"Marekani kutoa sheria inayolenga kuziadhibu nchi za Afrika ‘zinazofungamana’ na Russia." Hiki ni kichwa cha makala moja iliyochapishwa hivi karibuni katika gazeti la Nigeria Premium Times. Wakati huohuo, Gazeti la Daily Maverick nchini Afrika Kusini pia lilionya kuwa sheria hiyo inaweza kuliingiza "bara la Afrika katika msukosuko".
Mwezi Aprili Bunge la Marekani lilifanya mjadala kuhusu mswada wa sheria uitwao eti "kukabiliana na ushawishi na shughuli mbaya za Russia na mawakala wake barani Afrika", ambayo imetajwa katika makala za magazeti hayo mawili. Mswada huo wa sheria uliopendekezwa na mwakilishi wa Marekani chama cha Republican Bw. Gregory Meeks, unaruhusu Bunge la Marekani kutathmini maeneo ya ushawishi wa Russia barani Afrika, na kuchunguza kile inachoita usambazaji wa habari potovu na shughuli za kijeshi. Tarehe 27, Aprili Baraza la Wawakilishi la Marekani lilipitisha pendekezo hilo kwa kura 415 za ndio dhidi ya 9 za hapana.
Hali halisi ni kuwa kabla ya Bw. Meeks kupendekeza mswada huo, baadhi ya wanasiasa wa Marekani walikuwa tayari wanafikiria kulipiza kisasi dhidi ya nchi za Afrika ambazo zilikataa kuchagua upande katika mgogoro kati ya Russia na Ukraine. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Bibi Linda Thomas-Greenfield, aliwahi kusema, "Lazima tufanye juhudi zaidi ili kuzisaidia nchi hizi (za Afrika) kuelewa athari za uvamizi wa Russia nchini Ukraine." Uchambuzi unasema kauli ya Bibi Greenfield inaashiria kuwa viongozi wa Afrika wanahitaji kupewa ‘elimu’ na Marekani wanapofanya maamuzi ndani ya mamlaka zao.
"Elimu" hiyo ya Marekani sio ya kusema tu, hivi sasa nchi nyingi za Afrika tayari zimetishiwa kihalisia kutokana na mgogoro huo. Habari zinasema Marekani inataka uchunguzi juu ya serikali na maofisa wa nchi za Afrika ili kuona kama wanarahisisha malipo au shughuli nyingine zinazopigwa marufuku kwa mashirika na watu binafsi wa Russia waliowekwa vikwazo na Marekani, jambo ambalo litapelekea moja kwa moja nchi nyingi maskini za Afrika zinazotegemea mafuta kutoka Russia kukabiliana na vikwazo vya Marekani.
“Wazo la Vita Baridi" linalozidi kuwa kali la Marekani limetia wasiwasi wadau mbalimbali wa Afrika. Mchambuzi wa mambo ya siasa wa Afrika Kusini Nontobeko Hlela hivi karibuni aliandika kwenye jukwaa la kijamii la Kenya Elephant kwamba ingawa "(Afrika) imetengwa kimfumo katika maamuzi yoyote ya Marekani," lakini Marekani "inatarajia kuishawishi Afrika kujiunga katika kundi lake." Nao Zainab Usman na Katie Auth watafiti waandamizi katika Mpango wa Afrika katika Mfuko wa Carnegie kwa Amani ya Kimataifa wamesema kwa uwazi zaidi, "kwa miongo kadhaa, Marekani na washirika wake wameshirikiana na nchi za Afrika tu katika ngazi ya msaada wa kibinadamu na katika sekta ya usalama. Katika bara la Afrika lenye kambi na operesheni nyingi zaidi za kijeshi, Waafrika wengi wanatambua kwamba Marekani inazichukulia nchi za Afrika kama karata yake katika mchezo wa siasa za kijiografia tu na haina nia ya kuendeleza ushirikiano wa kweli na Afrika."
Russia na Ukraine ni wauzaji wakuu wa chakula kwa nchi nyingi za Afrika, na ikiwa mgogoro kati ya nchi hizo mbili utaendelea, mamilioni ya watu wasio na hatia barani Afrika watakabiliwa na njaa na hata kifo. Marekani isiuangalie mgogoro huu kwa mtazamo wa " Vita vya panzi, faida kwa kunguru ". Hatua za Marekani kuitishia na za kuadhibu nchi za Afrika ili kufikia malengo yake yenye hila hakika hazitafanikiwa. Mbali na hatua hizo kufanya sifa yake ya kimataifa kuendelea kuporomoka, pia zitazidi kudhoofisha uhusiano wake na Afrika.