TANZANIA hakuna amani nchini isipokuwa kuna utulivu, hivi ndivyo anavyosema Bunga Dettu, Mchungaji wa Kanisa la Waadventista (Wasabato) Mtaa wa Dodoma, anaandika Dany Tibason.
Mbali na hilo mchungaji huyo anasema “amani ya nchi haiwezi kupatikana kwa kutumia maguvu na mabavu kwa kuwatishia wananchi.”
Katika mkutano huo amesema, kama wananchi hawataweza kupata nafasi ya kutoa dukuduku zao kwa kunyimwa uhuru, kuna uwezekano wa amani kutoweka.
“Lazima ijulikane wazi kuwa wananchi wanataka kuona wanatendewa haki katika kutoa mawazo yao na kutumia rasilimali walizonazo kwa usawa.
“Lakini kama wananchi wataendelea kuona rasilimali za nchi zinatumiwa na watu wachache huku watu wengu wakiendelea kutaabika, kamwe amani haiwezi kuwepo”amesema Mchungaji.
Abrahman Ahmed, Mwakilishi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Ahmaddiya amesema, jumuiya hiyo ipo kwa ajili ya kukuza uhusiano mzuri kati ya jamii na serikali.
Sambamba na hilo amesema, kazi kubwa ya jumuiya hiyo ni kuhakikisha dini zote zinakuwa na uhusiano mzuri katika kudumisha amani na utulivu sambamba na kuliombea taifa na viongozi wake.