Kuna dhana isemayo, mtoto wa mjini lazima awe ni mjanja ambaye anazijua fitina zote za kimaisha vinginevyo anaweza kujikuta anakimbia mji kwa sababu ya kukosa mbinu na ujanja wa kumwezesha kuendesha maisha.
Kwa Watanzania wengi Jakata Kikwete ni Rais aliyekuwa dhaifu na hii ilikuja kwa sababu aliamini katika dhana ya mihimili ya dola bila kuelewa kuwa mihimili yetu ya dola ni dhaifu na katika udhaifu huo wajanja watajinufaisha huku rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma na uzembe vikitamalaki na lawama nyingi atazibeba yeye kama Rais wa Tanzania.
Kwa wanaCCM, Jakaya Kikwete lazima wamuenzi kwa sababu amewawekea mazingira ya kisiasa ambayo yanafanya kazi zao kuwa rahisi bila wengi ndani ya CCM kutambua mantiki yake.
Wakati akiongoza kikao cha mwisho cha Kamati Kuu kama Mwenyekiti wa CCM Taifa alisema.’’Kuna watu walidhani CCM ingekufa na walishajiandaa na salamu za rambirambi bila kujua kama CCM iko palepale na wale walidhani wangeibuka hawakuibuka na hawataibuka’’.
Maneno ya Rais Jakaya Kikwete unaweza kuyapuuza lakini kwa mtu mwenye fikra pana akiyachambua atagundua umuhimu wake katika mstakabali wa siasa za Tanzania.
Rais Jakaya Kikwete alitumia dhana ya wahenga isemayo, ‘’mchawi mpe mwanao akulelee’’ ili kuhakikisha CCM inaendelea kuishi kwa miaka mingi ijayo.
Rais Kikwete aliwapa wapinzani wana wa CCM ili wawalee bila wao kujitambua. Kwa sasa wapinzani hawawezi tena kuleta madhara makubwa kwa CCM kama wataendelea kuwalea watoto wa CCM ambao kwa sasa wanajiimarisha zaidi ndani ya wapinzani.
Bila wana wa CCM kulelewa na wapinzani, suala la Ufisadi na Katiba Mpya yenye tume huru ya Uchaguzi lingeisumbua sana CCM.
Kwa kulitambua hilo, Rais Kikwete aliwateuwa kwenye Mchakato wa Katiba Mpya wana wa CCM kama kina Kingunge Ngombale–Mwiru aliyewakilisha kundi la waganga wa kienyeji/jadi na genge lake kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba Mpya ili Watanzania wawafahamu vizuri kifikra kuhusu mitazamo yao kwenye suala la Katiba ya Tanzania. Tuliona jinsi ambavyo walipambana kuhakikisha Katiba mpya yenye maudhui mengi ya Rasimu ya Warioba haipati nafasi.
Kingunge na genge lake linaloongozwa na Lowassa kwa sasa ndio nembo ya wapinzani kuhusu Katiba Mpya na Tume huru ya Uchaguzi. Nani mwenye akili timamu na fikra pana atawaamini kwa kile wanachokisema kwa sasa wakati Katiba ambayo wameitunga inasubiri kura za maoni.
Kwenye ufisadi, Rais Kikwete alitengeneza mazingira ili kuhakikisha watoto wa CCM wanaonyoshewa vidole kama mafisadi anawapeleka kwa wapinzani ili wakawalee na kwa kufanya hivyo, hoja ya ufisadi itakuwa sio tatizo kubwa ndani ya CCM. Leo hii wapinzani wanaogopa hata kutamka neno ufisadi.
Wapinzani kwa sasa wamebaki na hoja ya udikteta bila kuelewa kuwa hoja ya udikteta haijawahi kuwa ni tatizo katika siasa za Tanzania kwa sababu mpaka sasa watanzania wengi wanataka Tanzania yenye misingi ya utawala wa Mwl. Nyerere ambaye alikuwa ni dikteta kweli kweli. Ikubukwe wakati wa utawala wake haki za binadamu kama freedom of expression na haki ya kuwa hai hazikutambuliwa kikatiba. Mabadiliko ya tano yanayohusu tamko la haki za binadamu kwenye Katiba ya nchi yaliingizwa mwaka 1984, miezi michache kabla ya Mwl. Nyerere kung’atuka kwenye kiti cha Rais wa Tanzania. Utawala wa Mwl. Nyerere ulisababisha baadhi ya watu kuwekwa kizuizini huku wengine wakikimbilia uhamishoni bila kupenda.
Kama Jakaya Kikwete angekuwa sio mtoto wa ‘’mjini’’ kwenye siasa za Tanzania, kwa sasa ninaamini CCM ingekuwa marehemu lakini badala yake, kwa sasa vyama vya upinzani havina ajenda kamili ya kuviingiza Ikulu.