Kuna Siku UVCCM Wataomba Serikali Izuie Uingizaji wa Magari.

Bams

JF-Expert Member
Oct 19, 2010
18,696
47,150
Kwa wiki nzima watu wamekuwa wakijadili uwezo wa akili wa baadhi ya viongozi wa UVCCM na baadhi ya viongozi wa dini, kufuatia kauli zao kuwa eti Serikali iufungie mtandao wa X (zamani twitter), kwa vile mtandao huo umeruhusu watumiaji kuutumia kwa masuala yanayohusiana na ngono.

Kauli hiyo imethibitisha jinsi CCM ilivyo kwenye janga kuu. Kama mwenyekiti wa UVCCM anaweza kuwa na upeo duni kiasi hicho, vipi hao UVCCM members wa kawaida? Halafu cha ajabu ni kuwa kwa ujinga mkubwa kama huu alio nao huyo kiongozi, kesho utasikia naye huyu kateuliwa kuwa kiongozi wa Serikali. Kweli nchi itapiga hatua kwa aina ya viongozi wenye uelewa duni kama huyu?

Kwa upeo mdogo na duni kabisa wa kiongozi huyu, leo hii ikitokea mtu akamwua mwenzake kwa kumchoma kisu, ataiomba Serikali izuie biashara ya visu. Na ikitokea kukawa na dereva wa gari aliyepagawa, kwa makusudi akawagonga watembea kwa miguu, ataiomba Serikali izuie uingizaji wa magari nchini kwa sababu yanaua watu!! Hapo ndipo ulipoishia uwezo wa akili ya mwenyekiti wa UVCCM.

Mtandao wa X ni wa kimataifa, siyo wa Tanzania. Upo kwaajili ya kukidhi mahitaji ya kila mtumiaji kwa khzingatia mahitaji na mazingira yake.

Wewe mtumiaji ndiye unaamua uutumie kwa namna gani kwa kuzingatia sheria za nchi yako, mahitaji na desturi za jamii yako. Na kama sheria za nchi yako zinazuia masuala ya ngono kuwekwa wazi, wewe ukaenda kuweka picha za ngono kwenye mtandao wa X, ukidakwa na kushtakiwa, huwezi kujitetea kuwa eti twitter waliruhusu.

Vijana hawa wa CCM, tabia za uchawa naona zinazidi kuwadunisha kabisa uwezo wa kufikiri, maana uchawa hauhitaji akili. Mazoea ya kutotumia akili, yanawapeleka kwenye tabia. Mtu kumwua mwanadamu mwenzake kwa kisu, tatizo siyo la kisu, bali mtumiaji kisu. Mtu kumwua mwanadamu mwenzake kwa makusudi kwa kumgonga na gari, tatizo siyo la gari, bali la mwendeshaji gari. Mtu kumwua mwenzake kwa kumwekea sumu iliyokusudiwa kuwaua wadudu waharibu wa mazao, tatizo siyo la sumu, bali mtumiaji. Na kwa mwenye akili hawezi kuthubutu kushauri dawa zote za kuua wadudu zisitengenezwe kwa sababu zimemwua mtu. Halikadhalika, kuitumia mitandao ya kijamii kukiuka sheria za nchi na maadili ya jamii husika, tatizo siyo la mtandao bali mtumiaji.

Kwa hoja ile ya mwenyekiti wa UVCCM, kwa hakika Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia atakuwa anajisikitikia huko aliko, kwa kuona aina ya vijana alio nao.

Watanzania tuendelee kuitumia mitandao yote ya kijamii kwa tija, tuwapuuze kabisa watu wasiojielewa wala kujitambua kama huyo mwenyekiti wa UVCCM. Siamini kama kuna yeyote mwenye akili timamu ndani ya Serikali atapoteza muda wake kufikiria hilo ombi la huyo mwenyekiti wa UVCCM.

Ushauri
UVCCM, mnapochagua viongozi, ni vyema mkawa mnawatafuta watu waliokamilika kiupeo, akili, hekima, na uwezo wa kutafakari. Mnapokuwa na viongozi wasiojielewa, wanaidhalilisha taasisi nzima na kuifanya ionekane ni ya watu wasiojitambua wala kujua Ulimwengu unaenda wapi.
 
Tatizo la UVCCM ni uwoga

UVCCM ilikuwa moto wakati ule wa akina Uhalula, Nchimbi, Nape nk siyo hawa madogo wa Leo 🐼
 
Tatizo la UVCCM ni uwoga

UVCCM ilikuwa moto wakati ule wa akina Uhalula, Nchimbi, Nape nk siyo hawa madogo wa Leo
Ni kweli. Kuna wakati UVCCM ilikuwa na watu wanaojitambua. Na hata wakuu wa CCM waliwaheshimu. UVCCM siku hizi, inaonekana ni ya wenye njaa waviziaji wa makombo ya wenye uwezo.
 
Back
Top Bottom