Kushuka gharama za umeme kuendane na huduma bora

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
HAKUNA ubishi kwamba, kuanza kutumika kwa gesi asilia katika uzalishaji umeme kwa asilimia 70, kumeanza kuleta tumaini jipya kwa Watanzania, wakiamini angalau unafuu wa gharama katika nishati ya umeme sasa itaanza kuonekana.

Hali hiyo imekuja baada ya Serikali kujenga bomba la gesi kusafirisha gesi mpaka Dar es Salaam kwenye mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I na Ubungo. Kutokana na kuanza kutumika kwa nishati hiyo katika kuzalisha umeme nchini, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa nyakati tofauti liliagizwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kuanza utaratibu wa kupunguza bei kwa walaji.

Tanesco waliitikia mwito huo hivi karibuni kuwasilisha katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) mapendekezo ya kutaka kushusha bei ya umeme. Katika maombi yake, Tanesco inaomba kushusha umeme kwa asilimia 1.1 na kuondoa kabisa gharama za maombi ya awali ya wateja wapya na gharama za huduma kwa wateja wa majumbani.

Kwa wale wasiofahamu, gharama za maombi hayo ya awali ambayo pia yanajulikana kama gharama za huduma au maarufu kama ‘service charges’ ni Sh 5,520 kwa mwezi kwa wateja wa majumbani. Kwa walio wengi, haya yamekuwa kama maajabu kwani miaka nenda miaka rudi, tulizoea kusikia Tanesco ikiwasilisha maombi ya kupandisha bei, na si kushusha.

Baada ya mapendekezo hayo ya Tanesco, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Ewura (Ewura CCC), lilieleza kuwa lilitarajia bei hiyo ishuke zaidi. Mwenyekiti wa baraza hilo, Amani Mafuru alisema Tanesco kukubali kushusha bei ya umeme, kutaleta ahueni kwa wateja wake kwani wanaweza kupata huduma kwa gharama nafuu.

Hata hivyo, alisema Baraza hilo linaitaka Ewura kufanya upembuzi yakinifu, ili kupungua kwa bei ya umeme isije ikawa sababu ya shirika hilo kushindwa kujiendesha au kujiendesha kwa hasara.

Alisema kwa mujibu wa hesabu za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2013, Tanesco ilipata hasara ya zaidi ya Sh bilioni 467, hivyo baraza lina wasiwasi kama Tanesco itaweza kujiendesha.

Lakini, Kaimu Mwenyekiti wa Ewura CCC, Thomas Mnunguli, alisema punguzo hilo la bei ya umeme kwa asilimia 1.1 kwa mwaka huu na 7.9 kwa mwaka ujao ni dogo na halitarajiwi kuleta unafuu wowote kwa mtumiaji. Alisema baraza hilo lilitarajia kuwa punguzo hilo lingekuwa kubwa zaidi hasa ikizingatiwa kuwa mazingira ya sasa yanaruhusu bei hizo kushuka zaidi, ikilinganishwa na mwaka 2013 wakati wa bei za sasa zilipopangwa na Ewura.

Alisema kama ombi hilo litakubaliwa, tafsiri yake ni kuwa bei hizo zitaendelea kuwa juu kwa asilimia 38.1 kulingana na bei ya umeme ya mwaka 2013 kabla Ewura haijapandisha bei. Ni dhahiri kuwa kila Mtanzania alikuwa na matarajio kama ya Ewura CCC, kwani mazingira ya kuwepo kwa matumizi ya gesi kwa asilimia kubwa yanapunguza gharama za uzalishaji, tofauti na wakati ambao Tanesco ilitegemea zaidi mitambo ya mafuta katika uzalishaji wa umeme.

Pamoja na kuanza kwa matumizi ya gesi, lakini pia Tanesco imejikita katika ujenzi wa miundombinu, jambo linalozidi kutia moyo kwamba, sasa shirika limejipanga kutoa huduma bora zaidi, lakini pia kwa gharama nafuu. Hata hivyo, pamoja na matarajio waliyonayo Watanzania, ni vyema Tanesco ikaanika uchambuzi yakinifu katika suala hili, ili waelewe ni kwa jinsi gani wananufaika na matumizi ya gesi inayopatikana katika uzalishaji umeme.

Hatua hiyo itasaidia Watanzania kuelewa na kuondokana na matumaini lukuki katika umeme kama walivyokuwa wakitarajia huku wakiangalia jinsi shirika hilo litakavyoweza kujiendesha. Katika hili, ni vyema wizara husika kukaa na Tanesco na Ewura na kuona jinsi watakavyojitokeza hadharani wakati wa kutangazwa rasmi punguzo la umeme ili Watanzania wasibaki na manung’uniko.

Ni dhahiri kuwa, Watanzania watashukuru kwa punguzo hilo ambalo litaleta nafuu kwa kiasi katika matumizi ya umeme, lakini ni vyema wakaelewa lengo la shirika hilo kushusha kwa asilimia hiyo na siyo zaidi.

Zaidi, ni kuipongeza Tanesco kwa kuwafikiria wateja wake na kwa hakika punguzo hilo linakuja katika wakati mwafaka. Naamini hatua hii ya kumpunguzia mteja gharama za umeme itakwenda sambamba na uboreshaji zaidi wa uzalishaji nishati hiyo, ili lengo la kuifanya Tanzania nchi ya viwanda lifikie na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye taifa kwa ujumla.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…