaa Chama cha Mapinduzi (CCM) , Rais Dr Magufuli amesema ametengeua uteuzi wa Kitwanga kwa kwa sababu ya ulevi ndani ya Bunge. Je, Wananchi wa Misungwi wasubiri maamuzi gani ya Chama juu ya jambo hili ambalo limeidhalilisha Serikali na Chama chao? Ni muhimu sasa Kamati kuu ya CCM ikakutana ili kuwapa faraja na matumaini Wananchi wa Misungwi kuwa Chama chao hakiwezi tena kuvumilia Misungwi ikaongozwa na mlevi, maana yake Kitwanga avuliwe Uanachama na Uchaguzi wa mdogo uitishwe mara moja.
Mwisho, Ujasiri huu wa Magufuli huonekane sasa katika mambo makubwa ya msingi katika Taifa letu kwa mfano , haki na amani ya Siasa za Zanzibar , Mfumo wa Tume huru ya Uchaguzi, Uhuru wa Bunge kuonekana na vile vile kurudisha matumaini ya Wananchi kwa kuwapa Katiba mpya ya maoni yao waliyoyatoa. Vinginevyo, tusipokuwa makini tunaweza kufikiri na kuambiwa kuwa bwawa la kuogelea (Swimming Pool ) ni bahari .
TAADHARI: Ninaomba kuufahamisha Umma kuwa sina akaunti yoyote kwenye mitandao ya kijamii kama Twitter, Facebook na kwingineko. Watu wote wanaotumia jina langu wajue wanatenda kosa la jinai.
Godbless Lema (MB)