Katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo katika jukwaa la JamiiForums.com, kumekuwa na majadiliano na masuali yanahoji au kutoa taarifa ambazo wengi hawana uthibitisho nazo kuhusu dawa za kuzuia maambukizi ya VVU ambazo muhusika anatakiwa kutumia ndani ya masaa 72. Je, hili lina ukweli? Na inakuaje kwa muhitaji ambaye si muhanga, na gharama zake zikoje?
Je, kuna ukweli kwenye hili?
- Tunachokijua
- Njia ya kukukinga usipatwe na maambukizi ya VVU baada ya kupitia mazingira au hali hatarishi ipo. Kitaalamu huitwa Post-exposure prophylaxis, au kwa kifupisho PEP.
Kwa mujibu wa Miongozo ya Matibabu na Orodha ya Kitaifa ya Dawa Muhimu Tanzania Bara iliyotolewa na Wizara ya Afya mwaka 2021, PEP ni utumiaji wa haraka wa dawa ili kuzuia maambukizi kufuatia mazingira ambayo mtu anadhani yanaweza kumsababishia kupata maambukizi ya VVU (Mfano: kugusana kwa damu au maji maji mengine ya mwili).
PEP inasaidia kupunguza hatari ya kupata maambukizi. Hata hivyo, inaelezwa kuwa inapaswa kuanza PEP ndani ya saa 72, au siku 3, baada ya kuambukizwa au kuhisi kuambukizwa VVU, la sivyo haitafanya kazi.
Mtu aliyepitia mazingira hatarishi yanayoweza kumfanya aambukizwe VVU anapaswa kufika kwenye hospitali yoyote ya serikali ili apatiwe msaada, pamoja na kupimwa kwanza kama tayari ni muathirika wa VVU au la.
Dozi ya mwanzo inapaswa kutumiwa ndani ya saa 2 baada kuhisi kuambukizwa na kabla ya kumpima mtu mwenye mashaka.
Kwa Tanzania, TDF 300mg+3TC 300mg+DTG 50mg au maarufu zaidi kama TLD ndiyo dozi ya dawa inayotumika kwa watu wazima. Kwa watoto, AZT+3TC+LPV/r ndiyo hutumika.
Muongozo huo wa Wizara pia unaonesha kuwa dozi hiyo hutumiwa na watu wazima kwa kidonge kimoja kila siku kwa muda wa siku 28, huku kwa watoto ikitumiwa mara mbili kwa siku katika muda wa siku hizohizo 28.