Nyendo
JF-Expert Member
- Jun 4, 2017
- 1,330
- 4,692
Tanzania ni moja ya nchi barani Afrika ambazo uchumi unakua kwa kasi. Toka mwaka 2017 kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni 7%.
Moja ya chachu ya kasi hiyo ni biashara ndogondogo ambazo kwa kiasi kikubwa zinamilikiwa na wanawake.
Takwimu za usawa wa kijinsia katika ajira zinaonyesha kwamba kufikia mwaka wa 2014 Watanzania milioni 2.1 walikuwa wameajiriwa katika sekta rasmi , ikiwa ni pamoja na serekalini na sekta binafsi, kwa mujibu wa kituo cha taifa cha takwimu nchini humo.
Hatahivyo takwimu rasmi za serikali zinaonyesha pia kwamba zaidi ya 60% ya wanawake walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 24 yaani milioni 13.9 wanajishughulisha na shughuli zisizo rasmi yaani biashara ndogondogo na kilimo.
Hii maana yake ni kwamba ni asilimia 0.75 tu ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi ndio wapo katika sekta rasmi. Kwa maneno mengine, idadi kubwa ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi nchini Tanzania ni wajasiriamali.
Licha ya kuwa na idadi kubwa ya wanawake wenye ujasiri wa kubuni na kuendesha biashara, kasi ya ukuaji wa mitaji yao bado ni finyu.
Chanzo kikuu cha mitaji karibuni duniani kote ni mikopo rasmi ya kibiashara. Hata hivyo, tafiti zinaonesha kuwa wanawake wengi wajasiriamali kutoka nchi zinazoinukia ikiwemo Tanzania hawana mikopo kutoka benki na taasisi rasmi za kifedha.
Kwa miaka mingi, dhana iliyoaminika ni kuwa wanawake wengi hawapati mikopo sababu pesa hazitoshi, lakini takwimu zinapingana na dhana hiyo.
Utafiti uliochapishwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2014 unaonesha kuwa zaidi ya 80% ya maombi ya mikopo ilitengwa kwa ajili ya wajasiriamali wanawake na 90% iliiva kwa ajili ya kutolewa. Hatahivyo, ni 18% ya wanawake wajasiriamali ambao waliomba mikopo benki na 28% waliomba mikopo katika taasisi nyenginezo za kifedha.
Takwimu hizo zinaashiria kuwa tatizo si uwepo wa fedha za mikopo bali utayari wa wanawake wajasiriamali kukopa.
Moja ya wataalamu waliondaa utafiti huo Vanessa Naegels hivi karibuni ameandika katika jarida la The Conversation kuwa, utayari wa wanawake kuomba mikopo unaathiriwa na mambo makuu mawili, dhana hasi juu ya mikopo rasmi ya kifedha na kukatishwa tamaa.
Kutokuwa na imani (dhana hasi)
Kwamujibu wa utafiti huo, wanawake wengi wamebainisha kuwa hawaamini kuwa wanabaguliwa na maafisa mikopo kwenye taasisi za kifedha.
Kilio cha waliowengi ni masharti yanayoambatana na mikopo hiyo ambayo yanakuwa kikwazo kwao. Sharti la kwanza lililolalamikiwa ni viwango vikubwa vya riba vinavyotozwa na mabenki kufikia 20% mpaka 30% kwa mwaka.
Wanawake hao pia wametaja kama dhamana ya mali kuwa ni kikwazo, wengi wao hawana mali kama nyumba au ardhi za kuweka rehani ili wapate mikopo.
Kwa wale ambao wenye mali hizo ni waume wamesema wenza wao hawawezi kuwapa ruhusa ya kuziweka rehani.
Kuna ambao wanamali zinazofaa kuwekwa rehani, lakini wamesema hawawezi kuzikopea wakiogopa kuzipoteza pale watakaposhindwa kulipa madeni yao.
Baadhi ya wajasiriamali wamelalamikia mchakato ni mrefu na wenye gharama. Kuna ambao wamelalamikia tabia za baadhi ya maafisa mikopo wakisema kuna ambao huwatongoza na kutaka wawape rushwa ya ngono ili wawasaidie.
Kutokuwa na ufahamu mzuri wa masuala ya kifedha na mikopo pia umetajwa kuwa ni kikwazo, wajasiriamali wengi wanawake wamesema hawakuwa wakijuwa kuwa wanapochelewa kulipa mikopo yao gharama za malipo huongezeka ama benki wana uwezo wa kuuza mali zao pale watakaposhindwa kulipa madeni kwa wakati.
Maumivu ya mikopo
Utafiti umeonesha kuwa kuna machungu ya aina mbili, ya moja kwa moja na ya kusikia kwa wengine. Hali zote mbili hizo zinachangia wanawake wajasiriamali kutoomba mikopo.
Baadhi ya wanawake waliohojiwa kwenye utafiti huo wamesema walishaomba mikopo huko nyuma na kukataliwa, wengine walipitia mashaka tele kwenye kulipa madeni yao na wengine kuombwa rushwa. Baadhi yao wamepata matatizo hayo kwenye mikopo isiyorasmi hali iliyopelekea kuwa na dhana hasi mpaka kwenye utayari wao kwenye kuomba mikopo rasmi.
Kwa kiasi kikubwa kuna ambao wamesikia habari za ugumu wa kupata na kurejesha mikopo kutoka kwa watu wengine ima wajasiriamali wenzao au habari zilizozagaa kwenye jamii.
Simulizi hizo huwafanya baadhi kutojaribu kabisa kuomba mikopo. Kuna ambao wanaamini wakiwa na mikopo watakosa uhuru wa kutumia pesa zao kwa namna wanavyoona inafaa.
Nini kifanyike
Ni dhahiri kulingana na utafiti wa ILO kuwa si kweli kuwa wanawake wajasiriamali waliowengi hawapati mikopo sababu ya ufinyu wa pesa.
Tatizo si pesa, bali dhana hasi zilizoota mizizi mirefu juu ya mikopo ya kibiashara. Ili kujenga utayari wa wajsairiamali wanawake kukopa dhana hizo potofu inabidi ziondoshwe, lakini haitakuwa kazi nyepesi.
Kwamujibu wa watafiti, njia bora zaidi na yenye tija ni kutoa elimu mahususi ya masuala ya kifedha kwa wanawake wajasiriamali. Ni kupitia elimu pekee wajasiriamali wanawake wanaweza kutunza hesabu zao na kulinda mitaji yao na kuikuza kwa kupitia mikopo rasmi.
Chanzo: BBC