Kizazi Kilichodanganywa na Likes na retweet......

Paspii0

JF-Expert Member
Apr 10, 2020
479
685
Kwa heshima na uzito mkubwa wa kiakili na kijamii, natangaza kwa sauti ya wazi na isiyoyumba kuwa vijana wengi wa kizazi hiki wanapoteza dira, maadili na mwelekeo wa maisha. Tunaushuhudia ushindi wa ujinga dhidi ya hekima, ushindi wa starehe dhidi ya juhudi, na zaidi ya yote, ushindi wa mitandao ya kijamii dhidi ya dhamira ya kweli ya maisha.

Visungura, pombe kali zinazouzwa Na kupatikana kwa urahisi, zimegeuka kuwa nembo ya ujasiri wa kijinga miongoni mwa vijana. Ni pombe zinazoua bila risasi, zinapumbaza akili na kuzima ndoto kwa kasi ya ajabu. Vijana wamegeuka mateka wa uteja wa kisasa, wakidhani ulevi ni sehemu ya maisha ya mafanikio. Hawajui kuwa huko ndiko kwenye kaburi la uwezo wao wa kufikiri na kujenga kesho.

Kamari na kubeti, vinavyohamasishwa na mabango, vipindi vya runinga, na mitandao ya kijamii, vimegeuza vijana kuwa wapangaji wa bahati badala ya kuwa watengenezaji wa fursa. Wanaamini fedha inatoka kwa kubahatisha si kwa maarifa, si kwa bidii, si kwa maadili. Jamii inavuna vijana waliopoteza nidhamu ya kazi, wakijenga tabia ya kukwepa ugumu na kutegemea bahati, hali inayozalisha taifa legevu kiuchumi na kimaadili.

Shisha, moshi wa starehe unaovuta maisha ya vijana polepole, umepewa heshima isiyostahili. Wanaiona kama alama ya usasa, kumbe ni kifaa kinachochoma afya zao taratibu. Ushahidi wa kisayansi uko wazi, uvutaji wa shisha una athari mbaya zaidi ya sigara za kawaida, na ni chanzo kikuu cha matatizo ya kupumua na saratani ya mapafu.
Tatizo si visungura pekee, si kamari pekee, si shisha pekee tatizo ni mfumo wa fikra ulioharibika. Mfumo unaohamasisha maisha ya kufuata mkumbo, ya kupenda raha kuliko kazi, ya kuchagua njia ya mkato badala ya ujenzi wa polepole wa mafanikio halisi,Hali hii haipaswi kuvumiliwa,Hii si hulka ya kijana wa Kiafrika,Si njia ya kuendeleza taifa,Si tabia ya mtu mwenye dhamira ya kweli ya kubadilisha dunia.

Ni wajibu wa kila taasisi ya kielimu, kila kiongozi wa dini, kila chombo cha habari na kila shirika la kijamii kuchukua hatua ya wazi na makusudi kurekebisha hali hii. Ni lazima tuanzishe mapinduzi ya kifikra, ambayo yatawafanya vijana waelewe kuwa,

Maisha hayajengwi kwa starehe, bali kwa maarifa, nidhamu na kazi ya kweli.
Sitaki kuomba. Sitaki kusihi. Natamka kwa msimamo wa kisomi.
Kama hatutarekebisha kizazi hiki, tutajenga majengo yasiyokuwa na wakazi wenye thamani. Tutakuwa na digrii nyingi, lakini busara sifuri. Tutakuwa na vijana wengi lakini taifa lisilo na uhai.


Muda wa kutenda ni sasa.

-Chavalikungu
Mtafiti wa Maendeleo ya Jamii
 

"Kizazi Kilichodanganywa na Likes na retweet......"​

Kichwa cha habari na yaliyoelezwa ni vitu tofauti. Nilifikiri nitakutana na uraibu wa mitandao ya kijamii.
 
Back
Top Bottom