Kwani hizo fedha ndogo ndogo unazookoa ziko wapi?

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,911
3,385
Rafiki yangu mpendwa,

Kuna watu huwa wanabana sana matumizi, wanakuwa na ubahili mkubwa kwenye fedha zao, lakini bado wanashindwa kujenga utajiri.

Watu hao huwa wanajisifia mbele ya wengine jinsi ambavyo hawana matumizi mabaya na ya anasa. Wamekuwa wanawaona wale wanaokuwa na matumizi makubwa ya fedha zao hawajielewi.

Lakini mwisho wa siku, wote wanakuwa hawatofautiani kwenye upande wa utajiri. Yaani wale ambao ni mabahili bado wanakuwa masikini kama wale ambao wana matumizi makubwa.

Ni sawa na kisa cha mtu aliyekutana na rafiki yake waliyepotezana kwa miaka 20. Wakati wanazungumza akagundua rafiki yake anavuta sigara kila baada ya muda mfupi. Akaamua kumuuliza anavuta pakiti ngapi za sigara kwa siku, akamjibu mbili. Akamuuliza tena pakiti moja ya sigara inauzwa shilingi ngapi, akamjibu elfu 2.


Mtu huyo akakokotoa kwamba kwa siku rafiki yake anavuta shilingi elfu 4, ambayo kwa mwaka ni zaidi milioni 1 na laki 4 na kwa miaka 20 zaidi ya milioni 28. Rafiki huyo akamjibu ni sahihi kabisa.

Basi mtu huyo akaendelea kumshauri kwamba kama asingekuwa anavuta sigara na kuokoa kiasi hicho cha fedha, angekuwa amefanya uwekezaji mkubwa na kunufaika nao.

Rafiki mvuta sigara alisikiliza kwa makini na kukubaliana na mwenzake. Lakini mwisho alimuuliza rafiki yake swali kama anavuta sigara. Rafiki yake alijibu kwa kujivunia kwamba havuti sigara na hawezi kupoteza fedha zake kwa kuzichoma.

Hapo rafiki mvuta sigara alimwuliza mwenzake, kama huvuti sigara, hayo mamilioni uliyookoa kwa hiyo miaka yote ya kutokuvuta yako wapi? Rafiki asiyevuta sigara alibaki mdomo wazi na asiwe na la kujibu.

Rafiki, hiyo ni hadithi yenye funzo, ambayo inabeba sana uhalisia wetu kwenye matumizi ya fedha zetu. Zile fedha ndogo ndogo ambazo tunaweza kuziokoa kwenye matumizi, huwa tunaishia kuzipeleka kwenye matumizi mengine.

Lengo la kuokoa fedha kwa kubana matumizi ni uweze kupeleka fedha hizo kwenye maeneo ambayo zinazalisha zaidi. Lakini kama utaokoa fedha kwenye eneo moja na kuzipeleka kwenye matumizi mengine, hakuna kitu umefanya. Yaani matokeo ni sifuri.

Hata kama unaokoa fedha kutoka kwenye matumizi mabaya na kuzipeleka kwenye matumizi mazuri, bado hujafanya kitu chochote. Unapoamua kujibana na kuachana na matumizi, hakikisha maumivu unayoyapata kwa kuachana na matumizi hayo unayatuliza kwa manufaa unayokuja kupata baadaye.

Tatizo kubwa linalopelekea watu kutumia fedha wanazookoa ni kushindwa kuzitofautisha fedha walizookoa na fedha nyingine za matumizi. Yaani mtu anaweza kuokoa fedha kwenye matumizi fulani, lakini akabaki nazo na kuishia kuzitumia kwenye matumizi mengine.

SOMA; NGUVU YA BUKU; Jenga Utajiri Mkubwa Kwa Kuanza Na Kiasi Kidogo Cha Fedha.

Njia pekee ya kuhakikisha unanufaika na fedha ndogo ndogo unazookoa ni kuzitenga kwa kuziweka mbali kabisa na fedha zako nyingine. Yaani pale unapookoa fedha yoyote ile, unapaswa kuiondoa kwenye mipango yako kabisa ili usiweze kuitumia.

Moja ya njia zitakazokusaidia kuona zile fedha unazookoa ni programu ya NGUVU YA BUKU. Kwenye programu hii unawekeza kiasi kidogo kidogo cha fedha unazookoa kila siku. Kwa kuwa kwenye programu hii, utaweza kuona kila fedha unayookoa na kuiweka mahali ambapo itakua na kuzalisha faida kubwa kwa baadaye.

Kupata nafasi ya kuwa kwenye programu hiyo ili uweze kuokoa fedha na kunufaika nazo, tuma ujumbe NGUVU YA BUKU kwenda namba 0678 977 007.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeeleza kwa kina kuhusu dhana hiyo ya kupoteza fedha ndogo ndogo unazookoa. Pia nimeeleza kuhusu programu ya NGUVU YA BUKU na jinsi inavyoweza kukunufaisha. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho na uchukue hatua ili kujenga utajiri kwa kutumia fedha ndogo ndogo unazookoa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
 
Back
Top Bottom